
Karibu sana ndugu msomaji wa makala mbalimbali katika mtandao huu wa isaackzake. Tunamshukuru Mungu sana kwa nafasi aliyotupa tena kukutana na wewe msomaji kwa njia ya makala hizi. Katika makala iliyopita tulitambulisha au kukuletea makala iliyopita tumejifunza kujibu swali la nini maana ya kusudi.
Leo hii tunakwenda kuanza kuchambua hatua muhimu za kuweza kutambua kusudi la maisha yako binafsi. Karibu sana.
Kama tulivyoona katika makala zilizopita ya kuwa kila kitu kina kusudi lake na kila mtu ana kusudi maalum la maisha yake awe anajua au hajui. Lakini kwa bahati mbaya ni watu wengi sana katika maisha hawana ufahamu juu ya makusudi ya maisha yao bila kujali kiwango cha elimu yao au uwezo wao wa kimamlaka au kifedha bado hili ni hitaji kubwa ndani ya mioyo ya wanadamu wote.
Hatua ya 1 –Tambua mamlaka juu yako
Hatua muhimu sana katika kufahamu juu ya kusudi la maisha yako ni kuanza kufahamu juu ya uwepo wa mamlaka ya juu katika maisha yao. Kila imani au dini hapa duniani inatambua au inakiri juu ya uwepo wa Mungu. Hii ina maana ya kuwa kila mwanadamu anafahamu au anakiri uwepo wa Mungu aliyeumba mbingu na nchi.
Mungu muumbaji ni mamlaka ya juu ya kila kiumbe ikiwa ni pamoja na wanadamu wote. Tunafahamu kwa sayansi ya kawaida juu ya mtu anavyozaliwa kupitia wazazi wake katika mwili. Lakini utu wa mtu ni zaidi ya mwili wake ila roho iliyo ndani yake ambayo inakaa ndani ya mwili. Ili tuweze kufahamu kuhusiana na kusudi la maisha yetu ni muhimu sana kutambua na kukubali ya kuwa ipo mamlaka kuu yenye kuhusiana na maisha yetu ambaye ni Mungu aliyetuumba sisi sote.
Tunaweza kuuona ukweli huu kupitia maandiko haya;
‘Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono; wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu cho chote; kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na pumzi na vitu vyote. Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao; ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu. Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda na kuwa na uhai wetu.’ Mdo.17:24 – 27
Kwa maandiko haya tunaweza kuona juu ya mamlaka ya juu kwa viumbe vyote ni Mungu muumbaji aliyeufanya ulimwengu wote. Lakini pia zaidi ya hayo ndiye aliyewafanya wanadamu wote na kuwapa pumzi ya uhai. Hivyo kila mmoja wetu kwa njia yoyote awe anaamini katika Mungu au la bado Mungu yu karibu yake zaidi ya pumzi anayopumua kila wakati. Utambuzi wa mamlaka ya juu kwa mwanadamu ndio hatua muhimu ya kwanza katika kuelekea kufahamu kusudi maalum la maisha yako hapa duniani.
Isaack Zake
Wakili, Mwandishi na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!