
Utangulizi
Karibu tena ndugu msomaji katika mfululizo wa makala hizi za kujifunza juu ya maana ya kazi kwa lengo la kuboresha maisha yetu kila siku na kusaidia watu wengi ambao wanapaswa kufanya kazi ili kuingia kazini.
Watu wengi wanafahamu ya kuwa kazi ni sawa na ajira au mtu akiwa ameajiriwa ndio anafanyakazi. Ndio maana mtu anaweza kuitwa mfanyakazi au mwajiriwa. Maneno haya yote yanaweza kutumika kumaanisha dhana moja. Hatahivyo, ipo tofauti kubwa sana kati ya maneno haya mawili yaani ‘kazi’ na ‘ajira’. Kushindwa huku kutofautisha maana ya maneno haya kumewafanya watu wengi kufikiri kwa sababu wameajiriwa basi ni wafanyakazi na wale wafanyakazi kufikiri wao ni waajiriwa.
Ni muhimu sana katika maisha kwenye jambo lolote mtu ujue tafsiri sahihi kuhusiana na jambo husika. Kama ukifahamu tafsiri halisi ya neno ‘kazi’ na tafsiri ya neno ‘ajira’ inaweza kusaidia sana kubadili mfumo wako wa maisha. Katika mfululizo wa makala hizi za maana ya kazi tunakwenda kujifunza juu ya tafsiri ya maneno haya na tofauti zake ili kukusaidia kujua kilicho muhimu katika maisha yako na kuchukua hatua stahiki.
Maana ya Kazi
Ukisoma katika kamusi ya kiingereza neno kazi linatafsiriwa kama ‘work’. Kwenye kamusi ya kiingereza neno ‘work’ ikiwa na maana ya ‘an activity involving mental or physical effort done in order to achieve a purpose or result’. Kwa tafsiri isiyo rasmi tunaweza kusema kazi ni shughuli inayohusisha akili au nguvu za mwili kwa lengo la kufikia kusudi au kupata matokeo yaliyokusudiwa. Hii ina maana kuwa neno kazi linausisha uwezo wa mtu kutumia akili yake au nguvu zake katika kufanya jambo au shughuli ili kufanikisha lengo au kusudi au kupata matokeo anayotarajia.
Kwa mantiki ya tafsiri hii tu ya neno tunaona kazi si lazima ihusishe kupatikana kwa fedha ingawa fedha inaweza ikawa mojawapo ya matokeo ya kazi.
Endelea kufuatilia makala hizi tunapoifafanua zaidi maana ya ‘kazi’
Asiyetaka kufanya kazi na asile…’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!