
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu katika mafunzo juu ya Kipawa/Vipawa katika mtandao wa isaackzake. Ukurasa huu ni maalum kwa ajili yako kujifunza mambo yote kuhusu kipawa au vipawa vyako. Hapa utapata makala, mifano mbalimbali kuhusu kipawa au vipawa vyako na kutambua kipawa chako. Tutajifunza namna mbalimbali za kunoa au kuboresha kipawa chako kila siku na nidhamu unayohitaji ili kipawa kilete faida kwenye maisha yako. Kipawa ni moja ya rasilimali muhimu sana katika maisha ya mwanadamu ambayo akiitambua na kuitumia vizuri humtofautisha na watu wengine na huvuta watu kwake kila siku. Karibu sana tujifunze leo kuhusu kauli mbiu yetu inayosema ‘Kipaji changu, fursa yangu’
Kipaji changu, fursa yangu ni kauli mbiu ambayo tungependa tuende nayo wakati wote wa mafundisho ya kipawa. Kauli mbiu hii ina lengo la kutuchagiza kufuatilia zaidi juu ya kipaji au vipawa vilivyopo ndani yetu.
Watu wengi hawahusianishi vipawa au vipaji vyao na fursa za kimafanikio hasa uchumi wao binafsi, wakati kwa uhalisia upo uhusiano mkubwa sana kati ya kipaji cha mtu na uchumi wake endapo ataweza kuunganisha vitu hivi vizuri.
Tunaweza kuita kauli mbiu hii katika namna tofauti kama ‘Kipaji changu, Nafasi yangu’ au Kipawa changu, fursa yangu’ au ‘Zawadi yangu, ujira wangu’
Pia tunaweza kuitafsiri kauli mbiu hii kwa lugha ya kiingereza na kupata misemo hii ‘My Gift, my Opportunity’ or ‘My talent, my position’ or ‘My talent, my pay’
Je, ni kwa nini tunapaswa kuwa na kauli mbiu hii?
- Kipawa ni kati ya rasilimali ndani ya mtu zenye nguvu kubwa ya kumfikisha kwenye kilele cha mafanikio kama akikigundua mapema na kukinoa vizuri.
- Kipawa ni njia ya mkato au rahisi ya kufikia mafanikio ya kiwango cha juu kwa muda mfupi sana kama mtu akiwekeza mapema katika kipawa chake.
- Kipawa ndio kitu kinachoweza kukutofautisha na kundi zima au dunia nzima. Ili ulete athari chanya duniani na kufanikiwa ni muhimu kuwa tofauti na wengine. Kipaji ndio kinaweza kukutofautisha.
- Kipawa kina nguvu ya kukupatia nafasi yoyote unayoitaka katika jamii, ikiwa ni nafasi ya kitaaluma, kimaarifa au kiuchumi. Huu ni ukweli ambao tumeendelea kuushuhudia kila kukicha, wapo watu kwa sababu ya vipawa vyao katika sanaa wamefanikiwa kuingia na kupata nafasi katika uongozi au kiuchumi.
- Kipawa kikitumiwa vyema na maarifa hakina mipaka bali huzidi sana na kuleta matokeo bora ya kiwango cha juu.
Itafakari kauli mbiu hii na unaweza kuichukua yoyote kati ya hizi ambazo tumejadili leo iwe kwa lugha yoyote ile muhimu kauli mbiu ina lengo la kukuchagiza kuchukua hatua na hamasa kubwa katika kutafuta kujua juu ya kipawa chako ili upate Nafasi unayostahili katika dunia. Hizi ni nyakati ambazo unahitaji kuwekeza zaidi kwenye vipawa vyako kuliko hata taaluma, ni nyakati za kufuatilia vipaji vya watoto au wale walio katika nyumba yako ili viwafae katika mambadiliko makubwa sana yaliyotokea duniani.
‘Kipaji changu, fursa yangu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!