• Twitter
  • Facebook
  • Instagram
Isaack Zake
  • Home
  • Kuhusu Mimi
  • Huduma
  • Vitabu
  • ULIZA
  • Shop
  • Blog
  • Mawasiliano
  • Search
  • Menu Menu
MAANA YA KAZI

Sehemu ya 1. Maana ya Kazi

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa mtandao wa isaack zake kwa ajili ya kupata maarifa na hekima zitakazoweza kukusaidia kupiga hatua katika maisha yako. Ukurasa huu ni maalum kwa ajili ya mafundisho yanayohusu kazi na ajira. Katika nyakati hizi tunashuhudia ongezeko kubwa la watu wasio na kazi au ajira. Hivyobasi Ukurasa wa ‘Uliza Kazi’ utakuwa mahsusi kwa lengo la kusaidia namna ya utatuzi wa changamoto hii. Karibu ufuatilie mfululizo wa makala za ‘Maana ya Kazi’ leo ikiwa ni sehemu ya kwanza. Karibu sana.

‘Maana aonavyo nafsini mwake ndivyo alivyo’ Mith.23.7a

Katika mambo ambayo yanaathiri sana maisha ya watu, kitabia, kimaamuzi na hata hali zao ni mtazamo unaojengwa na tafsiri ndani ya nafsi zao. Endapo mtu atapata tafsiri isiyo sahihi juu ya jambo fulani basi hitilafu hiyo itajitokeza tu katika mfumo wa maisha yake. Hivyo ni muhimu sana kuangalia na kupima tafsiri ya kile tunachofanyia kazi mara kwa mara ili isiwe tafsiri ambayo si sahihi.

Hali ya Ajira na Kazi katika Nchi yetu ya Tanzania

Tatizo la ajira ni mojawapo ya changamoto kubwa katika kizazi chetu. Kilio kikubwa kipo kwa kundi la vijana ambao ndio wanatarajiwa kuwa wazalishaji wakuu katika taifa. Kuna uhaba mkubwa wa ajira katika taifa letu kuliko nyakati zilizotangulia. Hata zile ajira zilizopo nyingi zipo hatarini kutokana na mabadiliko ya kimfumo wa uchumi wa utandawazi. Changamoto ya ajira si tu kwa taifa letu la Tanzania bali ni suala la dunia nzima.

Kwa mujibu wa takwimu mbalimbali inaonesha Tanzania ina idadi ya watu wasiopungua Milioni 55 kwa sasa na kundi kubwa kati ya hawa ni vijana ambao ndio umri wa kuzalisha. Tanzania inashika nafasi ya 23 katika nchi zenye idadi kubwa ya watu duniani wakati kwa Afrika inashikilia nafsi ya 5 ikitanguliwa na nchi za Nigeria, Ethiopia, Misri, Congo DRC.

Takwimu hizi ukizitazama ni kama zinaweza kutisha hivi, kwani idadi kubwa inaongezeka ya watu lakini kiwango cha kazi na ajira kinazidi kupungua kila siku. Inakadiriwa kila mwaka katika nchi yetu watu zaidi ya 800,000 huingia katika soko la ajira ambalo haliwezi kutoshelewa watu wote hao. Zaidi ya nusu ya Watanzania ni kundi la watu walio kati ya umri wa miaka 15 – 60 ambalo ndilo kundi la kuzalisha katika Tanzania.

Waathiriwa wakubwa wa changamoto hii ya ajira au kazi ni vijana waliosoma au wasiosoma wote wanatafuta namna ya kukabiliana na suala hili la ajira.

Tumesikia kauli nyingi na kelele kila kona kuhusu ‘ajira ni bomu linalosubiri kulipuka’ watu wanaipigia kelele Serikali tukidhani kuwa nao wana suluhisho. Ni kweli Serikali kwa sehemu inapaswa kuwa na sera, mipango na mikakati ya kujaribu kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira lakini haipaswi watu wote kulalamikia Serikali. Sisi wote ni mashahidi ya kuwa hakuna mzazi aliyefanya kikao na Serikali ili azae mtoto au watoto alionao, hivyo si sahihi kwa wazazi, walezi, viongozi au vijana ambao wanaathiriwa na tatizo hilo kuilaumu Serikali.

Hatahivyo lipo tumaini kwa njia ya Bwana Yesu Kristo anayetufariji na maneno yake akisema ‘Ninyi ni nuru ya ulimwengu’ akiwa na maana ya kuwa Kanisa ndilo limepewa dhamana ya kuangaza ulimwengu katika changamoto zinazowakabili watu. Ajabu ni kwamba Kanisa nalo linageuza kibao kuilaumu Serikali tunajikuta wote tumekwama. Hatuna sababu ya kusubiri hilo bomu la ajira au ukosefu wa kazi lije kulipuka wakati tuna uwezo wa kutafuta majibu ndani ya neno la Mungu na kushirikishana maarifa haya kulisaidia Kanisa na watu wengine wote.

Kwa hali hii Kanisa lina jukumu kubwa la kutafuta ufumbuzi wa changamoto hii ili kuleta suluhisho la kudumu kwa Kanisa na Jamii yote ya Tanzania.

Msingi wa Tatizo

Ili mtu au jamii iweze kuleta suluhusho katika jambo fulani ni muhimu sana au kuna ulazima wa kulifahamu tatizo kuhusiana suluhu husika. Kama unaleta suluhu yoyote pasipo kufahamu msingi wa tatizo, suluhisho hilo haliwezi kuwa la kudumu bali ni dhahiri tatizo litaendelea kuwepo.

Muda huu ukimuuliza kijana yeyote ambaye hajishughulishi na kazi au ajira atakujibu kuwa ‘sina kazi’ au ‘sijapata kazi au ajira’ au ‘natafuta kazi’ au ‘bado nasoma shule’. Haya ndio majibu ambayo tumezoea kuyasikia na jamii yote imeyakubali pasipo kuhoji uhalali wa majibu haya na pengine tumewasaidia vijana kuwasilisha utetezi huu kila mara suala la kazi linapojitokeza.

Lakini maandiko yanatueleza vyema juu ya msingi wa kazi kwa kila mwanadamu aliyefikia umri wa kuweza kufanya kazi.

‘Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula’ 2.The.3.10

Msingi wa maandiko haya, Mungu anataka kutueleza kuwa kula chakula ni matokeo ya kufanya kazi. Hivyo kama mtu hataki kufanya kazi basi asipate chakula pia. Je, vijana wangapi wapo katika umri wa kuzalisha tunao nyumbani kwetu wanakula chakula asubuhi, mchana na usiku?. Kwa mtazamo wa kimataifa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, kijana ambaye anapaswa kuanza kuzalisha kuanzia umri wa miaka 18.

Tuna vijana wangapi kwenye kanisa na jamii yetu sasa wa umri huo na hatujaanza kuwafundisha au kuona matunda ya kazi zao kama Kanisa na jamii kwa ujumla?. Kama watanzania tunasomesha vijana wetu kwa muda mrefu kwa kuwekeza fedha nyingi tukitarajia njia tulizopitia sisi nao ndio watapita lakini hali imebadilika soko la ajira limekuwa na watu wengi wenye vigezo lakini hakuna ajira. Hivyo matokeo yake elimu  wanayopata katika shule na vyuo haiwezi kuwasaidia kuchukua hatua mbadala endapo ajira itakosekana.

Kwa kutazama andiko hili ina maana Mungu kwa neema yake amempatia kila mmoja wetu kitu cha kuweza kufanya ili kumsaidia kupata riziki yake yaani chakula. Hivyo kwa hakika hakuna asiye na kazi ndani yake bali mazingira tuliyoyajenga kwa vijana na kuwaaminisha kuwa kazi na ajira ni matokeo ya kuajiriwa hivyo kutochukua hatua stahiki.

Tatizo linalojitokeza katika mazingira haya si ukosefu wa ajira au ukosefu wa kazi au sio wingi wa watu wasio na ajira katika soko la ajira bali ‘mtazamo wa vijana na jamii’ kuhusiana na kazi na ajira

‘ukosefu wa ajira sio tatizo bali ni matokeo ya mtazamo usio sahihi juu ya kazi na ajira ndani ya jamii’

Kwa hiyo ili kuleta suluhu ya tatizo lazima ufahamu msingi wa tatizo, na shida yetu kama vijana sio ukosefu wa ajira bali ‘fikra sahihi’ kuhusiana na kazi na ajira ndizo zimekosekana na matokeo yake ni ukosefu wa ajira.

Wapo wasomi waliosema kufahamu asili ya tatizo unalokabiliana nalo tayari una kiasi cha 50% ya kuelekea kulitatua kwa ukamilifu. Hivyo kiasi cha 50% kitatokana na kupata suluhi sahihi na kuchukua hatua zinazostahili.

Ndugu yangu ndio maana mafundisho haya yanakujia kwa lengo la kuamsha fikra zako kijana, mzazi na mlezi kwa lengo la kuchukua hatua za mapema ili kutumia nafasi hii tuliyopewa na Mungu kuwa sehemu ya taifa hili zuri lenye kila aina ya fursa ya kufanikiwa kama tukiweka fikra zetu sawasawa na kuisikiliza sauti ya Mungu.

Endelea kufuatilia mfululizo wa makala hizi ambazo zitatusaidia kujifunza masuala ya kazi na ajira na mbinu za kutusaidia kutimiza wajibu wetu katika kizazi chetu.

‘…ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi asile chakula’

Isaack Zake

Wakili, Mwalimu na Mshauri

Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.

Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.

Share this:

  • Click to share on LinkedIn (Opens in new window) LinkedIn
  • Click to share on X (Opens in new window) X
  • Click to share on Facebook (Opens in new window) Facebook
  • Click to share on Telegram (Opens in new window) Telegram
  • Click to share on WhatsApp (Opens in new window) WhatsApp
February 20, 2020/0 Comments/by Isaack Zake
Share this entry
  • Share on Facebook
  • Share on Twitter
  • Share on WhatsApp
  • Share on LinkedIn
  • Share by Mail
https://isaackzake.co.tz/wp-content/uploads/2020/02/pexels-photo-3583055.jpeg 1116 1880 Isaack Zake https://isaackzake.co.tz/wp-content/uploads/2020/02/zake-2.png Isaack Zake2020-02-20 10:23:162020-12-11 10:57:36Sehemu ya 1. Maana ya Kazi
0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

MAKUNDI YA MAKALA

  • ELIMU (20)
  • FAMILIA (2)
  • KIPAJI CHANGU (14)
  • KUSUDI LA MAISHA (13)
  • MAANA YA KAZI (17)
  • MAKALA (2)
  • NENO LA MUNGU (8)
  • SPIRITUAL FOOD (55)

MAKALA MPYA

  • Day.55. Spiritual Food: Je, ulipo kuna maneno ya uzima wa milele? March 26, 2022
  • Day.54. Spiritual Food: Je, unataka kuondoka? March 24, 2022
  • Day.53. Spiritual Food: Je umekwazwa na kitu gani maishani? January 15, 2022
  • AES.20. Upimaji ni rahisi kuwa na udanganyifu November 8, 2021
  • Day.52. Spiritual Food: Twamwendea Bwana Yesu kwa Neema October 18, 2021

Kuhusu | Vitabu | Mawasiliano

© 2020 Isaack Zake. All Rights Reserved

Day.1: Spiritual Food: Msingi wa Chakula cha Kiroho Day.2. Spiritual Food: Nafasi ya muujiza/ishara katika maisha ya Kiimani.
Scroll to top