
Utangulizi
Katika mwendelezo wa makala hizi za Mtazamo wa Kiroho kuhusu Corona Virus (Covid – 19) tunaona juu ya dunia nzima kuingia katika mashaka makubwa kutokana na kasi ya maambukizi ya ugonjwa huu. Changamoto kubwa imeendelea kuwa ukosefu wa tiba au chanjo ya kumaliza ugonjwa huu. Kila mmoja yupo katika hatua za kujiadhari kutokana na ugonjwa huu na wito upo duniani kote kutafuta suluhisho. Kila sekta ya kimaisha imeathiriwa kwa sehemu kubwa, hali ya kiroho, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na afya za wanadamu zimebadilika sana. Nchini kwetu Tanzania tunaendelea kuchukua taadhari ili kupunguza kasi ya maambukizi. Kasi ya maambukizi inaendelea kila siku na hofu kuu imetanda dunia yote, hakuna wa kumsaidia mwenzake. Makala ya iliyopita tulizungumzia juu ya Mamlaka ya Neno la Mungu. Leo tunataadharisha ya kuwa ‘Janga hili ni letu sote’. Karibu tujifunze.
Janga Hili ni Letu sote
Mwishoni mwa mwezi Disemba 2019 wakati maisha yanaendelea kama kawaida maeneo mengi duniani, janga la Corona likatibuka kutokea eneo la Wuhan nchini China. Kipindi hicho wala jila la maradhi haya hayakufahamika. Sehemu nyingi za dunia hatukubeba uzito wa janga hili tukahisi ni suala la China na wao ndio watawajibika kuhusiana na UTATUZI wa janga hili.
Tumeingia mwaka 2020, tumefanya sherehe mbalimbali za mwaka mpya, wakati wenzetu wachina wanahangaika kupambana na maambukizi ya virusi hivi. Maisha yaliendelea taarifa ya virusi hivi haikuwa kubwa sana wala hatukuona hatari ya sisi wa dunia ya tatu kufikwa na janga hili. Hakuna aliyepeleka msaada Uchina, walibaki peke yao, kila upande ukikebehi tabia zao za kula kula kila kitu kwani inasadikiwa ya kuwa maradhi haya yametoka kwa popo.
Taratibu nchi za jirani kuanzia Taiwan maambukizi yakaanza kutokea mwezi Januari 2020. Kidogo maambukizi yakaanza kuenea bara Asia katika nchi ya Ufilipino. Mwanzoni mwa Februari maambukizi yakaingia bara la Ulaya. Tarehe 14 Februari 2020 maambukizi yakaingia Afrika, nchini Misri. Maambukizi yakaendelea huku kila mtu akilaumu wachina lakini hakuna taadhari zozote zilizochukuliwa mapema kutokana na wasafiri waliotoka Uchina kurudi maeneo yao au kwa biashara au kwa kazi maalum. Mpaka sasa karibu kila eneo na nchi zote duniani zimeathiriwa kwa sehemu kubwa na maambukizi. Dunia ilikuja kushtuka sana pale nchi ya Italia ilipoanza kutoa taarifa ya vifo vingi vinavyotokana na virusi vya Corona.
Hii ni kawaida yetu wanadamu, jambo likiwa mbali tunaona si letu, halituhusu lakini sasa lipo nyumbani kwetu, kwenye miji yetu na dunia nzima inatetemeka. Tulifikiri hili linawahusu Wachina peke yao, dunia ikawaacha, likafika mataifa mengine ya Asia. Tulifikiri litaishia Asia likaingia Ulaya, tukaona si letu litaishia huko likaingia Marekani. Tukadhani halitafika huku likaingia Afrika. Tukaona kwa sababu nchi zile zina maingiliano la Ulaya halitafika Afrika Mashariki, cha ajabu janga hili limefika kila nchi dunia yote. Hakuna wa kumsaidia mwengine kwa wakati huu.
Ni dhahiri janga hili linaathiri dunia nzima. Tunaweza kunyoosheana vidole ya kuwa taifa lile hawana dini au hawamwamini Mungu au wanaabudu miungu ndio maana wamepata mabaya yote haya, lakini ni dhahiri ipo shida si kwa taifa moja moja tu bali kwa dunia yote. Hakuna taifa ambalo ugonjwa huu haujapeleka ujumbe. Hii ina maana sisi wakazi wa dunia yote kwa njia moja au nyingine tumehusika kuleta madhara haya juu yetu na tunapaswa kuwajibika kutafuta suluhisho juu ya madhara haya.
Bwana Yesu katika mafundisho yake aliwahi kuwaonya watu na mtazamo huu wa kufikiri wao ni wema sana kuliko wengine.
‘Na wakati uo huo walikuwapo watu waliompasha habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao. Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo. Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua, mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo’ Lk.13:1 – 5.
Kama tunavyoona maandiko haya tuliyonukuu ambapo watu wa wakati huo walimpasha habari Bwana Yesu juu ya watu walioangamizwa na Pilato. Lakini majibu yake ndio ambayo tunapaswa sisi wa wakati huu kuyatafakari na kuzingatia zaidi.
- Wale ambao wanapoteza maisha kwa kuuwawa au kwa majanga fulani si kwamba ni waovu kuliko sisi tuliobaki
- Vifo hivi ni ishara au ujumbe kwa ajili yetu tulio hai kutafakari njia zetu na kumgeukia Mungu
Wengi tulifikiri watu wa China ni waovu sana hawana Mungu hivyo ndio maana mabaya yamewapata. Pia tulidhani mataifa ya Ulaya ni waovu sana wamemwacha Mungu ndio maana wamekufa wengi. Tukaona taifa la Marekani nalo ni ovu sana kwa sababu kadhaa ndio maana wameongoza katika visa hivi vya maambukizi. Lakini ujumbe kwetu tunapotazama athari kubwa za Corona tunapaswa kujikagua sisi tunarudisha vipi mioyo yetu kwa Mungu kutuepusha na balaa hili.
Kwa sasa watu wengine wanafikiri ugonjwa huu utawaondoa wazee na wale wenye maradhi mengine kutokana na tafiti kwa sababu ndio waathiriwa wakubwa mpaka sasa, lakini hatuwezi kujua athari za ugonjwa huu kwa watu wengine hapo baadae, tunaweza kuondoka wote bila kujali jinsia, kabila, rangi, cheo au dhamana tulizopewa. Ugonjwa huu haujaangalia masikini wala tajiri.
Nitoe rai kwa watoto wa Mungu kila mahali ya kuwa jambo hili si lao peke yao bali ni letu wote, tunao wajibu wa kuchukua hatua sahihi wakati huu na si muda wa kulaumu wengine ila kuutafuta uso wa Mungu, kwa maana TUSIPOTUBU TUTAANGAMIA kama wengine.
Maombi ya leo
Ee, Mungu Baba uliyeziumba mbingu na nchi na vyote ndani yake, unayejua majira na nyakati za maisha ya wanadamu kizazi na kizazi, tunakushukuru kwa neema yako ya uhai uliyotupatia leo. Asante kwa neno la uzima ambalo linatukumbusha ya kuwa shida ya mahali basi inatuhusu na sisi. Tunaomba rehema zako kwa kuwanyooshea wengine vidole na kulaumiana huku tukiendelea kuangamia. Tusaidie kuchukua wajibu wetu kama wanadamu kuutafuta uso wako kwa kweli na kutubu. Tunakuomba utujalie haya kwa utukufu wa Jina lako na mwana wako Yesu Kristo. Amen
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!