Kipaji.12. Msingi wa Kipaji Na.3. Kipaji kinakupa Nafasi

Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu katika mafunzo juu ya Kipawa/Vipawa katika ukurasa huu wa vipaji. Katika makala iliyopita tuliona msingi wa kipaji kuwa zawadi. Leo tunaangalia msingi wa 3 ya kuwa Kipaji kinakupa Nafasi. Karibu sana tujifunze.
Msingi wa 3. Kipaji kinakupa Nafasi
Katika zama hizi ambazo idadi ya watu imekuwa kubwa zaidi duniani na kumekuwa na ufinyu mkubwa wa nafasi za ajira njia pekee iliyobaki kwa ajili ya kila mmoja wetu kupata nafasi mbele ya jamii ni kupitia kipaji.
Watu wengi wanahangaika na masuala ya shule au taaluma, hili ni zuri lakini sote tunajua ya kuwa wapo wengi wamesoma zaidi yako na wapo wenye vyeti bora sana kuliko wewe binafsi katika kila fani inayotuzunguka. Kila siku shule, vyuo na taasisi nyingi za elimu zinazalisha idadi kubwa ya wahitimu wanaoingia kwenye soko la ajira.
Inakadiriwa takribani vijana milioni 2 wanaingia katika soko la ajira nchini Tanzania kila mwaka. Yaani hawa ni vijana wanaohitimu katika ngazi mbalimbali za elimu na wale ambao wanafikia umri wa kuzalisha au wanaopaswa kuanza kuzalisha au kujitegemea kiuchumi. Hatahivyo uwezo wa soko la ajira kuchukua vijana hawa ni mdogo sana. Si zaidi ya ajira 100,000 hutengenezwa kwa mwaka, hivyo tunabaki na kundi kubwa sana ambalo wapo mtaani hawana ‘nafasi’
Je, kundi hili lote huishi vipi, hutunzwa na nani? Na wanawezaje kupata nafasi katika zama hizi za ushindani kila kona? Suluhisho walilonalo ni kuibua nguvu ndani yao kupitia kipaji au vipaji. Watu wengi hawatilii maanani masuala ya vipaji mpaka pale hali ya kimaisha inapokuwa ngumu sana ndipo wanaanza kutafuta ana uwezo wa asili katika eneo gani. ndio maana kwa sasa unaweza kuona wimbi kubwa la vijana wakiingia katika sanaa ya muziki, au michezo, hii ni kutokana na kukwama katika kupata nafasi kwenye ushindani mkubwa. Hii haina maana wote ni wanamuziki, la hasha tunafahamu wapo wanaojaribu lakini huko si sehemu yao lakini wapo wanaofanikiwa kupata nafasi kupitia sanaa ya muziki.
Kitu tunachopaswa kukifahamu kama jamii ni kuwekeza mapema sana kwenye kizazi chetu kwa kufahamu uwezo wa asili walionao ili kuuendeleza na kuwajengea mazingira ya wao wenyewe ‘kutengeneza nafasi’ katika jamii na kupata kipato chao. Kama Serikali na sekta binafsi kwa ujumla wake haziwezi kutengeneza nafasi zaidi ya milioni 2 kwa mwaka, mbadala tulionao ni kuwajengea vijana mazingira ya kufahamu vipaji vyao ili wao wenyewe watengeneze nafasi za ajira zao na kutoa thamani kubwa kwenye jamii yetu.
Kwa njia ya kipaji kila mmoja wetu ana uwezo wa kutengeneza nafasi ya kazi yake na hivyo kujipatia ajira na kusaidia kujenga uchumi wa taifa letu.
‘Kipaji changu, fursa yangu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.

Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!