
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu katika mafunzo juu ya Kipawa/Vipawa katika mtandao wa isaackzake. Ukurasa huu ni maalum kwa ajili yako kujifunza mambo yote kuhusu kipawa au vipawa vyako. Hapa utapata makala, mifano mbalimbali kuhusu kipawa au vipawa vyako na kutambua kipawa chako. Tutajifunza namna mbalimbali za kunoa au kuboresha kipawa chako kila siku na nidhamu unayohitaji ili kipawa kilete faida kwenye maisha yako. Kipawa ni moja ya rasilimali muhimu sana katika maisha ya mwanadamu ambayo akiitambua na kuitumia vizuri humtofautisha na watu wengine na huvuta watu kwake kila siku. Karibu sana tujifunze kwa pamoja kuhusu kipaji.
Leo tunaenda kujifunza Maana ya Kipaji au Kipawa.
Nadhani kila mmoja wetu amesikia au amewahi kuzungumzia juu ya kipawa au vipawa au kipaji katika mazingira mbalimbali. Tunaweza kuona mtu anacheza mpira wa miguu au anaimba au anapiga ala za muziki na tunajua ya kuwa ana kipaji au kipawa katika eneo hilo. Tunaona kwa watoto wadogo jinsi wanavyofanya mambo tofauti tofauti na watoto wa rika lao, wengine wana uwezo mkubwa katika maeneo ya masomo au ufundi au ubunifu n.k jamii tunasema huyu ana kipawa.
Je, kipawa ni nini? Au kipaji ni nini?
Kipaji ni uwezo wa asili wa kutenda mambo makubwa na yenye matokeo bora kwa kutumia nguvu na rasilimali ndogo ukilinganisha na watu wengine.(Tafsiri kwa mujibu wa kitabu cha KIPAJI na Emilian Busara na Mrembo Grace, 2015).
Mtandao wa Wikipedia pia unaelezea maana ya kipaji kuwa ni sehemu ya uwezo wa kufanya jambo fulani kwa ngazi ya juu. Kipaji huweza kuwa cha kimwili au kiakili.
Hii ina maana ya kuwa kipaji hakitokani na masomo au uzoefu au eneo ambalo mtu anazaliwa, ni uwezo wa asili ambao mtu anazaliwa nao. Suala la kipaji halihusianishwi na nasaba au wadhifa wa mtu, cheo, rangi, kabila, jinsia au namna yoyote ile bali ni suala la kuzaliwa nalo.
Mambo ya msingi kufahamu kuhusu kipaji
- Ni uwezo wa mtu binafsi – uwezo huu humsaidia kufanya mambo tofauti na kawaida.
- Ni kitu cha asili – yaani mtu huzaliwa na kipaji, hakiwezi kurithishwa, kila mtu ana kipaji cha aina yake. Ni zawadi kutoka kwa Mungu mwenyewe.
- Mtu anaweza akawa na kipaji asijue – wapo watu wengi wanaishi bila ufahamu wa vipaji vyao au wapo wanao ufahamu lakini hawavitumii.
- Kila mtu ana kipaji – hii ni kweli kabisa bila kujali hali zetu au asili yetu kila mtu anacho kipaji. Suala la kipaji kwa kila mtu ni jambo la hakika aidha uwe unajua au hujui lakini unacho kipaji.
- Kipaji ni ufunguo wa maisha ya mafanikio – pamoja ya kwamba kila mtu ana kipaji lakini si wengi wanahusianisha vipaji vyao na mafanikio yao kimaisha. Waliofanikiwa zaidi katika maeneo mbalimbali kwa sehemu kubwa wamefanikishwa na vipaji vyao. Ndio maana tunaona wanamichezo mbalimbali katika mpira wa miguu, kikapu, masumbwi, riadha n.k wamefanikiwa zaidi kwa sababu ya vipaji vyao na si elimu au asili zao.
Maswali ya msingi ya kujiuliza mimi na wewe
- Je, tunafahamu kipaji chetu au vipawa tulivyojaliwa na Mungu?
- Je, ikiwa tunafahamu, kwa kiasi gani tunavitumia katika maisha ya kila siku?
- Je, vipawa vyetu vina mchango kiasi gani katika uchumi wetu binafsi?
- Je, watu wengine au jamii wanatutambua kwa taaluma, ujuzi au vipaji vyetu?
Haya ni maswali muhimu sana ndugu yangu katika kutafuta kujua zaidi juu ya hazina ambayo ipo ndani yetu. Watu wengi tunahangaika huku na kule kutafuta kitu au vitu vya kutusaidia kuboresha maisha yetu, wakati kwa hakika tuna hazina ndani yetu ambayo hatujaigusa. Karibu kushiriki maswali haya na unaweza kujijibu mwenyewe au tukawasiliana kupitia website hii eneo la maswali na majibu au ukaweka maoni yako kuhusu makala hii ya kwanza katika makala za mfululizo kuhusu kipaji au vipawa.
‘Kipaji changu, fursa yangu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Vipi kama Kuna ugumu wakukitumia kipaji chako Hali yakua umekwisha kujua kua kipaji unacho,nininkifanyike?