
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu katika mafunzo juu ya Kipawa/Vipawa katika ukurasa huu wa vipaji. Katika makala iliyopita tuliona msingi wa kipaji kinakupa nafasi. Leo tunaangalia msingi wa 4 ya kuwa Kipaji unakufa nacho. Karibu sana tujifunze.
Msingi wa 4. Kipaji unakufa nacho
Kama vile njia ya kupata kipaji ni matokeo ya kuzaliwa nacho kadhalika njia ya kupoteza au kuondokewa na kipaji ni kufa nacho. Si watu wengi wanafahamu juu ya hili, kipaji hakiondoki kwa mtu ingawa kinaweza kupungua ufanisi wake kutokana na sababu mbalimbali kama ugonjwa, au umri nk lakini bado ndani ya mtu kipaji husika kipo.
Nadhani tumewahi kuona watu wengi waliofanya vizuri sana kwa vipaji vyao katika maeneo mbalimbali kama mpira wa miguu au mchezo wa ngumi au riadha au muziki n.k lakini baada ya muda watu hao hawasikiki tena katika fani hizo kulingana na sababu kadhaa. Lakini kwa hakika si kwamba wanakuwa wamepoteza vipaji vyao lakini wanakuwa wamepoteza ufanisi kutokana na muda au umri wao kushabiiana na mahitaji ya wakati husika.
Ndio maana ni muhimu sana kwetu kufahamu juu ya kipaji mapema kwa watoto na vijana wetu ili waweze kutumia mapema na kwa muda mrefu. Watu wengi wanapoteza ufanisi wa vipaji vyao kwa sababu ya mfumo wa elimu unaochukua muda mrefu sana katika ngazi mbalimbali. Chukulia mfano kijana mwenye uwezo wa kucheza mpira wa miguu lakini kwa muda mrefu anakuwa shuleni na anahitimu shahada na miaka 25 hapa anakuwa amepoteza muda na inawezekana asipate nafasi ya kutumikia au kukitumia kipaji chake cha uchezaji kwa sababu mahitaji ya muda ni vijana wa kati ya miaka 18 – 20 ndio wenye uwezo mkubwa katika kucheza ziaidi yake mwenye miaka 25 -30.
Hivyo ufahamu wa kipaji chako mapema kitakusaidia kufanya mipango madhubuti ya namna ya kuweza kukitumia kulinganisha na muda utakaokuwa nao. Kama matumizi ya kipaji chako yanaweza kuendelea kuwa bora kwa kadri umri unavyoendelea basi unayo nafasi nzuri, lakini kama matumizi ya kipaji chako yamefungwa kutokana na muda maalum basi unapaswa kufikiria vizuri zaidi namna ya kuwekeza katika kipaji chako kabla ya mambo mengine.
Ni muhimu kuzingatia kipaji unakuja nacho ukizaliwa na unaondoka nacho ukifa lakini suala la ufanisi wa kipaji chako kulinganishwa na mahitaji ya wateja wako inategemea muda utakaoweza kukiingiza kipaji chako kazini.
‘Kipaji changu, fursa yangu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!