
Karibu sana ndugu msomaji wa makala mbalimbali katika mtandao huu wa isaackzake. Tunamshukuru Mungu sana kwa nafasi aliyotupa tena kukutana na wewe msomaji kwa njia ya makala hizi. Katika makala iliyopita tuliangalia hatua ya nne ambayo ni kumwomba Mungu akujulishe kuhusiana na kusudi la maisha yako.
Leo hii tunakwenda kuangalia hatua ya 5 ya kujua kusudi la maisha yako. Karibu sana.
Hatua ya 5 –Amini juu ya kulijua kusudi lako
Maisha yetu kwa sehemu kubwa yanaendeshwa na kile ambacho tumesikia na kuamini ndani yetu. Tulivyo leo ni matokeo ya imani ambayo tumeijenga katika siku zilizopita. Maisha ni imani. Ndio maana wazazi au walezi wanahakikisha wanapolea watoto wanawafundisha maadili mema na kuwapa mafunzo ya imani zao kwa lengo la kuishi maisha ya baadae vizuri zaidi.
Kama tulivyoanza kuangalia hatua moja baada ya nyingine za kufahamu kuhusiana na kusudi la maisha yako, tangu kutambua uwepo wa mamlaka ya Juu ambaye ni Mungu aliyekuumba, kutengeneza shauku ndani yako ya kutaka kujua kusudi la maisha yako, kutafuta maarifa juu ya kusudi la maisha yako na hatua ya nne ya kumwomba Mungu akujulishe kuhusiana na kusudi la maisha yako, imani ya kuliishi kusudi lako ni muhimu sana katika kulifikia na kulitimiza.
Labda unaweza ukawa unajiuliza imani ni nini? Hapa sizungumzii imani ya kidini bali suala la uhakika juu ya mambo unayotarajia katika maisha yako. Swali la msingi ni je, unatarajia kutoka ndani yako kulijua kusudi la maisha yako na hatimaye kuliishi kikamilifu?
Hatua zote hizi tulizopitia kujifunza tangu mwanzo haziwezi kuwa na maana kama hatutaweka msingi wa imani ndani ya mioyo yetu ya kuwa tutalijua kusudi la maisha yetu kwa uhakika na hatimaye tutachukua hatua madhubuti kuliishi kwa siku zetu zote tutakazojaliwa na Muumba wetu kuwepo katika mwili.
Imani katika maisha yetu ni kiungo muhimu sana kinachounganisha maarifa ya Kimungu ndani yetu na maarifa ya hapa duniani na kutufanya kuleta tofauti katika jamii yetu. Imani inatuunganisha na ulimwengu usioonekana na kusababisha kufanya vitu vinavyoonekana na kuleta faida kwa jamii zetu.
Je, unaamini wewe ni wa kipekee na wala hakuna mwenye kufanana na wewe hapa duniani? Je, unaamini wapo watu wakati huu wanaoishi kusudi la maisha yao? Je, unaamini ya kuwa na wewe unaweza kuishi kusudi la maisha yako ukitaka na kufuata hatua hizi tulizojifunza?
Watu wote waliopita au waliopo sasa ambao wameishi makusudi ya maisha yao, ambao tunanufaika na mchango wao mkubwa waliotoa na wanaoendelea kutoa katika jamii, si kwamba wao ni watu maalum sana kuliko sisi wengine au wana upendeleo maalum kutoka kwa Mungu, bali ni watu ambao wamechagua aina ya maisha ambayo wanataka kuishi kwa kuacha alama katika kizazi chao. Hii pia inawezekana kwako na kwangu kama tukifuata mchakato huu katika mwaka huu ili kubadili mkondo wa maisha ya kimazoea yasiyozaa matunda.
Nikutakie baraka za Muumba katika kufuatilia hatua mbalimbali za kukuwezesha kulitambua kusudi la maisha yako na kulifanyia kazi.
Isaack Zake
Wakili, Mwandishi na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!