
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji wetu. Katika makala iliyopita tulijifunza juu tuliangalia changamoto Ushindani usio na tija. Leo hii tunaangalia juu ya changamoto ya Masomo Usiyoyahitaji. Karibu sana.
Tunaendelea kuzichambua changamoto ambazo zipo ndani ya mfumo wa elimu na jinsi zinavyoweza kuathiri wanafunzi ambao tunatarajia kuwa wazalishaji katika taifa lolote ili kujiletea maendeleo.
3. Changamoto ya Masomo Usiyoyahitaji
Kuna siku moja niliamua kutafakari juu ya safari yangu ya masomo tangu awali mpaka sasa. Nilijaribu kuorodhesha masomo mbalimbali niliyosoma angalau kuanzia kidato cha kwanza. Nilishangazwa na msururu wa masomo ambayo hata mimi sikudhani kama niliwahi kusoma na kufanya vizuri. Lakini leo hii masomo yale ni kiasi kidogo sana ninayatumia maarifa yake kwenye maisha yangu.
Hali hii ipo kwa watu wengi au mfumo wetu unatuandaa hivyo. Wewe peke yako jaribu kuangalia idadi ya masomo au ‘course’ ulizosoma tangu sekondari tu mpaka sasa uone ni kwa kiasi gani masomo haya unayatumia kwenye maisha yako ya kila siku.
Tunayo haja mara kwa mara kuitafakari hasa maana ya elimu ambayo niliwahi kuiandika kwenye mfululizo wa makala hizi. Kwa kurejea ningependa kuinukuu
‘ni kitendo au mchakato wa kupata jumla ya maarifa, kukua kwa uwezo wa kufikiri au kuamua na kujiandaa binafsi kimaisha’
Kwa kifupi elimu unaweza kusema ni mfumo wa taarifa unazozihitaji wewe binafsi ili kupata maarifa yatakayokusaidia katika safari yako binafsi ya kimaisha. Msisitizo wa tafsiri hii ni kuwa elimu ili iwe imefikia lengo lake ni lazima ikunufaishe wewe binafsi ili na wewe uweze kuinufaisha jamii. Hatahivyo, kwa jinsi mfumo ulivyokaa ni kama tunabahatisha juu ya utoaji wa elimu ndio maana tunalundika masomo mengi kwa wanafunzi ili yumkini kuna kitu ataambulia ili kimsaidie. Hapa tunakosea sana na kupoteza muda.
Tunaweza kuona nyakati hizi hasa shule za msingi ‘english academy’ zinavyorundika masomo mengi kwa watoto wadogo. Unaweza kuona mtoto wa chini ya darasa la 3 ana masomo takribani 10. Ni kweli tunaweza kusema watoto wana uwezo mzuri wa kujifunza lakini mtazamo wangu wanapaswa kujifunza vitu vicheche kwa undani zaidi. Mfano ningependelea mtoto wa chini ya darasa la 3 kujifunza zaidi juu ya KUSOMA, KUANDIKA na KUHESABU. Nguvu nyingine ipelekwe katika kuvumbua vipaji vyake ili vije kumsaidia zaidi.
Nikupe changamoto ndugu msomaji, kagua vyeti vyako angalia kozi au masomo uliyosoma katika ngazi za sekondari au chuo ni masomo mangapi kwa sasa unaweza kuyatumia kuleta manufaa kwako na kwa jamii?
Nikuhakikishie unaweza kukuta ni chini ya 5% ya kile ulichojifunza darasani kwa miaka yote ndicho unatumia kwa sasa. Tutafute namna ya kuwasidia watoto na vijana wetu kujifunza kwa ajili ya safari za maisha yao binafsi na si kile mitaala inachotaka kuwalisha.
‘Mungu ibariki Afrika’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Ni ukweli usiopingika kabisa, nimejaribu kuvuta picha kidogo tu na kuona kuwa tumejazwa vitu visivyo na maana na ktk mfumo huo pia tunaoutumia ndio unaoperekea watu kuchagua kusomea vitu kwa kubahatisha mean mbali kabisa na ndoto yake…. Tunajazwa story za kinjekitile ngwale stor za kina mabara the farmer sijui kina Three suitors one husband until now sijui ndayatumia wap haya!? In fact we need changes..????
Karibu sana Victor ni kweli tunayo changamoto kubwa ya mfumo huu lakini lipo tumaini kwa kizazi hiki kama watatumia fursa kubwa ya teknolojia iliyopo kujifunza vitu wanavyotaka.