Utangulizi
Karibu tena ndugu msomaji katika mfululizo wa makala hizi za kujifunza juu ya maana ya kazi kwa lengo la kuboresha maisha yetu kila siku na kusaidia watu wengi ambao wanapaswa kufanya kazi ili kuingia kazini.
Katika makala iliyopita tumejifunza kwa kuangalia tatizo kubwa si ukosefu wa kazi au ajira bali ni changamoto ya mtazamo au fikra ndani ya watu. Pia tumeangalia tafsiri ya neno kazi kwa maana ya kawaida. Leo tunaendelea kupangalia tafsiri ya neno kazi kwa maana ya kibiblia. Karibu sana.
‘Yesu akawaambia, Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake’ Yn.4.34
Maneno haya ya Bwana Yesu aliyasema kwa wanafunzi wake baada ya kumletea chakula ili ale naye akasema anacho chakula wasichokijua (soma Yn.4:31-38). Bwana Yesu anaeleza wazi kuwa hicho chakula wasichokijua ambacho yeye ndicho anakula ni kuyatenda mapenzi yake aliyempeleka na kuimaliza kazi yake. Hakuna ubishi kuwa Bwana Yesu alifanya kazi ya Mungu hapa duniani na hatujasikia akieleza endapo alikuwa akilipwa kwa mwezi au wiki katika kipindi chote alichokuwa akifanya kazi. Andiko hili linatupa chachu ya kutaka kuchunguza kwa ndani hasa juu ya asili ya neno kazi kwa mujibu wa maandiko ya neno la Mungu. Hii ina maana kuwa neno kazi kwa mujibu wa maandiko ni zaidi ya lengo la kupata kipato au ujira kama tulivyoona kwenye tafsiri ya kawaida.
Kwa sentensi hii ya Bwana Yesu tunaweza kujiuliza maswali kadhaa ya kuchokonoa fikra zetu kufikiri zaidi maana na upana wa neno kazi kwa maandiko
- Je, ni kazi gani hiyo Bwana Yesu aliyoisema kuwa anapaswa kuifanya?
- Ni nini maana ya neno kazi kwa mujibu wa neno la Mungu?
- Kama Bwana Yesu hakupokea mshahara au ujira au kipato kwa kazi hapa duniani aliwezaje kujikimu maisha yake kwa mahitaji ya kimwili?
- Je, mimi na wewe tunafanya kazi kwa msingi wa tafsiri ya neno la Mungu au kwa tafsiri ya kawaida?
Nikiri hapa kwamba mpaka sasa sijaweza kuona tafsiri ya moja kwa moja kwenye maandiko inayoeleza kazi ni nini hasa, ila kwa kupitia maandiko tunaweza kuona namna shughuli zilivyofanyika na zikaibua aina na tafsiri mbalimbali za neno kazi katika mazingira husika. Hivyo tafsiri zitakazoainishwa katika makala hiii si mwisho wa tafsiri husika bali kwa kadri na kipimo kile tulichofunuliwa na Roho Mtakatifu kwa hitaji la sasa. Karibu tuzitazame tafsiri na aina za kazi kama zinavyofunuliwa katika maandiko matakatifu.
Maana ya 1.
Kazi ni Uwezo wa Kuumba (Creative ability)
‘Hapo mwanzo Mungu aliziumba Mbingu na Nchi. Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji. Mungu akasema, iwe nuru, ikawa nuru.’ Mwa.1:1-3
‘Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote. Na siku ya saba Mungu aliimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya’ Mwa.2:1-2
Maandiko tuliyonukuu hapa yanaonesha juu ya historia ya uumbaji katika Kitabu cha Mwanzo 1 -2. Ukisoma habari hizi zinaonesha juu ya uumbaji wa Mungu katika siku sita na kustarehe kwake siku ya saba. Hivyo kwa tafsiri inayofunuliwa katika maandiko haya neno KAZI lina maana ya UWEZO WA KUUMBA. Hivyo mojawapo ya tafsiri sahihi ya neno kazi kimaandiko ni uwezo wa kuumba au kwa lugha ya kiingereza unaweza kusema ‘creative ability’ au ‘ability to create’.
Katika historia ya uumbaji ambao Mungu alifanya kwa siku 6, tunaona akiumba mbingu na nchi na vyote vilivyoijaza. Tunaona ameumba nuru, anga, akatenga nchi kavu na bahari, akatoa mimea katika nchi, akaumba jua, mwezi na nyota, akaumba ndege wa angani, wanyama na viumbe ndani ya bahari. Kisha akamuumba mwanadamu kwa sura na mfano wake.
Baada ya uumbaji huu hatuoni Mungu akiingia moja kwa moja kuendeleza uumbaji isipokuwa kwa kupitia mbegu ya vile alivyoviumba. Tangu wakati huo mwanadamu ndiye amekuwa akiendeleza kazi ya uumbaji kwa kutengeneza vitu ambavyo Mungu hakuviumba mwanzo.
Tunaona maendeleo yameleta vyombo vya usafiri ikiwa magari, pikipiki, meli, ndege, treni n.k tumeona nyumba na magorofa makubwa yakijengwa, barabara na vifaa mbalimbali tunavyotumia ikiwepo luninga, kompyuta, simu n.k vyote hivi ni kazi ya uumbaji iliyofanywa na mwanadamu toka kizazi hadi kizazi.
Hivyo ni sahihi kusema ndani ya kila mwanadamu aliyeumbwa kwa mfano na sura ya Mungu anao uwezo wa kufanya kazi ya uumbaji kulingana na mazingira yake na mahitaji yaliyopo wakati huo.
Ndugu msomaji leo tumeanza kuona tafsiri ya neno kazi kwa mujibu wa maandiko ya biblia, endelea kufuatilia mfululizo wa makala hizi kujifunza zaidi juu ya maana ya kazi kama inavyofafanuliwa na maandiko.
‘Asiyefanya kazi asile…’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!