
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu katika mafunzo juu ya Kipawa/Vipawa katika ukurasa huu wa vipaji. Katika makala iliyopita tulianza kujiuliza swali la ‘Kwa nini watu hawawekezi kwenye vipaji vyao?. Tuliangalia sababu ya 1 ya watu wengi kutokujua kuhusu kipaji au vipaji vyao. Hii ni sababu kubwa sana ambayo inawazuia watu wengi kutowekeza kwenye vipaji vyao. Leo tunaangalia sababu nyingine inayowazuia watu kuwekeza kwenye vipaji vyao.
Sababu 2. Kutokutumia Kipaji
Kuna watu wanabahatika kufahamu au kujua kipaji walichojaliwa na Mungu lakini kwa bahati mbaya sana hawakitumii. Tumeona mifano mingi sana na tunao ndugu wengi ambao tunafahamu uwezo wao katika maeneo mbalimbali kama fani za muziki, sanaa za michezo, uandishi, uongozi, kufundisha, ufundi n.k lakini hawajaweka nguvu zao katika kuvitumia vipaji hivi.
Watu hawa wanaweza kuwa na sababu mbalimbali za kuwazuia kutumia vipaji vyao lakini wasichojua ni kuwa kipaji ndio nyenzo kuu nay a asili ambayo kila mmoja wetu amepewa kwa lengo la kufanikisha makusudi yake duniani. Hivyo sababu hizi hazina uzito wowote wa kumzuia mtu asitumie kipaji chake.
Tunaweza kuona baadhi ya sababu wanazotumia watu kutokuwekeza katika vipaji vyao au kutokutumia vipaji vyao;
Sababu zinazopelekea watu wasifuatilie kujua kuhusu vipaji
- Mtazamo ya kuwa vipaji au kipaji hakina mchango wowote katika uchumi binafsi. Watu wengi wamekuwa hawatumii vipaji vyao kwa sababu ya kutoona fursa ya kiuchumi inayoambatana na kipaji chake, hivyo anaona kutumia kipaji hicho ni kupoteza muda. Kile ambacho wengi hawajui ni kuwa fursa huambatana na pale unapoanza kukitumia kipaji chako na kuonekana na wengine.
- Kisingizio cha kukosa muda wa kutosha kwa ajili ya kutumia kipaji chako. Dhana hii pia imekuwa ikiwazuia baadhi ya watu kutokumia kipaji au vipaji vyao kwa sababu ya muda. Wengi husingizia kuwepo kwenye masomo au kuwa na kazi nyingi hata kukosa muda wa kupumzika. Kitu ambacho watu hawa hawatambui ni kipaji peke yake ndicho kinaweza kukutengenezea muda wa ziada kwa sababu kinakuwezesha kupata matokeo makubwa kwa muda mdogo au nguvu kidogo. Unaweza kusubiri mpaka uwe na muda unajikuta umeshachelewa. Uwekezaji kwenye kipaji chako kwa matumizi hata kidogo kidogo unakusaidia kurudisha uhuru wako.
- Dhana ya kufikiri wapo wenye vipaji bora zaidi yako hivyo huna sababu ya kutumia kipaji chako. Hali hii hata mimi ilikuwa inanisumbua ndani yangu. Unaweza kukuta una kipawa cha kuandika au kuchora lakini kila ukitazama kazi za wenzako unaziona ni bora zaidi yako hivyo unadhani huna nafasi. Dhana hii si kweli kwani pamoja na kuwa tunaweza kuwa na vipaji vinavyofanana lakini kila mmoja ana watu wake au mashabiki wake wanaoweza kufuatilia kazi zake.
Ndugu msomaji, hizi ni sababu tu chache ambazo zinawazuia watu wengi kutokutumia vipaji vyao. Je, wewe ni miongoni mwao unayezuiwa na sababu hizi au sababu nyingine yoyote? Haipaswi kuwa hivyo usikubali sababu yoyote kukuzuia kutumia kipaji chako iwe suala la muda, uchumi au ubora za kazi za wengine wenye vipawa kama vyako. Wapo watu ambao kwa matumizi ya kipaji chako watabadilishwa na kuboresha maisha yao.
Embu fikiri kama na mimi ambaye ninaandika hapa nisingetengeneza mazingira ya matumizi ya kipaji changu cha uandishi ni dhahiri usingepata andiko hili siku ya leo. Fikiria dunia ina watu zaidi ya Bilion 7.7 wote hawa wana vipaji tofauti na wewe pia unacho chako na wapo washabiki wako wanaokusubiri ukitumie. Usiache nafasi hii ya kutumia kipaji chako kama unakijua.
‘Kipaji changu, fursa yangu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!