Karibu tena ndugu msomaji katika mfululizo wa makala hizi za kujifunza juu ya maana ya kazi kwa lengo la kuboresha maisha yetu kila siku na kusaidia watu wengi ambao wanapaswa kufanya kazi ili kuingia kazini.
Katika makala iliyopita tumejifunza kwa kuangalia tatizo kubwa si ukosefu wa kazi au ajira bali ni changamoto ya mtazamo au fikra ndani ya watu. Leo tunaangalia tafsiri ya neno kazi. Karibu sana
Utangulizi
Watu wengi wa umri wa kufanya kazi tunaamka kila siku tukiweka tumaini na mipango mingi na namna bora ya kuboresha kazi zetu. Tunazifikiria kazi zetu za kitaaluma au ujuzi tulionao au biashara tunazofanya kila siku. Ndani yetu tunaweka matarajio mengi ya kupiga hatua za mafanikio katika maisha kwa kuzitegemea kazi tunazofanya.
Hatahivyo, ni jambo la kushangaza ya kuwa si wengi wanaofanya kazi wanapata muda wa kutafakari kwa kina maana ya neno Kazi. Hatupati muda wa kutafakari juu ya kile tunachofanya endapo ni ajira au kazi? Je ipo tofauti kati ya kazi na ajira na kama ipo ni nini tofauti zake?
Katika makala hii tunakwenda kuona kwa kina maana ya kazi kama inavyotafsiriwa na walio wengi, na pia tafsiri ya kazi kwa mujibu wa maandiko matakatifu yaani Biblia.
- Maana ya Kazi tafsiri ya Kawaida
Kazi inatafsiriwa kama shughuli yoyote halali inayompatia mtu kipato au fedha au ujira. Katika kuitazama maana hii au tafsiri hii ya kawaida tunaweza kuona mambo makuu matatu yanayojitokeza
- Shughuli yoyote – hii ina maana kazi ni lazima ihusishe kufanyika kwa kitu fulani yaani shughuli iwe inatumia nguvu za kimwili au akili au vyote kwa pamoja.
- Uhalali wa shughuli – shughuli hiyo ni lazima iwe halali, yaani haipingani na matakwa ya kisheria. Kwa mantiki hii, si kila shughuli ni kazi. Ili shughuli iweze kuwa kazi, basi ni lazima iwe kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazoongoza jamii husika.
- Kipato/ujira – matokeo ya kazi ni kunufaika kwa mfanyakazi kiuchumi yaani kupata fedha au malipo kutokana na kazi aliyoifanya.
Huu ndio mtazamo wa tafsiri wa walio wengi wanaofanya kazi au wale wanaosema kuwa hawana kazi. Yule anayejitambulisha kuwa anafanya kazi ana maana kuwa ipo shughuli halali anayoifanya ya kumwingizia kipato. kadhalika na yule anayesema hana kazi ana maana kuwa hajaona bado au hajapata bado shughuli halali ya kumwingizia kipato.
![](https://isaackzake.co.tz/wp-content/uploads/2020/02/1.jpg)
Changamoto ya Tafsiri ya Kawaida juu ya neno Kazi
Kwa hakika tafsiri hii kwa sehemu kubwa ndio inachangia tatizo la kazi au ajira kuwa kubwa sana katika nchi zinazoendelea na hata zile zilizokwisha kuendelea. Tafsiri hii inayo mapungufu mengi ambayo tunaweza kuyaainisha hapa kama ifuatavyo;
- Shughuli yoyote – ile kwamba tafsiri inahusisha shughuli yoyote kwa walio wengi wanakosa mwelekeo na shabaha (focus) ya kujua ni kitu gani wanapaswa kufanya kwenye maisha. Hali hii inawasumbua sana vijana, wanauliza mno wasome kitu gani ambacho kinalipa badala ya kujiuliza wao ndani yao wana nini cha kuipa dunia. Hapa ndipo tunakutana na wanataaluma wa eneo moja, wakifanya shughuli nyingine kabisa mbali na taaluma zao. Ndipo tunakutana na msemo usemao ‘kazi ni kazi bora mkono kinywani’
- Isiyozuiliwa kisheria – ile kwamba sheria au taratibu hazizuii kile unachofanya haina maana jamii au Mungu anakubaliana na kile unachofanya. Watu wengi wanaamua kufanya aina ya kazi ambayo kwa hakika ina madhara kwao na kwa jamii lakini kwa kuwa hakuna sheria inayowazuia na wao wanaona faida ndani yake wanaamua kufanya. Hapa ndipo tunakutana na aina za biashara ambazo kwa hakika zina madhara kwa wanadamu wenzetu kama biashara za vilevi au madawa ya kulevya na sigara au wengine kujiuza miili yao n.k
- Kipaombele cha kipato – kwa tafsiri hii kipato au ujira ndilo lengo kuu. Hii ina maana kuwa mtu yupo radhi kufanya lolote ndani ya uwezo wake ili apate fedha. Mfanyakazi haweki nguvu katika kuhudumia watu au wateja wake bali namna gani ataipata fedha yao iwe kwa uhalali au hila kupitia kazi yake. Hapa ndipo tunakutana na changamoto ya dhuluma na rushwa kwenye kazi au matukio ya unyang’anyi na aina nyingine za kupata fedha.
- Utegemezi – tafsiri hii pia kwa sehemu kubwa inamweka mfanyakazi katika hali ya utegemezi wa aidha kuajiriwa, au kutafuta mtaji au ujuzi ili kufanikisha kazi yake. Fikra za mfanyakazi zinajengeka kwamba, ili aweze kufanya kazi ni lazima aajiriwe katika shughuli halali au aanzishe shughuli halali yenye kuweza kuingiza kipato.
Kwa uchache tu tunaweza kuona athari zinazosababisha jamii yetu kwa sehemu kubwa kubaki katika hali ya uduni kwa sababu tu ya kutokuwa na fikra sahihi juu ya jambo husika. Maandiko yanasema ‘aonavyo nafsini mwake ndivyo alivyo’ maana yake hali zetu kimaisha, hali zetu kuhusiana na kazi ni matokeo ya kile tulichoona au tulichotafsiri ndani yetu. Kama tafsiri yetu kuhusiana na kazi ni shughuli yoyote halali ya kuingiza kipato basi, ni mpaka pale tutakapokuwa na aina ya shughuli halali yenye kutupatia fedha ndipo tunajihesabu kuwa ni wafanyakazi mbali na hapo sisi si wafanyakazi.
Endelea kufuatilia mfululizo wa makala hizi ambazo zitatusaidia kujifunza masuala ya kazi na ajira na mbinu za kutusaidia kutimiza wajibu wetu katika kizazi chetu.
‘Asiyefanya kazi na asile…’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!