
Utangulizi
Karibu tena ndugu msomaji katika mfululizo wa makala hizi za kujifunza juu ya maana ya kazi kwa lengo la kuboresha maisha yetu kila siku na kusaidia watu wengi ambao wanapaswa kufanya kazi ili kuingia kazini.
Katika makala iliyopita tumeendelea kujifunza maana ya neno kazi kwa tafsiri ya biblia na tukaona juu ya maana ya 2 na 3 ya neno kazi. Leo tunaendelea kupangalia tafsiri ya neno kazi kwa maana ya kibiblia kwa kutazama maana nyingine zinazoanishwa kimaandiko. Karibu sana.
Maana ya 4. Kazi ni Uwezeshaji wa kupatikana kwa kitu au vitu (Business ability)
‘Hata saa hii ya sasa, tuna njaa na kiu, tu uchi, twapigwa ngumi, tena hatuna makao; kisha twataabika tukifanya kazi kwa mikono yetu wenyewe. Tukitukanwa twabariki, tukiudhiwa twastahimili’ 1.Kor.4:11-12
‘Mwibaji asiibe tena, bali afadhali afanye juhudi, akitenda kazi iliyo nzuri kwa mikono yake mwenyewe, apate kuwa na kitu cha kumgawia mhitaji’ Efe.4:28
Kwa maandiko haya tuliyonukuu ni dhahiri maana ya kazi inaonekana kuwa hali ya kuwezesha upatikanaji wa kitu au vitu kwa ajili ya wahitaji. Tunamwona Paulo akieleza pamoja na kuhubiri kwake bado yeye na washirika wenzake wanafanya kazi kwa mikono yao wenyewe ili wasiwe tegemezi kwa mtu yeyote. Pia anatoa ushauri kwa waibaji ambao inaweza kumaanisha wezi au watu wanaofanya shughuli isiyo halali katika jamii yaani yule asiye na kazi halali kwamba aache kuiba afanye kazi ambayo italeta kitu kwa mhitaji. Neno mhitaji katika andiko hili halijatumiwa kumaanisha mtu asiyejiweza au anayehitaji msaada bali limetumika kumaanisha ‘mteja’ au ‘customer’ yaani mtu mwenye kuhitaji bidhaa fulani au huduma.
Hivyo mojawapo ya maana ya neno kazi kwa mujibu wa maandiko ni UWEZESHAJI WA KUPATIKANA KWA KITU AU VITU (BIDHAA) au kwa lugha ya kiingereza linatafsiri ya ‘business ability’ au ‘trading ability’.
Kama tulivyoona katika maana zilizotangulia dunia ya sasa ina mahitaji makubwa kutokana na wingi wa wakaazi waliopo. Mifumo ya mawasiliano na usafiri vimekuwa rahisi sana kwa wakati huu kuliko wakati wowote uliotangulia. Mtu anaweza kufanya biashara kutoka bara moja kwenda lingine na kuagiza bidhaa zake ndani ya siku chache sana. Kila mtu anacho kitu cha kuuza kwa dunia, changamoto ni kuwa wengi hatujajua ni kitu gani cha thamani kilichopo ndani yetu ambacho tunaweza kukiuza kwa wengine. Kama ndani yako una uwezo wa kuumba, kubuni na kuzalisha hakika vipo vitu au bidhaa ambazo unaweza kutengeneza kwa ajili ya wengine. Pia unaweza kutumia uwezo wa kuuza kwa lengo la kutumia bidhaa zilizotengenezwa na wengine na kupata faida.
Leo tumeona juu ya maana ya kazi kama uwezeshaji wa kupatikana kwa kitu au vitu yaani bidhaa. Kazi ni zao la biashara. Hivyo zipo kazi za biashara ndani ya watu ambazo zimekusudiwa kufanywa. Endelea kufuatilia makala hizi kujifunza zaidi juu ya maana ya kazi.
‘Asiyefanya kazi asile…’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!