
Karibu sana ndugu msomaji wa makala mbalimbali katika mtandao huu wa isaackzake. Tunamshukuru Mungu sana kwa nafasi hii ya kuanza mwaka mwengine wa 2021. Kila mmoja wetu amepitia changamoto mbalimbali katika mwaka uliopita 2020 lakini mpaka sasa bado tupo salama ni jambo la kushukuru sana.
Leo tunaanza kuleta mfululizo maalum wa kujifunza kuhusiana na ‘KUSUDI LA MAISHA’ au kwa tafsiri ya kiingereza ‘LIFE PURPOSE’. Huu utakuwa mfululizo wa makala na masomo maalum kwa kila mmoja wetu mwenye nia ya kujifunza kutafuta na kutumikia kusudi la maisha yake hapa duniani.
Nimesukumwa kuanza kuandika makala hizi kwa lengo la kuamsha ari ya watu wengine na wengi zaidi kufahamu ni nini hasa makusudi ya wao binafsi kuwepo hapa duniani. Leo ni tarehe 4 Januari 2021 ni siku ya kumbukizi ya kuzaliwa kwangu ni jambo la kushukuru. Ninajua wapo watu wengi wa umri wangu au walio chini ya umri huu lakini wamemaliza safari yao hapa duniani pasipo kufahamu ni nini hasa walikuja kufanya. Hivyo kwa neema za Mungu aliyenijalia umri huu na uzima huu mpaka sasa kushirikisha kwa sehemu kile ambacho ninafahamu kuhusiana na KUSUDI LA MAISHA.
Hakuna mwanadamu au kiumbe chochote kilichopo hapa duniani kwa bahati mbaya au pasipo kuwa na kusudi la maisha. Kila kitu kipo hapa na kila mtu yupo hapa kwa sababu maalum. Lakini si watu wengi wanafahamu juu ya kusudi la maisha yao. Wengi wanaishi kwa muda mrefu miaka hata 70 au 80 au hata 100 lakini hawajawahi kuwa na ufahamu ni kwa nini walizaliwa walipozaliwa na kwa nini Mungu aliwapa maisha eneo alilowapa n.k
Maandiko matakatifu kupitia kitabu cha Muhubiri yanatueleza wazi juu ya majira yetu na makusudi ya maisha kwa kila mmoja wetu.
‘Kwa kila jambo kuna majira yake Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; wakati wa kupanda, na wakati wa kung’oa yaliyopandwa; Muh.3:1 – 2
Tunaelezwa hapa juu ya wakati na majira juu ya kila kitu, lakini pia ndani ya huo wakati na majira hayo kuna kusudi ambalo linapaswa kutimizwa au kukamilishwa. Watu wengi tunafurahia sana kuhusiana na kuzaliwa kwetu hasa tunapopata mwaka mwengine wa kumbukizi ya maisha yetu, lakini kile tusichojua ni nini hasa kusudi la kuzaliwa kwetu na iwapo tumeanza kutekeleza ile sababu kuu ya sisi kuwepo hapa duniani.
Maandiko pia yanafafanua ya kuwa upo wakati wa kuzaliwa na upo wakati wa kufa. Jambo hili haliepukiki kwa kila kiumbe. Hofu kuu ya watu katika suala la kifo inaweza kuchangiwa kwa sehemu kubwa kutokana na kutokujua ni nini hasa sababu ya maisha ya mtu mwenyewe. Mtu anayejua kuhusiana na kusudi la yeye kuwepo na kisha akalitekeleza kwa ukamilifu, kifo hakiwezi kuzua hofu kwake lakini atakikaribisha kwa furaha kwa maana anakuwa amemaliza KUSUDI LA MAISHA YAKE hapa chini ya mbingu.
Ni maombi yangu kwa Mungu katika mwaka huu 2021 na miaka mingine ijayo akujalie wewe ndugu msomaji wa makala hizi kufahamu kwa hakika ni nini kusudi la maisha yako na kisha kuchukua hatua sahihi ndani ya muda sahihi kutekeleza makusudi hayo katika muda wote utakaojaliwa kuwepo chini ya mbingu.
Isaack Zake
Wakili, Mwandishi na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Asante wakili
Karibu sana Neema