Karibu sana ndugu msomaji wa makala mbalimbali katika mtandao huu wa isaackzake. Tunamshukuru Mungu sana kwa nafasi aliyotupa tena kukutana na wewe msomaji kwa njia ya makala hizi.
Katika mfululizo wa awali wa makala hizi tumeweza kujifunza mambo ya msingi sana katika kupata maarifa juu ya kusudi la maisha yetu binafsi. Tumejifunza juu ya maana ya kusudi la maisha kwa mtu binafsi, na tumejifunza hatua 5 muhimu ambazo mtu anaweza kuzitumia katika safari ya kufahamu kusudi la maisha yake. Endelea kuzifuatilia hatua hizi kwani ndio msingi wa masomo haya ya kusudi la maisha.
Leo nataka tukajifunze juu ya Mamlaka ya Juu katika maisha yako kwa undani zaidi ili kutusaidia namna ya kuungana nayo kwa lengo la kufahamu kusudi la maisha yetu binafsi.
Sehemu kubwa ya waazi wa ulimwengu huu wanaamini juu ya uwepo wa Mungu au Muumba wa dunia yote hii. Bila kujali aina za imani au dini au mafundisho tuliyonayo au kutokana na asili yetu na nasaba zetu, kwa sehemu kubwa wanadamu wanakubaliana uwepo wa ‘Mamlaka ya Juu’ zaidi katika maisha yao yaani Mungu.
Ikiwa tunakubaliana na uwepo wa Mamlaka ya Juu au Muumba wa Mbingu na dunia, na kwamba sisi ni matokeo ya uumbaji wake, basi ni lazima ipo SABABU MAALUM kwa ajili yetu sisi kuwepo katika majira au nyakati hizi. Tuna ufahamu kupitia historia na maandiko mbalimbali juu ya uwepo wa mwanadamu katika karne nyingi zilizopita. Swali la kujiuliza kwa nini sisi hatukuwepo katika karne hizo zilizopita na tumeingia dunaini kati ya karne hii ya 20 na 21?
Lazima tufahamu ya kuwa hakuna kitu kinachotokea au mtu anayezaliwa kwa bahati mbaya, bila kujali namna mtu huyo alivyotungishwa mimba kwa mzazi wake. Inawezekana hatukuzaliwa ndani ya ndoa au familia, inawezekana sisi ni zao la kitendo cha kunyanyaswa kwa mama zetu, lakini ile kwamba tuliruhusiwa kutungishwa mimba kwa wazazi wetu basi tuwe na uhakika Mamlaka ya Juu ilikuwa na sababu ya sisi kuwepo katika majira haya.
Tunaweza kuona mfano huu kupitia andiko hili alilonena nabii Yeremia akisema
‘Neno la BWANA lilinijia, kusema, Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.’ Yer.1:4-5
Maneno haya hayakusemwa kwa Nabii Yeremia peke yake bali yanamuhusu kila binadamu anayevuta pumzi ya uhai sasa, ya kuwa kabla hata hatujaingia katika matumbo ya mama zetu tayari tulishajulikana na Muumba wetu na kabla hatujatoka tumboni tayari alishatutenga au kututakasa kwa kazi maalum kwa ajili yetu. Nabii Yeremia alitengwa kwa ajili ya kuwa nabii wa Mataifa.swali muhimu kwangu na kwako tumetengwa kwa ajili ya kazi gani? je tumetega sikio letu la ndani ili neno la Muumba wetu litujie kwa ajili ya kutujulisha kazi yetu au kusudi la kuwepo kwetu ambalo lipo kabla hata hatujaumbwa katika matumbo ya mama zetu?
Maneno haya yatusaidie kupata muda wa tafakari ndani yetu na kujiuliza na zaidi sana kumuuliza Muumba wetu juu ya hasa sababu ya mimi na wewe kuwepo hapa. Tusiridhike tu na kuzaliwa, kupata elimu, kufanya kazi au kuajiriwa, kuanzisha familia na kusomesha watoto kisha kuzeeka na kustaafu alafu kusubiri kifo. Si wote wanaweza kufikia mchakato huu wa kimaisha. Lakini hivi ni kweli kabisa Mungu ametuleta kwa sababu ya mchakato huu tu wa kimaisha au ana sababu ya ziada kwa ajili yetu?
Jua ya kuwa Mamlaka ya Juu ina ufahamu kuhusu wewe na mimi kuliko tunavyojifahamu, chukua hatua leo kutafakari na kuuliza juu ya kazi au kusudi la maisha yako binafsi ili uweze kuingia kazini leo.
Nikutakie baraka za Muumba katika kufuatilia hatua mbalimbali za kukuwezesha kulitambua kusudi la maisha yako na kulifanyia kazi.
Isaack Zake
Wakili, Mwandishi na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!