Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala mbalimbali katika mtandao huu wa isaackzake. Tunamshukuru Mungu sana kwa nafasi aliyotupa tena kukutana na wewe msomaji kwa njia ya makala hizi.
Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya kujulkana kwetu na Mamlaka ya Juu kabla hatujazaliwa na nafasi ambazo kila mmoja wetu amepewa kutimiza wajibu wake hapa duniani.
Leo nataka tukajifunze juu ya Mamlaka ya Juu kutambua juu ya siku zako zote. Karibu tujifunze.
Kila siku watu wanasherekea kumbukizi ya kuzaliwa kwao miaka kadhaa iliyopita, hata siku ya leo wapo maelfu ya watoto wamezaliwa duniani kote. Hizi ni nyakati nzuri za kufurahia maisha yetu na mara kwa mara tunapata nafasi ya kutafakari kule tulipotoka na kule tunapotaka kwenda kwenye maisha yetu.
Kitu ambacho wengi wetu hatukijui ni kuhusinana na siku yetu ya kifo, lakini ni kweli kabisa ya kwamba kadri tunavyosherekea kumbukizi za kuzaliwa kwetu ndivyo tunakaribia katika siku ya kifo chetu ambayo hatuijui.
Lakini tofauti na sisi, Mamlaka iliyo Juu yaani Muumba wetu anao ufahamu tangu siku yetu ya kuzaliwa na hata siku ya mwisho wetu niavyopaswa kuwa. Furaha kubwa inakuwepo tunapokumbuka siku ya kuzaliwa lakini hofu inaongezeka tunapofikiri kuhusiana na kifo chetu.
Tunaweza kuona hilo kupitia hekima tunayojifunza katika maandiko haya;
‘Kwa kila jambo kuna majira yake Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; wakati wa kupanda, na wakati wa kung’oa yaliyopandwa; Muh.3:1 – 2
Kama ulivyokuwepo wakati wa kuzaliwa pia upo wakati maalum wa kifo kwa ajili ya kila mmoja wetu. Wakati huu umewekwa na Mamlaka ya Juu kwa ajili ya kila kiumbe kinachopita chini ya Mbingu.
Swali muhimu sana la kujiuliza kadri tunavyoendelea kuzihesabu siku za maisha yetu na kila mwaka tunapopata nafasi ya kuadhimisha kumbukizi zetu za kuzaliwa, je kwa nini bado nipo hai mpaka leo hii? Kwa maana sisi sote ni mashahidi ya kuwa kila iitwapo leo watu wanakufa au wanaondoka katika maisha haya, tumekuwa tukisikia habari za misiba, tumeudhuria mara kwa mara na kushiriki shughuli za mazishi n.k
Je, kitu gani ambacho tunasubiri mpaka sasa kabla ya siku yetu ya kifo? Je, tumeshatambua kazi au kusudi la maisha yetu binafsi na kufanyia kazi?
Nikutakie baraka za Muumba katika kufuatilia hatua mbalimbali za kukuwezesha kulitambua kusudi la maisha yako na kulifanyia kazi.
Isaack Zake
Wakili, Mwandishi na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!