Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu katika mafunzo juu ya Kipawa/Vipawa katika ukurasa huu wa vipaji. Katika makala iliyopita tulianza kujiuliza swali la ‘Kwa nini watu hawawekezi kwenye vipaji vyao?. Tuliangalia sababu ya 2 ya watu wengi kutokutumia vipaji vyao. Leo tunaangalia sababu nyingine inayowazuia watu kuwekeza kwenye vipaji vyao.
Sababu 3. Changamoto ya Umri
Kama tulivyoona katika makala zilizotangulia ya kuwa kipaji au vipaji ni kitu cha asili yaani mtu anazaliwa nacho au anazaliwa navyo. Inawezekana kabisa kwa muda wote mtu asijue kuhusiana na kipaji au vipaji alivyojaliwa na Mwenyezi Mungu mpaka akafikia umri mkubwa. Kama tunavyofahamu juu ya mifumo yetu ya maisha husisitiza zaidi suala la mfumo rasmi wa elimu hivyo watu wengi hujikuta wanaweka msisitizo katika mfumo wa elimu na hawana muda kwenye vipaji vyao.
Watu hawa hutumia muda mwingi kabisa katika kujishughulisha na kazi zinazoambatana na elimu yao na kuacha kwa muda mrefu kuhusiana na vipaji vyao. Lakini kwa njia moja ama nyingine baada ya muda mrefu wanakuja kufahamu kuhusu vipaji vyao.
Wengi wakifikia umri mkubwa wanakata tamaa katika kuwekeza kwenye vipaji vyao wakiona hawana nafasi tena ya kufanya vizuri kwa sababu ya umri ulivyoenda. Wengine wanafahamu wakiwa na umri kama miaka 40 au 50 au 60 pale wanapostaafu kazi zao au utumishi wao.
Qn. Je, wewe ni miongoni mwa watu ambao umegundua kipaji chako na unaona umri wako ni mkubwa?
Jambo hili lisikusumbue wala lisikukukatishe tamaa hata kidogo bali unachopaswa ni kumshukuru Mungu na kuanza kufanyia kazi kipaji chako. Kipaji ni nyenzo ya asili ambayo Mungu amekupatia kwa lengo la kufanikisha mambo kwa ufanisi mkubwa zaidi. Mtu mwenye kipaji huwa hastaafu mpaka pale anapofariki. Hivyo bado una nafasi ya kubadilisha maisha yako na ya watu wengine kwa kutumia kipaji chako hata kama unaona muda umeenda.
Unaweza kuwa umefahamu juu ya kipaji chako kilikuwa cha kucheza mpira lakini sasa umri umeenda unaweza kufanya nini? Wekeza kwa kizazi kinachokuja kwa kufundisha au kuelekeza nidhamu inayohitajika katika michezo. Labda kipawa chako ni kuongoza lakini hukukitumia, unayo nafasi ya kushauri au kufundisha namna ya wengine kuwa viongozi bora katika siku zijazo.
Jambo muhimu la kufahamu ni kuwa kipaji chako hata kama umekigundua baada ya umri mkubwa bado unaweza kukitumia kwa ufanisi mkubwa na kuleta mabadiliko.
Kamwe usiache kutumia kipawa chako kwa sababu ya changamoto ya umri kwani huwezi kujua ni wangapi walikuwa wanasubiri uingize kazini kipaji chako ili nao waweze kunufaika.
‘Kipaji changu, fursa yangu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!