
Utangulizi
Katika mwendelezo wa makala hizi za Mtazamo wa Kiroho kuhusu Corona Virus (Covid – 19) tunaona juu ya dunia nzima kuingia katika mashaka makubwa kutokana na kasi ya maambukizi ya ugonjwa huu. Changamoto kubwa imeendelea kuwa ukosefu wa tiba au chanjo ya kumaliza ugonjwa huu. Kila mmoja yupo katika hatua za kujiadhari kutokana na ugonjwa huu na wito upo duniani kote kutafuta suluhisho. Kila sekta ya kimaisha imeathiriwa kwa sehemu kubwa, hali ya kiroho, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na afya za wanadamu zimebadilika sana. Nchini kwetu Tanzania tunaendelea kuchukua taadhari ili kupunguza kasi ya maambukizi. Kasi ya maambukizi inaendelea kila siku na hofu kuu imetanda dunia yote, hakuna wa kumsaidia mwenzake. Makala iliyopita tulingalia juu ya ‘Waathiriwa wa adhabu’. Leo tunaangalia suala la Sababu ya Adhabu. Karibu tujifunze.
Hatua ya 3
Chunguza Sababu ya Adhabu
‘BWANA akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimepachagua kuwa nyumba ya dhabihu. Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa’. 2.Nya.7:12 – 15
Katika mfululizo wa makala ambazo tumekuwa tukijadili kuhusu mtazamo wa kiroho wa Corona Virus, tumejifunza kuanzia hatua ya kwanza ya kufahamu Asili au Aina ya Adhabu, kisha hatua ya pili tumejifunza juu ya Aina ya waathiriwa wa Adhabu. Sasa tunajifunza juu ya sababu au chanzo cha adhabu. Ni nini kimepelekea adhabu hiyo kuletwa kwa jamii au ulimwengu?
Maandiko haya tuliyonukuu yanaonesha juu ya aina 3 za adhabu ambazo Mungu amezitangaza juu ya nchi;
- Ukame – kwa kuzifunga mbingu isiwe mvua
- Uharibifu wa mazao – kwa kuamuru nzige kula nchi, na
- Tauni – ugonjwa wa kuambukiza kwa watu
Je, ni mazingira gani yanayopelekea adhabu hizi juu ya nchi au jamii katika eneo?
Kwa hali ya kawaida watu hutarajia mambo mema kutoka kwa Mungu ambaye siku zote hutuvumilia katika maisha yetu ya udhaifu. Lakini inapotokea hali ya matatizo ambayo yanatokea katika jamii hasa kuhusiana na tabia nchi au aina za magonjwa ambayo hakuna tiba, hapo watu huanza kujiuliza ni kitu gani kimetokea katika maisha yao.
Ukiendelea kusoma kile ambacho Mungu alimsemesha Mfalme Sulemani
…ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya…
Tunaweza kuona dhahiri sababu ya adhabu yoyote ambayo inatekelezwa juu ya nchi au kwa jamii ni matokeo ya NJIA MBAYA za wanadamu.
Tunaweza kuona suala hili la NJIA MBAYA au UOVU au DHAMBI juu ya nchi zinaweza kumkasirisha Mungu kiasi cha kuachia adhabu juu ya mtu, familia, ukoo, eneo, taifa au hata dunia nzima. Maandiko yanathibitisha haya kizazi hata kizazi tangu mwanadamu alivyoasi mbele za Mungu pale Eden.
Tunaweza kuona baadhi ya mifano ya NJIA MBAYA ambazo zilisababisha adhabu kwa watu na maeneo mbalimbali katika maandiko matakatifu.
Mfano. 1. Kisa cha Nuhu na Gharika
‘Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao, wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wo wote waliowachagua. BWANA akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini….BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote. BWANA akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo. BWANA akasema, Nitamfutilia mbali usoni pa nchi; mwanadamu na mnyama, na kitambaacho na ndege wa angani; kwa maana naghairi ya kwamba nimewafanya. Lakini Nuhu akapata neema machoni pa BWANA’ Mwa.6:1 – 8
Hii ni habari ambayo wengi tunaifahamu sana na tumejifunza kwa muda mrefu tangu utoto wetu. Tunafahamu juu ya gharika yaani mvua ya siku 40 mchana na usiku jinsi ilivyoangamiza kila kitu kilichokuwa na uhai yaani binadamu na wanyama na ndege wa angani isipokuwa Nuhu na familia yake jumla ya watu 8 na viumbe vilivyoachwa kama mbegu ndani ya Safina.
Dunia imeshapitia majanga makubwa sana kuliko hili la Corona linalotukuta sasa, lakini changamoto yetu sisi binadamu hatujifunzi kutokana na makosa ya wale waliotutangulia.
Sababu kubwa ambayo ilipelekea maangamizi haya makubwa juu ya wanadamu na viumbe vyote ni UOVU wa wanadamu. Kabla ya hapo wanadamu walikuwa na uwezo wa kuishi muda mrefu mpaka miaka 900 lakini hali ya MAOVU ilimfanya Mungu atoe adhabu ya kupunguza miaka mpaka 120. Lakini bado haikutosha, wanadamu walizidisha uovu kiasi kwamba ADHABU ilienda kwa watu wote bila kujali kama ni watoto wachanga, vijana, wazee, wazima, wagonjwa, walemavu, wanyama, wadudu n.k.
Huyu ndiye Mungu ambaye ALIKUWAKO, YUPO na ADUMU MILELE, sifa yake HABADILIKI.
Tujiulize kama Mungu aliweza kufanya hivyo kwa wanadamu na kubakisha watu 8 tu katika dunia ya wakati huo yaani familia 1 tu katika dunia nzima, je tunadhani hawezi tena kuadhibu? Adhabu ile ilikuwa KUBWA mno kiasi ilimuhuzunisha Mungu mpaka akaapa kutokuadhibu kwa namna hiyo tena. Lakini hii haiondoi sifa yake ya kuwa Mungu.
Je, MAOVU au NJIA MBAYA walizofanya wakati wa Nuhu zilikuwa zaidi ya zile ambazo sasa zinafanyika? Nadhani majibu yetu tunayo, sisi wa kizazi hiki tumejawa zaidi na UOVU na NJIA MBAYA kiasi kwamba waliotangulia wangelistahili rehema kuliko kizazi hiki.
Maombi ya leo
Ee, Mungu Baba uliyeziumba mbingu na nchi na vyote ndani yake, unayejua majira na nyakati za maisha ya wanadamu kizazi na kizazi, tunakushukuru kwa neema yako ya uhai uliyotupatia leo. Uwepo wetu siku ya leo si kwamba sisi ni wema kuliko waliotangulia mbele zetu katika kizazi kilichopita ila kwa rehema zako ndio maana tupo mpaka sasa, tunakuomba utujalie kufahamu Uovu wetu na njia zetu mbaya ili tujipatie moyo wa toba, tusiangamie sisi na kizazi chetu katika Jina la Mwana wako Yesu Kristo utusikie na kuturehemu. Amen
# Sauti ya Matumaini # Toba ya Dunia
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!