
Karibu sana ndugu msomaji wa makala mbalimbali katika mtandao huu wa isaackzake. Tunamshukuru Mungu sana kwa nafasi aliyotupa tena kukutana na wewe msomaji kwa njia ya makala hizi. Katika makala iliyopita tulitambulisha au kukuletea makala ya utangulizi kuhusiana na ‘kusudi la maisha’.
Leo hii tunakwenda kujibu swali ni nini maana ya Kusudi? Karibu sana ufuatane nami ili tujifunze zaidi.
Kwa tafsiri ya kawaida neno ‘kusudi’ linajibu swali ambalo linataka kujua sababu ya uwepo wa kitu au kufanyika kitu fulani. Kusudi inaweza pia kutafsiriwa kama ‘dhumuni au kiini’ cha kitu fulani. Kwa hivyo tunapozungumzia kusudi la maisha ya mwanadamu ina maana sababu ya msingi ambayo inamfanya mwanadamu huyo kuwepo.
Si watu wengi sana wanafahamu kuhusiana na kusudi lao binafsi kwa nini wapo mpaka sasa na kwa nini wamezaliwa katika familia au taifa walilopo sasa. Watu wengi wanazaliwa, wanakua na wanaambiwa kwa njia mbalimbali za mifumo ya kibinadamu juu ya wao kuwa nani na wanapaswa kufanya nini.
Nikukuuliza wewe ndugu msomaji wangu swali hili, je nini kusudi la kuwepo kwako au la maisha yako? Utajibu vipi?
Kila mtu ana sababu ya kuwepo hapa duniani, lakini si wote wanafahamu kuhusiana na sababu hiyo na hivyo huishi maisha yao kama wanavyoona wao. Tunafahamu ya kuwa sisi sote asili yetu inatokana na Mungu mwenyewe kama maandiko matakatifu yanavyotueleza;
‘Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono; wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu cho chote; kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na pumzi na vitu vyote. Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao; ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu. Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda na kuwa na uhai wetu.’ Mdo.17:24 – 27
Kupitia maandiko haya tunaweza kujifunza mambo mengi sana kuhusiana na ukuu wa Mungu aliyeziumba Mbingu na nchi na juu ya mamlaka yake kwa kila mmoja wetu, ili itusaidie kufahamu ni nini hasa kusudi la maisha yetu, na kwamba ni Mungu peke yake mwenye uweza wa kujibu hitaji letu hili.
Kama wote tunaamini ya kuwa sisi tu viumbe wa Mungu na kwamba Yeye ndiye aliyetuumba na anajua hatma ya maisha yetu basi tuwe na uhakika ya kuwa Mungu pekee ndiye anayejua kusudi la kuwepo kwa kila mmoja wetu. Hakuna Serikali au mwanadamu anayeweza kukuonesha kusudi lako isipokuwa Mungu mwenyewe.
Isaack Zake
Wakili, Mwandishi na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Yes