
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu katika mafunzo juu ya Kipawa/Vipawa katika mtandao wa isaackzake. Ukurasa huu ni maalum kwa ajili yako kujifunza mambo yote kuhusu kipawa au vipawa vyako. Hapa utapata makala, mifano mbalimbali kuhusu kipawa au vipawa vyako na kutambua kipawa chako. Tutajifunza namna mbalimbali za kunoa au kuboresha kipawa chako kila siku na nidhamu unayohitaji ili kipawa kilete faida kwenye maisha yako. Kipawa ni moja ya rasilimali muhimu sana katika maisha ya mwanadamu ambayo akiitambua na kuitumia vizuri humtofautisha na watu wengine na huvuta watu kwake kila siku. Karibu sana tujifunze kwa pamoja juu ya namna ya kupima kipaji chako.
Nadhani tunakumbuka ile tafsiri ya kipaji au kipawa inavyosema
Kipaji ni uwezo wa asili wa kutenda mambo makubwa na yenye matokeo bora kwa kutumia nguvu na rasilimali ndogo ukilinganisha na watu wengine.
Kwa kuitazama maana hii tunaona mambo makuu 4
- Uwezo wa asili
Kipaji au vipawa mtu anazaliwa navyo si vitu vya kusomea. Watu wanaweza kujifunza maarifa au ujuzi fulani lakini wapo watu ambao kwa asili wana utaalam au ujuzi husika. Kipaji ni zawadi kutoka kwa Muumba wa wanadamu wote. Ni dhahiri hatupaswi tu kumwabudu Mungu katika imani zetu bali tuna sababu ya kumtafuta ili atujulishe vile vitu ambavyo ametupa kwa asili ili tuvitumie kunufaisha wengi zaidi. Watu wengi huzaliwa, huenda shule na kuishi maisha yao yote hawajawahi kujua kuhusu vipaji vyao wala hawajawahi kumuuliza Mungu kuhusu vipaji husika.
- Je, wewe ulishawahi kumuuliza Mungu juu ya kipaji au vipawa alivyokupa?
- Je, watu wanasemaje kuhusu uwezo wako mwengine ambao wanakuambia lakini hujawahi kuutumia?
- Ubora au kiwango cha utendaji kuwa bora
Kipaji hudhihirisha ubora au kiwango cha juu cha utendaji wa mtu husika. Ili uweze kujua mtu huyu ana kipaji angalia matokeo ya kazi yake au utendaji wake wa kazi, ni lazima utakuwa na ubora wa hali ya juu kulinganisha na watu wengine katika jambo hilo hilo.
- Je, ni kazi gani au mambo gani unayafanya kwa kiwango cha juu hata watu wengine wakakubali ubora huo?
- Matumizi ya rasilimali ndogo
Kipaji kinapowekwa kazini hakihitaji nguvu nyingi kukamilisha jambo bali nguvu chache au rasilimali kidogo kabisa. Tunawaona watu wenye vipaji vya kucheza mpira tunafurahia kazi yao na wanalipwa vizuri, lakini kimsingi wao hawaumii kwa kazi ile bali wanaifurahia kwa sababu ni sehemu ya kipaji chao. Hawahitaji nguvu kubwa katika kutekeleza wajibu wao wa kimchezo bali nidhamu tu ya mazoezi.
- Je, ni kitu gani ulishawahi kufanya kwa kutumia nguvu ndogo au maarifa kidogo na kuleta tofauti kubwa na watu wengine inavyotarajiwa
- Utofauti na watu wengine
Kipaji kina namna ya kukutofautisha na kundi zima la jamii. Watu wengi hufikiri sisi binadamu tunafanana kwa kila kitu wakati ukweli ni kwamba tupo tofauti. Ndio maana kila mmoja ana vinasaba vyake yaani ‘DNA’, pia tuna alama za mikono au miguu zinazotutofautisha na wengine. Namna nzuri ambayo tunaweza kuitumia kuonesha tofauti yetu na watu wengine ni kutumia vipaji tulivyopewa. Mfumo wa shule unafundisha wanafunzi kufanana kwa kila kitu na unatarajia wote wawe na uelewa sawa na ufaulu sawa. Mfumo wa vipaji unataka kila mmoja anoneshe uwezo wake kwa njia tofauti ili tuweze kuhudumiana. Utofauti ninaozungumzia hapa si wa kielimu au kiuchumi au hadhi bali ule wa asili uliozaliwa nao wewe binafsi.
- Je, kitu gani cha asili kinakutofautisha na jamii au ndugu au wafanyakazi wenzako
Haya ndio maeneo 4 ambayo unaweza kutumia kujipima kuhusu kipaji chako au mtoto wako au mtu yeyote unayetaka ajifunze katika kuwekeza katika uwezo wake wa kiasili. Kipaji ni kitu muhimu sana ambacho kila mtu anapaswa kuzingatia. Kipaji hutuweka wanadamu wote katika fursa sawa kama vile tunavyopewa pumzi ya uhai na saa 24 kwa kila siku ndivyo kila mmoja wetu anacho kipaji au vipaji. Kinachotofautisha watu kimaisha ni wale waliojifunza juu ya uwezo wao wa kiasili na kuwekeza nguvu zao huko zaidi. Jifunze kuhusiana na kipaji chako, omba Mungu akuoneshe vipaji vyako na uanze kuwekeza nguvu zako huko zaidi kwa manufaa yako na jamii kwa ujumla.
‘Kipaji changu, fursa yangu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!