Kipaji.11. Msingi wa Kipaji Na.2. Kipaji ni zawadi

Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu katika mafunzo juu ya Kipawa/Vipawa katika ukurasa huu wa vipaji. Katika makala iliyopita tuliona msingi wa kipaji kuwa kila mtu anacho kipaji. Leo tunaangalia msingi wa 2 ya kuwa kipaji ni zawadi. Karibu sana tujifunze.
Msingi wa 2. Kipaji ni zawadi
Umewahi kufikiri au kujiuliza juu ya utamaduni ambao upo karibu duniani kote wakati mtoto anazaliwa huwa analetewa zawadi? Naamini wewe umewahi kushiriki kutoa zawadi au kupokea zawadi kwa niaba ya mtoto wako. Umewahi kujiuliza kwa nini huwa unatoa zawadi unapoenda kumtazama mtoto au watu wanapokuja kumtazama mtoto katika familia yako? Huu ni utamaduni wa siku nyingi sana hata tunauona katika vitabu vya maandiko matakatifu wakati Yesu anazaliwa walikuja mamajusi na zawadi kumwona mtoto Yesu.
Kitua ambacho kinaashiriwa juu ya utamaduni huu ni kuwa mtoto anayezaliwa kuna kitu amebeba cha thamani kwa ajili ya dunia na ndio maana kama wawakilishi wa dunia tunaenda kupeleka zawadi zetu ikiwa ni fedha, nguo, chakula, na mahitaji mengine. Kile ambacho mtoto anachokuja nacho ni zawadi kwa ajili ya dunia yaani amebeba vipawa kwa ajili yetu vitakavyotufaa katika maisha yetu.

Kila mtu anacho kipawa na anakipata bure kabisa kama zawadi kutoka kwa Muumba wa Mbingu na Nchi. Kipawa huwezi kusomea au kujifunza darasani ila kipawa unapaswa kukigundua kilichopo ndani yako na kuanza kukifanyia kazi katika maisha yako.
Je, wewe ulipokuwa mdogo uliletewa zawadi au wazazi wako walikueleza juu ya zawadi ulizoletewa na majirani, ndugu, jamaa na marafiki wa familia yako? Je, ulipopata mtoto wako walileta zawadi kwa ajili yake?
Je, mpaka sasa wewe umetoa zawadi au thamani kwa jamii kiasi gani kutokana na kipawa chako? Hapa sizungumzii suala la elimu yako na kazi unazofanya za kutumikia watu kutokana na taaluma yako. Kipo kitu ambacho unacho zaidi ya elimu au ujuzi uliojifunza kinapaswa kwenda kwa watu wengine ni kwa kiasi gani umekitoa ndani yako?
Je, umefahamu juu ya kipawa cha mtoto wako au wale unaowalea ulipowawakilisha kupokea zawadi walizoletewa na marafiki zako?
Kile kitu ambacho sisi hatufahamu ni kuwa kipawa ni kikubwa sana kuliko elimu au ujuzi wa kujifunza kwani tunaona ishara ya kukubaliwa na jamii kupitia kipawa na si taaluma zetu. Wakati tukiwa dhaifu bado, watoto wadogo, wageni katika dunia hii bado watu walikuja kutufuata nyumbani kwa wazazi wetu na kuleta zawadi zao kwa ajili ya ujio wetu. Hii inatuonesha ya kuwa ndani yetu kuna kitu tumebeba cha thamani sana kuliko elimu au ufahamu au ujuzi wa shuleni ambacho jamii imekuwa tayari kutoa vitu vya thamani ili na sisi tuweze kutengeneza thamani hiyo kwao. Hivi ni vipawa ambavyo Mungu ametupatia bure kabisa. Tunahitaji kuvitumia kila siku kuleta mabadiliko kwa jamii yetu.
‘Kipaji changu, fursa yangu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.

Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!