
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu katika mafunzo juu ya Kipawa/Vipawa katika ukurasa huu wa vipaji. Katika makala iliyopita tuliona changamoto ya Kiburi. Leo tunaanza kuangalia misingi ya vipaji kwa ajili ya kila mmoja wetu. Karibu sana tujifunze.
Msingi wa 1. Kila mmoja wetu anacho kipaji
Fikiria idadi kubwa ya watu wote duniani sasa ni takribani Bilioni 7.8 na kwamba kila mmoja wetu anacho kipaji chake alichopewa na Mungu. Kipaji hakijali dini, hadhi, kabila, wala rangi au kujulikana kwa mtu au kutokujulikana.
Kila mtu anacho kipaji chake binafsi ambacho kinakuwepo cha asili ndani yake. Ile tu kuzaliwa kwako na kuwa mwanadamu kunakufanya uwe na kipaji au vipaji kadhaa kwa ajili ya kukuwezesha kuishi maisha yako.
Wako watu tunaona wanazaliwa na changamoto mbalimbali katika miili yao wengine hawana mikono au miguu, wengine wana ulemavu wa macho n.k lakini katika makuzi yao tunaweza kuona uwezo wao wa ajabu na ziada kuliko wale ambao wamekamilika kwa viungo vyote.
Tuna historia ya watu walifanya vizuri sana katika maeneo mbalimbali kama sayansi, muziki na michezo lakini wana upungufu wa viungo kama uwezo wa kutembea, kuona, au matumizi ya mikono yao.
Wewe na mimi tunavyo vitu ambavyo havipo kwa wengine. Pata picha dunia nzima wewe au mimi tunacho kitu ambacho hakipatikani kwa mwengine yeyote, je ni kwa kiasi gani tunaweza kutumia kitu hicho kuzalisha thamani kuu siku ya leo.
Wengi tunadharau kipawa tulichonacho, hatuijui thamani yake kwa dunia, muhimu sana siku ya leo kukinoa kipaji chetu na kuathiri ulimwengu wetu kwa njia chanya na kuleta mabadiliko yanayostahili. Ninacho kitu cha kuipa dunia siku ya leo, ili dunia nayo inijaze na vitu kwa kipimo kikubwa sana.Weka kipaji chako kazini siku ya leo ili dunia inufaike nawe utanufaika na kupata nafasi yako duniani. Hakikisha kipawa chako kwanza kinaleta faida kwake yeye Mungu aliyekupatia.
Kile unachopata leo kutoka kwa dunia ni matokeo ya mtu kufanyia kazi kipawa chake kukufaidisha wewe, nawe una wajibu wa kufanyia kazi leo. Mfano, nyumba unayokaa, kitanda, mswaki, feni, maji, umeme, computer, gari, vitabu etc hizo ni kazi za vipawa vya watu, wewe unaipa nini dunia leo.
‘Kipaji changu, fursa yangu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!