
Utangulizi
Katika mwendelezo wa makala hizi za Mtazamo wa Kiroho kuhusu Corona Virus (Covid – 19) tunaona juu ya dunia nzima kuingia katika mashaka makubwa kutokana na kasi ya maambukizi ya ugonjwa huu. Changamoto kubwa imeendelea kuwa ukosefu wa tiba au chanjo ya kumaliza ugonjwa huu. Kila mmoja yupo katika hatua za kujiadhari kutokana na ugonjwa huu na wito upo duniani kote kutafuta suluhisho. Kila sekta ya kimaisha imeathiriwa kwa sehemu kubwa, hali ya kiroho, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na afya za wanadamu zimebadilika sana. Nchini kwetu Tanzania tunaendelea kuchukua taadhari ili kupunguza kasi ya maambukizi. Kasi ya maambukizi inaendelea kila siku na hofu kuu imetanda dunia yote, hakuna wa kumsaidia mwenzake. Makala ya iliyopita tulitaadharisha ya kuwa ‘Janga hili ni letu sote’. Leo tunaanza kujifunza juu ya upana wa maandiko ya 2.Nyak.7:13 – 14. Karibu tujifunze.
Fahamu upana wa maandiko ya 2.Nyak.7:13 – 14
Mwanzoni mwa mfululizo wa makala hizi, nilieleza wazi juu ya hitaji la watu kuingia katika toba ya kweli kwa sababu ya dhambi na makosa. Nilinukuu maandiko kutoka 2.Nya.7:13 -14 ambayo yameendelea kunukuliwa na kutumiwa na waombaji wengi duniani kumsihi Mungu kutuondolea janga hili.
‘Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao’ 2.Nyak.7:13 – 14
Jambo muhimu ambalo tunapaswa kulifahamu hasa ni maana ya maneno haya na kwa namna gani yanaakisi suala ambalo linaikumba dunia kwa sasa. Haitoshi tu kukariri mistari hii na kuambiana tuitumie kwenye maombi bila kufahamu ina maana gani kwetu sisi na kwa namna gani tunaweza kuielewa na kuitumia kupata msaada wa Mungu tunaouhitaji wakati huu. Hivyo katika mfululizo unaofuata tutaangalia tafsiri za maandiko haya ili yaweze kuwa msaada kwetu katika majira haya.
Habari ya 2.Nya.7:13 -14
Watu wengi wanaisoma mistari hii bila kufahamu asili yake na upana wa maandiko haya. Uli uweze kuupata ujumbe mahsusi katika 2.Nya.7:13 -14 ni lazima uanze kusoma angalau tangu 2.Nya. 6 – 7. Yaani kitabu cha 2 cha Nyakati kuanzia sura ya 6 mpaka 7. Hapa ndipo unaona mtiririko mzima wa habari hii na maana ya maneno hayo ambayo yanatumika kwenye toba kwa sasa.
Mlango wa 6 unazungumzia sala ya Mfalme Sulemani mara baada ya kumaliza kuijenga nyumba ya BWANA wakati wanaiweka wakfu. Mfalme aliomba mambo mengi katika sura hii akieleza endapo wana wa Israel watamkosea Mungu katika mazingira mbalimbali basi Mungu asikie maombi yao na kusamehe. Pia endapo atakuja mgeni kuomba katika nyumba ile Mungu amsikie mgeni huyo ili dunia nzima wapate kumjua Mungu na kumcha kama taifa la Israel.
Mlango wa 7 unaonesha kile kilichotokea mara baada ya Mfalme Suleimani kufanya maombi, moto wa Mungu ukashuka kutoka mbinguni na kuteketeza sadaka na wakaendelea kwa sherehe za kufanya wakfu nyumba ya Mungu. Ndipo 2.Nya.7:12 maandiko yanaeleza juu ya BWANA kumtokea Mfalme Sulemani kujibu maombi yake akisema;
‘BWANA akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimepachagua kuwa nyumba ya dhabihu. Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa’. 2.Nya.7:12 – 15
Lakini pia kuanzia 2.Nya.7:19 – 22, Mungu anatoa maonyo kwa watu wake Israel endapo watamwacha Mungu kwa kutokuzishika amri zake na kuenda kutumikia miungu mingine na kuiabudu ndipo atakapoachilia uovu kati yao na kuwaondoa mahali pao.
Hivyo inatupasa kwanza tuelewe mazingira au upana wa mazungumzo waliyofanya Mfalme Sulemani na Mungu ambayo yalizalisha mistari hii ya 2.Nya.7:13 – 14, ili tunapotaka kuitumia tuweze kujua kwa hakika ni kwa nini tunaitumia katika mazingira haya.
Kwa kuzisoma kwa umakini sura ya 6 – 7 katika Nyakati 2 tunaweza kuona juu ya maombi ambayo Mfalme Sulemani aliyaomba kama akiba kwa ajili ya watu wa Mungu katika taifa la Israel au wageni yaani mataifa endapo watakuwa na mahitaji au endapo kuna makosa wametenda basi maombi hayo yaweze kuwasaidia pale watakapotambua makosa yao na kuchukua hatua stahiki.
Ili tuweze kuingia kwenye maombi sahihi ya toba kwa kutumia maandiko haya na mengine kadri Mungu atakavyotujalia tujipe muda wa kusoma habari hii na kuitafakari kwa kina ili kuyatambua makosa yetu na nini hasa kimesababisha pigo hili ambalo limeikumba dunia yote.
Bwana Yesu atujalie roho ya hekima na ufunuo katika kuyajua mapenzi na makusudi yake kwa Kanisa lake na ulimwengu wote tunapotafakari maneno haya.
Nikusihi mtu wa Mungu pata muda wa kusoma na kutafakari maneno kutoka 2.Nya. Sura ya 6 na 7 huku ukimwomba Mungu atujulishe dhambi yetu na kosa letu, tuweze kujitwalia moyo wa unyenyekevu na toba ya kweli.
Maombi ya leo
Ee, Mungu Baba uliyeziumba mbingu na nchi na vyote ndani yake, unayejua majira na nyakati za maisha ya wanadamu kizazi na kizazi, tunakushukuru kwa neema yako ya uhai uliyotupatia leo. Tunakushukuru kwa ajili ya neno lako la kutuongoza katika maombi na toba kwa ajili yetu binafsi, taifa letu na ulimwengu mzima. Tunakusihi utujalie Roho ya Ufunuo na hekima ili maarifa ambayo unayatoka katika neno lako tuweze kuyatumia kwa ajili yetu na kizazi chetu kipate msaada wako kama wengine waliotangulia walivyopata msaada wako, tunaomba haya katika Jina la Bwana Yesu Kristo. Amen
# Sauti ya Matumaini # Toba ya Dunia
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!