
Utangulizi
Katika mwendelezo wa makala hizi za Mtazamo wa Kiroho kuhusu Corona Virus (Covid – 19) tunaona juu ya dunia nzima kuingia katika mashaka makubwa kutokana na kasi ya maambukizi ya ugonjwa huu. Changamoto kubwa imeendelea kuwa ukosefu wa tiba au chanjo ya kumaliza ugonjwa huu. Kila mmoja yupo katika hatua za kujiadhari kutokana na ugonjwa huu na wito upo duniani kote kutafuta suluhisho. Kila sekta ya kimaisha imeathiriwa kwa sehemu kubwa, hali ya kiroho, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na afya za wanadamu zimebadilika sana. Nchini kwetu Tanzania tunaendelea kuchukua taadhari ili kupunguza kasi ya maambukizi. Kasi ya maambukizi inaendelea kila siku na hofu kuu imetanda dunia yote, hakuna wa kumsaidia mwenzake. Makala ya iliyopita tuliangalia juu ya upana wa maandiko ya 2.Nyak.7:13 – 14. Katika makala ya leo tunaanza kujifunza Hatua muhimu za kuchukua ili kushughulikia pigo katika jamii. Karibu tujifunze.
Hatua Muhimu za kuchukua ili kushughulikia Pigo
Kama tulivyoanza katika makala ya Siku ya 4 kwa kuangalia upana wa maandiko ambayo tumekuwa tukinukuu kutoka 2.Nyak.7:13 – 14 ambapo tumeona umuhimu wa kuisoma na kutafakari ujumbe mzima wa mazungumzo baina ya Mungu na Mfalme Sulemani katika Sura ya 6 – 7. Ukisoma sura hizi mbili unapata angalau mtiririko mzuri wa mazungumzo haya. Leo tunaanza kuziangalia hatu muhimu zinazopaswa kuchukua kwa waombaji katika kushughulikia pigo au janga katika jamii. Nitanukuu tena maandiko haya ili kupata ufafanuzi wa kila hatua.
‘BWANA akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimepachagua kuwa nyumba ya dhabihu. Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa’. 2.Nya.7:12 – 15
Hatua ya 1
Ifahamu asili na aina ya adhabu
‘Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni…’
Hii ni hatua ya kwanza ambayo waombaji au Kanisa wanapaswa kuijua yaani aina za adhabu. Maandiko yanaeleza wazi juu ya aina za adhabu ambazo Mungu anaweza kuachilia katika eneo au jamii. Hapa anataja wazi juu ya adhabu juu ya majira na hali ya hewa kiasi cha kuleta ukame katika eneo na kusababisha njaa, pia anazungumzia adhabu ambayo inakwenda kuathiri mazao ya nchi kupitia nzige na aina ya adhabu ambayo inapelekea kuangamia kwa watu kwa ugonjwa wa kuambukiza.
Kwa hali ya kawaida inatarajiwa ya kuwa Mungu asizuie mvua au aachilie mvua kwa majira na kiasi chake juu ya nchi, hali kadhalika Mungu anatarajiwa kulinda mazao ya nchi ya watu wake na uhai wao. Ila kipo kinachosababisha Mungu kufanya kinyume chake na kuachilia madhila juu ya watu wake. Hivyo jambo muhimu la kwanza ambalo linaonekana kwa nje ni madhara tunayopata wanadamu aidha katika ukame, au baa la njaa au ugonjwa wa kuambukiza.
Hatua hii inatuonesha ishara ya nje au ishara ya kimwili ya kuwa tayari katika ulimwengu wa kiroho kuna namna fulani watu wamemkosea Mungu. Sasa inawezekana sayansi ina namna ya kuelezea mambo yake kuhusu ukosefu wa mvua au wingi wa mvua kupitiliza kiasi, sote tunasikia tabiri za hali ya hewa na suala zima ya mabadiliko ya tabia nchi. Inawezekana sayansi ina namna yake ya kuelezea suala la nzige kuharibu mazao na kutafuta dawa za kunyunyiza ili kupambana na nzige hao, halikadhalika sayansi ina namna yake ya kuelezea ugonjwa wa tauni au ugonjwa wa kuambukiza juu ya asili yake na namna ya kukabiliana nao. Lakini ni muhimu sana mtu wa Mungu na mwombaji kufahamu pia maandiko yanaeleza nini juu ya matatizo haya katika jamii.
Sisi ni mashahidi wa mabadiliko ya hali ya hewa katika nyakati hizi, pia hivi karibuni tumesikia juu ya kundi kubwa la nzige ambalo lilishambulia baadhi ya maeneo Afrika Mashariki na Kati na hali kadhalika sasa tupo katika janga la Corona ambalo limeathiri dunia nzima. Hizi ni ishara katika ulimwengu wa kimwili ya kuwa kuna tatizo katika hali ya kiroho juu ya maeneo fulani.
Tunaweza kujifunza ukweli huu kupitia kisa cha Mfalme Daudi na baa la njaa katika nchi ya Israel wakati wa uongozi wake.
‘Kulikuwa na njaa siku za Daudi muda wa miaka mitatu, mwaka kwa mwaka; naye Daudi akautafuta uso wa BWANA. BWANA akasema, Ni kwa ajili ya Sauli, na kwa nyumba yake yenye damu, kwa kuwa aliwaua hao Wagibeoni’ 2.Sam.21:1
Hii ni habari ya kuwepo kwa baa la njaa au ukame katika nchi ya Israel wakati Daudi akiwa Mfalme. Daudi alikuwa mfalme wa pili wa taifa la Israel baada ya kutawala Mfalme Sauli ambaye alitawala kipindi cha miaka 40. Kwa kuisoma habari hii utaona ya kuwa kipindi Sauli ni mfalme aliwaangamiza kabila moja ya Wagibeoni ambao ni masalia ya Waamori waliokuwa na kiapo baina yao na wana wa Israel ya kuwa hawataangamizwa bali wataendelea kukaa katika mipaka ya Israel. Lakini Sauli aliwaangamiza baadhi yao. Kipindi chake cha utawala kikaisha na Daudi kuingia madarakani kisha baa la njaa likaingia katika nchi kwa miaka 3 mfululizo. Baada ya Daudi kufanya maombi na kuutafuta uso wa Mungu ndipo Mungu anamweleza sababu iliyosababisha nchi kupigwa na njaa. Unaweza kukisoma kisa hiki kuanzia 2.Sam.21:1 – 14.
Lakini tunaweza kujifunza mambo kadhaa katika kisa hiki
- Kila changamoto katika eneo au jamii huwa na chanzo chake. Jinsi changamoto inavyoonekana kimwili ina asili yake katika ulimwengu wa kiroho
- Namna bora ya kuanza kutatua changamoto ya kimwili ni kushughulikia asili ya changamoto iliyopo rohoni.
- Hatua muhimu ni kuutafuta uso wa Mungu mapema kabla madhara hayajawa makubwa na kuharibu kabisa jamii.
- Maelekezo ya kiroho utakayopata unapaswa kuyafanyia kazi ili kuleta mabadiliko katika ulimwengu wa kimwili.
Tunaona taifa liliingia katika ukame kwa muda wa miaka 3 mfululizo kwa kosa la kiongozi aliyetangulia. Si watu wengi katika taifa wangedhani ya kuwa wapo katika njaa kwa sababu ya makosa ya Mfalme Sauli fulani. Hii itupe picha ya kutusaidia wakati huu namna bora ya kushughulikia changamoto tunayokabiliana nayo ambayo kwa sasa imeikumba dunia nzima.
Ni dhahiri sasa wa kizazi hiki na wa karne hii ya 21 kuna mahali tumekosea ndio maana madhila haya yameletwa katika kila taifa na kila kabila, rangi, jinsia n.k hakuna mahali ambapo hapajaathiriwa na hali hii.
Ukisoma habari hii ya kisa cha njaa wakati wa Mfalme Daudi ule mstari wa 14 baada ya kufahamu chanzo cha tatizo na kufuata masharti ya kushughulikia ndipo Mungu hapo baadae aliiridhia nchi yaani majira ya nchi yakarudi katika hali yake ya utele wa chakula. Unaweza ukadharau au usielewe haya mambo yanavyofanya kazi lakini kwa hakika yanafanya kazi. Mungu ndiye aliyeziumba mbingu na nchi ana uwezo wa kujua sababu na asili ya changamoto tunazopitia majira haya na ana uwezo wa kutusaidia ila tunalo jukumu kama la Mfalme Daudi kuutafuta USO wa BWANA katika majira haya ili atuoneshe chanzo na asili ya adhabu hii na kujipatia moyo wa hekima na unyenyekevu wa toba.
Maombi ya leo
Ee, Mungu Baba uliyeziumba mbingu na nchi na vyote ndani yake, unayejua majira na nyakati za maisha ya wanadamu kizazi na kizazi, tunakushukuru kwa neema yako ya uhai uliyotupatia leo. Tunaokusihi utusamehe kwa kuomba pasipo kutafuta uso wako kwa nia ya kujua asili ya tatizo hili. Tunaomba Roho Mtakatifu atusaidie kufahamu nini hasa asili ya janga hili na kosa letu ili tuweze kufanya toba ya kweli katika Jina la Mwana wako Yesu Kristo tunakusihi. Amen
# Sauti ya Matumaini # Toba ya Dunia
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!