
Utangulizi
Karibu tena ndugu msomaji katika mfululizo wa makala hizi za kujifunza juu ya maana ya kazi kwa lengo la kuboresha maisha yetu kila siku na kusaidia watu wengi ambao wanapaswa kufanya kazi ili kuingia kazini.
Katika makala iliyopita tumeendelea kujifunza maana ya neno kazi kwa tafsiri ya biblia na tukajifunza kazi kwa maana ya biashara. Leo tunaendelea kupangalia tafsiri nyingine ya neno kazi kwa maana ya huduma. Karibu sana.
Maana ya 5. Kazi ni Uwezeshaji wa kupatikana kwa Huduma (Service ability)
‘Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe’ Efe.4.11-12
Kwa mujibu wa andiko tulilonukuu hapo neno kazi linafunuliwa kumaanisha HUDUMA. Ukitazama vizuri maandiko haya neno ‘huduma’ haimaanishi juu ya nafasi zile za manabii, wachungaji, wainjilisti, waalimu na mitume bali nafasi hizi zinatumika kwa lengo la kuwakamilisha watakatifu ili hao watakatifu watende ‘KAZI YA HUDUMA’. Hii ina maana kuwa kila mkristo au kila mwanadamu anayo nafasi yake ndani ya Kristo. Kila mtu anacho kitu cha kufaidia mwili wa Kristo.
Hivyo mojawapo ya maana ya neno kazi kwa mujibu wa maandiko ni UWEZESHAJI WA KUTOA HUDUMA au kwa lugha ya kiingereza linatafsiri ya ‘service ability’.
Utoaji wa huduma ni namna moja wapo ya biashara ya bidhaa isiyoshikika kwa mkono. Kulingana na maendeleo ya sayansi na teknolojia tunaona uchumi wa dunia unaelekea katika huduma zaidi. Mfano mashirika ya kutoa huduma za mawasiliano ndiyo yanaongoza katika kutengeneza fedha nyingi zaidi duniani. Tunaona makampuni kama facebook, instagram, Microsoft n.k ni huduma za mawasiliano zenye wafuasi wengi duniani wanaozitumia. Je, mimi na wewe tunatumia vipi vifaa hivyo kwa lengo la kutoa huduma ya kuleta faida kwa jamii na ufalme wa Mungu kwa ujumla.
Leo tumeona juu ya maana ya kazi kama uwezeshaji wa kupatikana kwa aina mbalimbali za huduma. Kazi inaweza kuwa zao la huduma. Hivyo zipo kazi za kihuduma ndani ya watu ambazo zinapaswa kufanywa siku kwa siku. Endelea kufuatilia makala hizi kujifunza zaidi juu ya maana ya kazi.
‘Asiyefanya kazi asile…’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!