
Utangulizi
Karibu tena ndugu msomaji katika mfululizo wa makala hizi za kujifunza juu ya maana ya kazi kwa lengo la kuboresha maisha yetu kila siku na kusaidia watu wengi ambao wanapaswa kufanya kazi ili kuingia kazini.
Katika makala ilizotangulia tumeangalia juu ya changamoto za ajira ambayo ni ‘nafasi ya ajira’ hii ina maana ili ajira iweze kupatikana ni lazima nafasi itengenezwe katika mfumo wa ajira, wakati kwa upande wa kazi, mtu anatengeneza mwenyewe nafasi ya kazi. Leo tunaangalia changamoto nyingine katika mfumo wa ajira ambayo inahusisha kushindanisha watu. Karibu tujifunze.
Ufinyu wa nafasi za ajira unapelekea ushindani usio na tija katika nafasi chache za ajira zinazojitokeza maeneo mbalimbali. Tumeshuhudia mara kwa mara unakuta kampuni au shirika la umma lina nafasi za kazi chache mathalani nafasi 10 lakini utaona maelfu ya waombaji wa nafasi hizo wakituma maombi yao au wakiitwa kwenye usaili mara kwa mara.
Hali hii ya ukosefu wa ajira inapelekea hata waajiri kushindwa kupata waajiriwa ambao wana vigezo vizuri zaidi kwa sababu ya zoezi la uchambuzi kuwa gumu sana kutokana na wingi wa watu.
Pia mazingira haya ya wingi wa waombaji katika nafasi chache, hupelekea kutengenezwa mfumo wa rushwa au upendeleo katika nafasi za kuajiriwa. Ndio maana katika ajira haijalishi unajua nini bali hasa unamjua nani katika kukusaidia kufanikisha azma yako kwenye kupata ajira.
Kwa upande mwengine, ikiwa watu au wahitimu wanatambua uwezo wao au wameendeleza uwezo wao wa kutenda kazi, hakuna sababu ya kushindana na wahitimu wengine bali kila mmoja anaingia kazini kwake kwa kuishindania ndoto yake kubwa iliyo ndani yake. Kama tulivyoandika katika makala zilizopita ya kuwa kazi ni zao la uwezo binafsi ambao kila mmoja wetu anao na endapo atawekeza ndani yake hatokuwa na sababu ya kuzunguka na vyeti kutafuta ajira bali atatumia uwezo wake kuzalisha na kubadilisha maisha ya watu wanaomzunguka.
Kuingia katika mfumo wa ajira ni hatari kwani ushindani uliopo unaweza usitoe nafasi ya kutosha kwako kupata ajira husika lakini mtu akibadili fikra zake na kujenga tafsiri ya kazi haitaji ajira ili kufanya mabadiliko katika jamii yake anaweza kuanza kazi yake mara moja bila kusubiri na hatimaye kazi hiyo inaweza kumuingizia kipato baada ya kutoa thamani kuu kwa jamii.
Asiyetaka kufanya kazi na asile…’
Isaack Zake
Wakili, Mwandishi na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!