Kipaji.7. Changamoto ya Kutonoa kipaji
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu katika mafunzo juu ya Kipawa/Vipawa katika ukurasa huu wa vipaji. Katika makala iliyopita tuliona changamoto ya Umri kumzuia mtu kutumia kipaji chake. Leo tunaangalia sababu nyingine ni Kutonoa kipaji
Sababu 4. Changamoto ya Kutonoa Kipaji
Tunafahamu ya kuwa kipaji ni zawadi ya bure ambayo mtu huzaliwa nayo. Kila mtu anacho kipaji iwe anakijua au hakijui lakini anacho kipaji. Unaweza kuvuka kihunzi cha kutokujua kipaji chako na ukapata kukifahamu mapema lakini bado ukakwamishwa na kutoweza kukitumia kipaji hicho kwa kutojizoeza kunoa kipaji chako.
Wengi wetu tunafuatilia sana juu ya wanamichezo hasa wa mpira wa miguu au kikapu au wakimbiaji mbalimbali. Tunawatazama watu hawa na kuwaona ni wa tofauti sana na sisi kwa sababu ya uwezo na ujuzi wanaoonesha katika vipaji vyao. Kitu muhimu ambacho tunashindwa kukifuatilia ni kuwa wana utaratibu wa kunoa vipaji vyao katika maisha yao ya kila siku. Ndio maana hata mchezaji awe na kipaji kiasi gani ni lazima afanye mazoezi ili kupata nafasi ya kucheza kwenye timu.
Mazoezi au kunoa kipaji ndio siri ya kujitofautisha na watu wengine wenye kipaji cha aina yako. Kama wewe ni mwimbaji mzuri hatutaweza kukujua kati ya waimbaji wengi kama huna mazoezi ya kujitofautisha na wengine wengi. Kunoa kipaji ndio msingi wa kujitofautisha na wengine wenye kipaji kama chako.
Unaweza ukawa na sifa nzuri kama mchoraji au mwandishi au mwigizaji lakini kama hutuoni namna unavyojinoa na kujifua kila siku basi utaishia kusema mimi mwenyewe naweza lakini wengine wenye kipaji kama chako wataonekana kwa sababu wanawekeza muda mwingi kunoa vipaji vyao.
Haitoshi tu kusema unacho kipaji hakikisha unaweka mpango mkakati wa kunoa kipaji chako kila siku ili kikutofautishe na wengine wengi wenye kipaji kama chako.
‘Kipaji changu, fursa yangu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!