
Utangulizi
Karibu tena ndugu msomaji katika mfululizo wa makala hizi za kujifunza juu ya maana ya kazi kwa lengo la kuboresha maisha yetu kila siku na kusaidia watu wengi ambao wanapaswa kufanya kazi ili kuingia kazini.
Katika makala iliyopita tumeanza kujifunza maana ya neno kazi kwa tafsiri ya biblia na tukaona juu ya maana ya 1 ya neno kazi ni Uwezo wa Kuumba. Leo tunaendelea kupangalia tafsiri ya neno kazi kwa maana ya kibiblia kwa kutazama maana nyingine zinazoanishwa kimaandiko. Karibu sana.
Maana ya 2. Kazi ni Uwezo wa Kubuni (Innovation ability)
‘BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Angalia, nimemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda; nami nimemjaza roho ya Mungu, katika hekima na maarifa, na ujuzi na mambo ya kazi ya kila aina, ili abuni kazi za ustadi, kuwa fundi wa dhahabu, na wa fedha, na wa shaba, na kukata vito kwa kutiwa mahali, na kuchora miti, na kufanya kazi ya ustadi iwayo yote’ Kut.31:1-5
Maandiko ambayo tumenukuu hapa yanaonesha juu ya maagizo ambayo Musa alipewa na BWANA Mungu kuhusiana na kumjengea patakatifu ambayo alianza kuyapokea kuanzia Kitabu cha Kutoka 25 – 30. Kisha yale aliyomwagiza ndipo anamweleza kuwa yatafanywa na Bezaleli. Katika maandiko haya tunaona neno kazi linapewa tafsiri ya UWEZO WA KUBUNI. Hivyo mojawapo ya tafsiri sahihi ya neno kazi kimaandiko ni uwezo wa kubuni au kwa lugha ya kiingereza ‘Innovation ability’ au ‘ability to invent or innovate’.
Ubunifu ni kuongeza ufanisi au utendaji wa kitu fulani kwa nia ya kuboresha zaidi matokeo yanayotarajiwa. Kuna vitu vingi vimeundwa au kuumbwa muda mrefu lakini kwa kadri muda unavyosogea mahitaji ya kitu au huduma bora zaidi yanahitajika na jamii, hapa ndipo dhana ya ubunifu inapoingia. Pia mtu anaweza akawa na wazo au tafsiri ya kitu au aina ya kitu anachotaka lakini anashindwa namna ya kutekeleza anaenda kwa mtu mwengine na kumweleza kisha huyu mtu anabuni hicho kitu na kukitoa katika mawazo ya huyo mtu kuwa halisi. Hapa ndipo taaluma za wachoraji wa majengo zilipotokea na wabunifu wa fani za aina mbalimbali.
Zipo kazi nyingi za ubunifu zimefichwa ndani ya watu ambazo zimekusudiwa zitolewe na wahusika hao kwa manufaa ya dunia nzima na wao kwa ujumla.
Maana ya 3. Kazi ni Uwezo wa Kuzalisha (Productive ability)

‘Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi’ Mwa.1:28
‘BWANA Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya… BWANA Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza’ Mwa.2:8, 15
Kwa maandiko yaliyonukuliwa hapa tunaona neno la msingi linalojitokeza kuhusianishwa na kazi ni uwezo wa kuzaa au kuzalisha. Neno zaeni haina maana suala la kupata watoto tu bali lina maana pana zaidi. Kwenye tafsiri ya mstari huu neno zaeni linasomeka kama ‘be fruitful’ tafsiri ya Biblia ya Mfalme James (King James Version), hii ina maana ya kuzaa matunda. Ili matunda yawepo ni lazima kazi ifanyike na ndio msingi wa Mungu kumweka mtu katika bustani ya Edeni ailime na kuitunza. Hivyo mojawapo ya maana ya neno kazi kwa mujibu wa maandiko ni UWEZO WA KUZAA AU KUZALISHA au kwa lugha ya kiingereza linatafsiri ya ‘ability to produce’ au ‘productive ability’.
Zipo shughuli nyingi ambazo mwanadamu anaweza kuzalisha kupitia hizo, zinaweza kuwa shughuli za kilimo au ufugaji au viwanda n.k. Wengi hawachukui hatua za kuzalisha wakisema hakuna kazi lakini mambo ya kuzalisha yapo na mahitaji ya dunia bado ni makubwa sana. Kwa sasa dunia ina wakaazi takribani Bilion 7.7 watu hawa wote wanahitaji chakula, maji, mavazi na malazi kila siku achilia mbali mahitaji mengine muhimu. Sisi tunaokaa katika zama hizi tunao wajibu mkubwa wa kuhakikisha tunatengeneza uzalishaji mkubwa zaidi kukidhi haja na mahitaji ya wanadamu wengi.
Ndugu msomaji leo tumeendelea kuona tafsiri ya neno kazi kwa mujibu wa maandiko ya biblia, endelea kufuatilia mfululizo wa makala hizi kujifunza zaidi juu ya maana ya kazi kama inavyofafanuliwa na maandiko.
‘Asiyefanya kazi asile…’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!