
Utangulizi
Karibu tena ndugu msomaji katika mfululizo wa makala hizi za kujifunza juu ya maana ya kazi kwa lengo la kuboresha maisha yetu kila siku na kusaidia watu wengi ambao wanapaswa kufanya kazi ili kuingia kazini.
Katika makala iliyopita tumeendelea kujifunza maana ya neno kazi kwa tafsiri ya biblia na tukajifunza kazi kwa maana ya huduma. Makala iliyopita ilihitimisha maana za kazi ambazo zinafunuliwa katika maandiko. Hii haina maaana ya kuwa hazipo maana nyingine, lakini kwa muktadha wa somo hili tutaendelea kuzijadili maana 5 tulizoziona. Leo tunazingalia maana hizi zote kuwa ufupi na namna zinavyoshabiiana na shughuli zetu za kila siku. Karibu sana.
Tafsiri pana ya maana ya kazi
Kwa mujibu wa tafsiri kadhaa ambazo tulizipata kutokana na maandiko, ni dhahiri kuna maana nyingi au aina nyingi za kazi ambazo zinaweza kutambulika. Hatahivyo tunaangalia zile maana 5 za msingi tulizojifunza na kutengeneza maana pana zaidi katika kufahamu neno kazi.
Kazi inaweza kutafsiriwa kumaanisha
Ni uwezo wa kuumba au kubuni au kuzalisha au kuwezesha upatikanaji wa bidhaa au huduma kunakopelekea tija, ufanisi na manufaa kwa jamii
Kwa tafsiri hii tunaziona maana zote 5 ambazo tumezijadili katika makala zilizopita.
Dondoo
- Kazi ni uwezo wa kuumba
- Kazi ni uwezo wa kubuni
- Kazi ni uwezo wa kuzalisha
- Kazi ni uwezeshaji wa kupatikana kitu au vitu (bidhaa)
- Kazi ni uwezeshaji wa kupatikana kwa huduma
Ndugu msomaji jaribu kupima kwa kutazama tu kila kazi inayofanyika katika mazingira yako utaona ya kuwa inaangukia katika maeneo haya 5 ambayo tumeanza kuyajadili katika mfululizo wa makala hizi za maana ya kazi. Iwe una taaluma ya kufundisha au mwanasheria au daktari maana yake unatoa aina ya kazi ya huduma. Ikiwa una aina ya usanii au ubunifu wa aina yoyote au ufundi basi utaona unaangukia katika aina ya kazi za kuumba au kubuni. Je, wewe ni mkulima au unafanya kazi za viwanda basi unafanya kazi za aina ya uzalishaji. Iwapo unahusika na ubadilishanaji wa bidhaa kwa fedha basi unafanya biashara n.k.
Tafsiri hii pamoja na kueleza maana za kazi zinavyofunuliwa ndani ya Biblia halikadhalika zinaeleza juu ya aina mbalimbali za kazi ambazo watu wanaweza kuzifanya. Hii ina maana kila mmoja wetu anao uwezo wa kuumba kitu au kubuni au kuzalisha au kuuza au kutoa huduma. Hakuna mtu mmoja kati yetu bila kujali hali yake ambaye hana kitu kwa ajili ya watu wengine.
Ni muhimu sana kwetu kupata tafsiri ya neno kazi kwa upana wake pasipo kufungwa na tafsiri finyu zinazotokana na mazoea au taaluma tulizosoma. Watu wengi wanafikiri ili uwe na kazi ni lazima uwe umeajiriwa, lakini kwa kuangalia ufafanuzi huu na kwa kadri tutakavyoendelea kujifunza tunaweza kuona aina zote hizi za kazi kama maandiko yanavyoeleza ni kazi ambazo unaweza kuzianzisha wewe mwenyewe bila kujali hali uliyonayo sasa au kiwango chako cha elimu.
Tunachopaswa kufanya ni kuendelea kujifunza juu ya tafsiri hizi za neno kazi na kujichunguza ndani yetu ni aina ipi ambayo tunaweza kuifanya na kuleta matokeo mazuri kwa maisha yetu na jamii kwa ujumla.
‘Asiyetaka kufanya kazi na asile…’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!