
Karibu sana ndugu msomaji wa makala mbalimbali katika mtandao huu wa isaackzake. Tunamshukuru Mungu sana kwa nafasi aliyotupa tena kukutana na wewe msomaji kwa njia ya makala hizi.
Katika makala iliyotangulia tuliangalia Kanuni ya 2 inayosema Mungu aliumba kila kitu kwa Kusudi. Leo hii tunaangalia kanuni ya 3 inayosema Si kila Kusudi linajulikana kwetu.
Si kila Kusudi linajulikana kwetu
Pamoja na kwamba katika Kanuni ya 1 tumeona ya kuwa Mungu ni wa Kusudi na kwamba kila alichokiumba ndani yake kina kusudi maalum kama tulivyoona kwenye Kanuni ya 2, lakini ajabu ni kwamba Si kila Kusudi linajulikana kwetu.
Hii ndiyo hali ambayo wengi wetu tumeirithi kutokana na asili ya uasi wa Adam. Wanadamu tumepoteza ule ushirika na Mungu ambaye ndiye asili ya uhai wetu na kutujulisha juu ya makusudi yake. Ndio maana tunaona kila kukicha watu wanakimbizana na mambo mengi lakini mwisho wa siku hakuna cha maana wanachokamilisha au ndani ya maisha yao kunakosekana utoshelevu.
Ukosefu wa makusudi au kutokujua juu ya makusudi katika uumbaji na viumbe vya Mungu umeleta hasara kubwa sana kwa wanadamu. Tumekuwa tukishuhudia watu wakipigana, mataifa yakiingia katika migogoro, makabila yakiuana n.k
Tunaweza kuona ukweli huu kimaandiko juu ya sisi wote kuwepo ndani ya kusudi lake
‘Mungu aliyeufanya ulimwengu wote na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono; wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu cho chote; kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na pumzi na vitu vyote. Na alifanya kila taifa la wanadamu kutoka mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao; ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu’ Mdo.17:24-27
Kama maandiko yanavyoonesha ya kuwa Mungu aliwafanya watu wote kutoka mmoja yaani Adam na kisha akawapa amri ya kukaa juu ya nchi yote yaani dunia nzima na mipaka ya makazi yao na mataifa yao aliiweka Mungu. Lakini kila kukicha utasikia ugomvi baina ya mtu na jirani yake. Hii ni kwa sababu wengi hatujui kwa nini tupo mahali tulipo. Moja ya migogoro mikubwa sana duniani ni migogoro ya ardhi. Wapo watu wengi sana wanagombania na kuuana kwa ajili ya ardhi.
Kutokujua kusudi ni hasara kubwa sana kwetu sisi wanadamu, kuna watu wapo kwenye mataifa wanalaumu ni kwa nini walizaliwa hapo wanaona ni afadhali wangezaliwa nchi nyingine hata kama ni wanyama. Hiki ni kiwango kikubwa sana cha upotovu wa kutokujua ni sababu gani hasa Muumba alikuwa nayo aliporuhusu tuzaliwe katika familia, kabila, taifa na bara tulilopo.
Sisi tunao wajibu wa kwenda kwake kuuliza kuhusu kusudi la maisha yetu, ili tuweze kubadilisha mazingira yetu na kutawala ipasavyo.
Isaack Zake
Wakili, Mwandishi na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!