
Utangulizi
Karibu tena ndugu msomaji katika mfululizo wa makala hizi za kujifunza juu ya maana ya kazi kwa lengo la kuboresha maisha yetu kila siku na kusaidia watu wengi ambao wanapaswa kufanya kazi ili kuingia kazini.
Katika makala ilizotangulia tumeangalia juu ya changamoto za ajira ambayo ni hali ya uchumi. Hapa tumeona juu ya hali ya uchumi ikiwa mbaya au imeshuka basi watu wengi hupoteza ajira na hata wengine kutopata fursa ya kuajiriwa. Leo tunaangalia changamoto nyingine katika ajira ambayo ni ‘nafasi ya ajira’.
Ajira ni zao la nafasi wakati kazi ni zao la uwezo. Ili mtu apate ajira ni lazima ‘nafasi’itengenezwe katika kampuni au sehemu ya kazi. Bila uwepo wa nafasi ajira haiwezekani. Mazingira ya sasa ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia ajira nyingi zimekuwa mashakani kutokana na ufinyu wa nafasi na makampuni yanavyotafuta mbinu mbalimbali za kupunguza matumizi. watu wengi waliokuwa wakiajiriwa kufanya kazi za mikoni siku hizi kazi hizo zinakamilishwa na mashine mbalimbali. Waajiri na makampuni makubwa kila siku wanawekeza zaidi katika kutengeneza mifumo isiyotegemea watu bali vitu ili kuzalisha faida kubwa. Hakuna kampuni lenye maslahi kwa ajili ya kutengeneza ajira kwa watu bali wanachotaka ni matumizi ya fedha kidogo na kupata faida kubwa. Hali hii inapunguza sana nafasi za ajira ambazo watu wengi wamekuwa wakizitigemea katika maisha yao.
Wimbi kubwa la watu wanahitimu kila mwaka katika vyuo na ngazi za elimu mbalimbali huku wakibeba matumaini ya kupata ajira, huku wimbi kubwa la makampuni au waajiri kila mwaka wanatafuta namna ya kupunguza nafasi za ajira kwa kutumia zana za kisayansi kiteknolojia.
Je, wewe unatarajia kupata nafasi ya ajira? Umejipanga kwa namna gani kuhakikisha unaipata hiyo nafasi? Ushauri wangu kwako ni kuhakikisha unajipanga kufanya ‘kazi’ ili kutengeneza ‘nafasi yako’ binafsi kulingana na uwezo ulio ndani yako.
Asiyetaka kufanya kazi na asile…’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!