
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu katika mafunzo juu ya Kipawa/Vipawa katika ukurasa huu wa vipaji. Katika makala iliyopita tuliangalia namna ya kupima kipaji chako. Makala ya leo tunajiuliza swali ‘Kwa nini watu hawawekezi kwenye vipaji vyao? Karibu sana tujifunze.
Zinawezekana kuwepo sababu nyingi sana ambazo zinawafanya watu wasiwekeze katika vipaji vyao au vipaji vya watu wengine. Kama tulivyoona katika makala zilizotangulia ya kuwa kipaji ni uwezo wa asili wa kutenda mambo makubwa na yenye matokeo bora kwa kutumia nguvu au rasilimali kidogo. Pamoja na kuona manufaa makubwa sana ya matumizi ya kipaji au vipawa katika maisha ya wanadamu, bado si wengi wanawekeza katika kutumia au kuendeleza vipaji vyao.
Katika mfululizo huu tutakwenda kuangalia angalau sababu 5. Leo tunaanza na sababu ya 1 yenye kujibu swali la kwa nini watu hawawekezi katika vipaji vyao.
Sababu 1. Kutokujua kuhusu kipaji au vipaji alivyonavyo mtu binafsi
Mfumo wa maisha yetu sisi sote tunapozaliwa, tunalelewa na wazazi au walezi wetu. Hawa wanaotulea wana athari kubwa sana katika namna tutakavyoendesha maisha yetu siku zijazo. Wazazi au walezi wana nguvu kubwa ya kuamua juu ya kazi au huduma ambazo tutakuja kutumika katika jamii.
Mifumo ya malezi hasa kwa watoto wa bara la Afrika haijali sana katika vipaji ila suala zima la mfumo wa elimu. Nchi zilizoendelea zina mfumo tofauti sana na wanatazama zaidi kipaji au vipaji vya mtu kama sehemu ya kujenga mfumo wa maisha yake na kuendeleza zaidi kiuchumi.
Aina ya wazazi ambao tumezaliwa kwao hawakulelewa katika misingi ya kugundua vipaji vyao au kuviendeleza bali msingi mkubwa waliojengewa na wazazi wao ni suala la ELIMU au shughuli za kiuchumi walizorithi kwa wazazi wao kama kilimo, uvuvi na ufugaji. Kutokana na hali hii wazazi hawa hawana mfumo wa kuwezesha watoto wao kugundua au kuwasaidia kuwekeza katika vipaji vyao.
Sababu zinazopelekea watu wasifuatilie kujua kuhusu vipaji
- Kusisitizwa kwa mfumo wa elimu katika maisha ya watoto kuliko vipaji vyao
Tunapokuwa watoto tunapelekwa katika shule na kusisitizwa kuzingatia masomo yetu zaidi ya kitu chochote. Wazazi wengi walichukulia suala la michezo kwa watoto kama utovu wa kinidhamu. Watoto wengi wamezimwa ndoto zao kwa sababu ya msisitizo wa mfumo wa elimu. Wengi wamepoteza fursa za kutumia au kujua vipawa vyao kwa sababu tunadhani elimu pekee ndio mfumo rasmi wa kusaidia watu katika maisha yao ya kila siku.
- Kutokuhusianisha vipaji vya mtu na mafanikio ya kimaisha
Wazazi wengi hawajaweza kufanya tathmini ya kina katika kupima mafanikio ya kimaisha kutokana na vipawa vyao. Tunaona ya kuwa vipaji havina mchango mkubwa katika maisha yetu ya kila siku. Tunafikiri ya kuwa watu wote wanapaswa kufuata aina fulani ya mfumo wa maisha.
- Kuhusianisha vipaji na uhuni au mwenendo mbaya kitabia
Wazazi wengi wamekuwa wakikemea watoto wao wasijihusishe na masuala ya vipaji kwa sababu ya kutazama mwenendo wa watu maarufu kwa vipaji vyao. Tunaona wanamuziki wakubwa, au wachezaji mpira wakihusianishwa na kashfa mbalimbali. Hali hii inasababisha watu wengi kudhani ya kuwa vipaji huharibu mwenendo au tabia njema ya mtu. Kwa mtazamo huu wengi hawajishughulishi na vipaji kwa sababu wanaona ni eneo ambalo linaweza kuhatarisha maadili ya mtoto au kijana.
Kujua kuhusu kipaji chako au mtoto wako ni jambo muhimu sana katika safari ya kuanza kuwekeza. Kipaji ni mtaji mzuri kama utaufuatilia na kuwekeza vizuri. Haipaswi kufikiri ya kuwa kipaji huaribu tabia ya mtu. Mtu yeyote anaweza kujenga tabia yake pamoja na kipawa alicho nacho. Pia ieleweke ya kuwa wapo wenye elimu kubwa na maarifa mengi lakini hawana maadili mema katika jamii. Hatahivyo, tumeanza kuona mabadiliko kwa wazazi wa kipindi hiki wanaanza kufuatilia na kuwekeza katika vipaji vya watoto wao.
Wito wangu kwa wazazi wote, kama kuna eneo linahitaji uwekezaji wetu mkubwa zaidi hata kuliko mfumo wa elimu, ni UWEKEZAJI katika KIPAJI cha mtoto au watoto wako. Hii ni njia nzuri sana ya kuwajengea fursa kubwa zaidi katika maisha yao na kwa hakika hata wewe kitakunufaisha siku zijazo.
‘Kipaji changu, fursa yangu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!