
Utangulizi
Karibu tena ndugu msomaji katika mfululizo wa makala hizi za kujifunza juu ya maana ya kazi kwa lengo la kuboresha maisha yetu kila siku na kusaidia watu wengi ambao wanapaswa kufanya kazi ili kuingia kazini.
Katika mfululizo wa makala za tofauti ya kazi na ajira tumeanza kwa kuangalia maana ya neno kazi katika makala iliyotangulia. Leo tunazidi kuichambua maana hii ili kukujengea msingi muhimu wa kutofautisha kati ya neno ‘kazi’ na ‘ajira’ karibu sana.
Maana ya Kazi
Tuliona ya kuwa neno ‘work’ lina maana ya ‘an activity involving mental or physical effort done in order to achieve a purpose or result’. Kwa tafsiri isiyo rasmi tunaweza kusema kazi ni shughuli inayohusisha akili au nguvu za mwili kwa lengo la kufikia kusudi au kupata matokeo yaliyokusudiwa.
Kwa kuitazama tafsiri hii tunaweza kupata mambo yafuatayo ndani ya neno ‘kazi’
- Kusudi au lengo; ili kazi iwepo ni lazima kuwe na kusudi au sababu ya mtu kufanya au kutaka kufanya kile anachofanya. Lazima mtu awe na sababu kwa nini anatumia akili yake au nguvu zake kufanya anachofanya.
- Matumizi ya akili au nguvu; kazi inahusisha matumizi ya akili au nguvu au vyote kwa pamoja yaani akili na nguvu. Haitoshi tu kuweka lengo au kuwa na kusudi lazima hatua zichukuliwe kufanya kitu kwa kutumia akili na nguvu ili kupata matokeo yanayotarajiwa.
- Matokeo; matokeo ni zao la kazi. Yapo matokeo ya aina nyingi inategemea kusudi la mtenda kazi alilokuwa nalo kabla hajawekeza akili na nguvu zake katika kazi husika. Mtu anaweza kupata matokeo ya furaha kama lengo ilikuwa kufurahi au kuona wengine wakisaidika kama lengo ilikuwa kutoa msaada kwa kazi yake au kupata fedha kama lengo la kazi ilikuwa fedha.
Hivyo mtu akisema anafanya kazi maana yake ana kusudi ndani yake ambalo analifikia kwa kuweka akili yake na nguvu zake kwenye matendo ili hatimaye apate matokeo aliyokusudia. Hii ndio maana halisi ya neno kazi. Hivyo mtu yeyote mwenye lengo au kusudi na kuwekeza muda wake akili yake na nguvu zake kuhakikisha anafikia lengo lake basi huyo ni mfanyakazi au mtenda kazi.
Nisisitize ya kuwa si lazima lengo la mtu huyo liwe kupata fedha bali anaweza kuwa anafanya anachofanya kwa malengo mengine kabisa labla kubadilisha maisha ya watu au kuleta furaha au kusaidia n.k
Asiyetaka kufanya kazi na asile…’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!