Karibu sana ndugu msomaji wa makala mbalimbali katika mtandao huu wa isaackzake. Tunamshukuru Mungu sana kwa nafasi aliyotupa tena kukutana na wewe msomaji kwa njia ya makala hizi.
Katika makala iliyotangulia tulianza kuangalia kanuni za msingi za Kusudi kwa kuitazama Kanuni ya 1 inayosema Mungu ni wa Kusudi. Leo tunaendelea kujifunza Kanuni ya 2 inayosema Mungu aliumba kila kitu kwa Kusudi.
Mungu aliumba kila kitu kwa Kusudi
Nadhani ulishawahi kusikia mtu au habari za watu wakisema wao hawana thamani na hakika hawastahili kuishi hapa duniani. Tuna hadithi za watu wengi waliojizuru au kuondoa uhai wao kwa sababu ya kuona hawana mwelekeo wa maisha. Kile ambacho wasichojua kuhusu maisha yao ni kwamba wapo kwa kusudi maalum. Haitoshi tu kwa wanadamu kufahamu ya kuwa wanalo kusudi la maisha yao, bali Kanuni hii inahusisha kila kiumbe kilichopo duniani na hata nje ya dunia vipo kwa makusudi maalum.
Hakuna kitu au kiumbe kipo mahali au kilizaliwa kwa bahati mbaya. Kila kitu kipo hapa kwa kusudi maalum. Mbali na Mungu kuumba kila kitu kwa ajili ya Kusudi maalum, ndani ya kila kiumbe ameweka uwezo wa kiumbe husika kutimiza kusudi la kuwepo kwake. Tunaona kwa mfano ndege ameumbwa kuruka na ndivyo alivyotengenezwa na uwezo wa kuruka. Mwanadamu ameumbwa kutawala na ndani yake amewekewa uwezo huo wa kutawala mazingira yake.
Tunaweza kuona ukweli huu kupitia andiko hili
‘Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. Mwa.1:26 -27
Katika maisha yetu tunakumbana na changamoto mbalimbali za kimazingira ambazo zinaweza kuonekana ni ngumu sana katika maisha yetu, lakini tuwe na uhakika kuwa ndani yetu kila mmoja ana uwezo wa kukabiliana na changamoto zake za kila siku na kutawala mazingira yake.
Suala la mwanadamu kuwa na uwezo wa kuyatawala mazingira yake halitokani na elimu ya darasani, aina ya kabila au utaifa, aina ya rangi au hadhi ya kimaisha, bali ni kusudi ambalo lipo ndani ya kila mmoja wetu.
Hivyo, siku ya leo bila kujali changamoto ulizonazo au nilizonazo ni lazima tufahamu ya kuwa kila kiumbe kiliumbwa kwa kusudi maalum, kwa upande wetu sisi wanadamu tuliumbwa kuyatawala mazingira yetu kwa ukamilifu. Hilo ndilo kusudi la sisi kuwepo na uwezo huu upo ndani yetu. Tuamshe sasa uwezo huu ndani yetu na kuanza kuchukua hatamu ya maisha yetu kiutawala.
Ninakutakia siku njema katika kutimiza kusudi la maisha yako kama mwanadamu.
Isaack Zake
Wakili, Mwandishi na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!