
Karibu sana ndugu msomaji wa makala mbalimbali katika mtandao huu wa isaackzake. Tunamshukuru Mungu sana kwa nafasi aliyotupa tena kukutana na wewe msomaji kwa njia ya makala hizi. Katika makala iliyopita tuliangalia kuhusu hatua ya tatu ambayo ni kutafuta maarifa kuhusu kusudi la maisha yako.
Leo hii tunakwenda kuangalia hatua ya nne ya kujua kusudi la maisha yako. Karibu sana.
Hatua ya 4 –Mwombe Mungu akuoneshe kusudi la maisha yako
Moja ya eneo kubwa kabisa la kiimani bila kujali dini au imani za wanadamu ni suala la dua, sala au maombezi mbalimbali. Suala la maombi ni kitu cha msingi sana katika maisha ya mwanadamu. Huwa tunafundishwa au kujifunza mapema sana kuhusiana na maombi na tunaendelea na maisha hayo kwa muda wote wa maisha yetu.
Hatahivyo, si watu wengi wanapata muda wa kuomba kuhusiana na kusudi la maisha yao. Huwa tunamshirikisha Mungu katika masuala ya afya zetu, familia zetu, uchumi wetu, amani ya nchi yetu n.k lakini huwa hatumuhusishi katika eneo muhimu sana la maisha yetu yaani kupata ufahamu kuhusiana na kusudi la maisha yetu ni nini hasa.
Wengi ambao tumekuwa wazazi, tunapopata taarifa za kutarajia watoto huwa tunakuwa na shahuku kubwa sana na kusubiria kwa hamu kubwa juu ya ujio wa mtoto. Pale mtoto anapozaliwa huwa tunajawa na furaha kiasi cha kufanya hata sherehe na kumshukuru Mungu kwa kutupatia zawadi ya mtoto. Kisha tunaendelea na maisha yetu ya kulea na kupeleka watoto shule na hatimaye wanaondoka mikononi mwetu na kwenda kuanza maisha yao ya kujitegemea. Katika kipindi chote hiki huwa hatuna muda wa kuuliza kwa yule aliyemleta kwetu ni nini hasa kusudi la maisha ya mtoto husika ili tuweze kuwa na maarifa sahihi ya malezi yanayoshabihiana na kusudi la mtoto husika. Kwa kuwa sisi hatukuambiwa na wazazi wetu juu ya kusudi la maisha, vivyo hivyo hatua kitu cha kuwaeleza watoto wetu, tunaiacha dunia na mifumo yake kuwapa maana ya maisha na makusudi ya maisha yao.
Lakini maandiko yanatupa hekima na ufahamu thabiti ya kuwa kama wazazi au sisi vijana tunaweza kupata kufahamu makusudi ya maisha yetu au ya watoto wetu
‘Manoa akasema, Basi sasa hayo maneno yako yatakapotimia je! Huyo mtoto atakuwa wa namna gani na kazi yake itakuwa ni nini.’ Amu.13:12
Hili ni swali ambalo baba mzazi wa Samson, Mzee Manoa alimwuliza malaika wa Mungu kuhusiana na taarifa alizopokea kwa mke wake juu ya kupata mtoto wa kiume ambaye atawaokoa wana wa Israel kutoka kwa Wafilisti. (Soma. Am.13:1 -25). Wazazi hawa hawakuridhika tu na taarifa zilizoletwa ya kuwa watapata mtoto lakini walienda mbele zaidi kutaka kujua zaidi kuhusiana na kusudi la Mungu juu ya mtoto husika. Sisi nasi tumepata watoto au tumekuwa watu wazima na tuna mambo mengi tumemwomba Mungu na kupata majibu, je si wakati mwafaka sasa kumuuliza Mungu juu ya kusudi la maisha yetu ? au la basi tuulize hata kwa ajili ya watoto wetu, na Mungu mwenyewe atahakikisha anatujibu.
Isaack Zake
Wakili, Mwandishi na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!