Kazi 13. Kazi ipo ‘ndani yako’ wakati ajira ni ya ‘ipo nje yako’

Utangulizi
Karibu tena ndugu msomaji katika mfululizo wa makala hizi za kujifunza juu ya maana ya kazi kwa lengo la kuboresha maisha yetu kila siku na kusaidia watu wengi ambao wanapaswa kufanya kazi ili kuingia kazini.
Katika mfululizo wa makala za tofauti ya kazi na ajira tumeanza kwa kuangalia maana ya neno kazi katika makala iliyotangulia. Katika makala iliyopita tumeona tofauti ya kazi kuwa ya ‘asili’ na ajira ya ‘muda’. Karibu sana.
Kazi ipo ndani yako
Kwa kutazama maana ya kazi ambazo tumejifunza katika makala zilizotangulia tunaweza kuona ya kuwa suala la kazi lipo ndani ya mtu binafsi na si kitu cha kutafuta au kukipata kutoka nje au kwa kujifunza.
Maana ya neno kazi inaweza kuhusiasha uwezo wa kuumba au kubuni au kuzalisha au kuwezesha upatikanaji wa kitu au huduma inayopelekea tija, ufanisi na manufaa kwa jamii.
Kwa maana hii tunaona ya kuwa suala la kazi ni ‘uwezo’ ulio ndani ya mtu katika kutekeleza mojawapo wa mambo haya tuliyoainisha. Kila mmoja wetu anao uwezo wa kufanya chochote kati ya haya ikiwa ni kuumba au kubuni kitu au kuzalisha au kufanya biashara au kutoa huduma.
Mambo haya yote yanaweza kufanywa na mtu yeyote pasipo kujali kiwango cha ufahamu au elimu aliyonayo mtu husika. Ndio maana unaweza kuona walio wengi ambao hawana elimu kubwa ndio wanamiliki makampuni makubwa na kuajiri wale wanaoonekana wamesoma sana. Hii ni kwa sababu wapo waliojitambua ya kuwa ndani yao wamebeba kazi huku wengine wakiwa wanasaka ajira.
Ajira ipo nje yako
Tofauti na ilivyo kazi ambayo ipo ndani ya uwezo wa mtu binafsi, ajira ipo nje ya mtu husika. Hii ina maana ya kuwa mtu hana uwezo wa kuamua juu ya ajira yake itakuwa ipo kwa muda gani, hili ni jambo ambalo huamuliwa na mtu mwengine. Ajira hutengenezwa kutokana na utashi wake yule anayeajiri na si utashi wa anayetaka kuajiriwa. Hii inamfanya anayetaka kuajiriwa kutokuwa na nguvu kubwa ya kuamua maslahi yake katika ajira kama vile angeamua katika utendaji wa kazi zake.
Familia nyingi na watu wengi hujibidiisha katika kusoma au kufikia ngazi za juu za elimu wakilenga sana kupata ajira ambayo hawana udhibiti nayo kwani ni suala la nje ya uwezo wao. Unaweza kujifunza aina ya masomo fulani ukadhani kuwa utapata ajira hiyo lakini baada ya muda unaweza kukuta ajira husika haipo. Hii haimaanishi ya kuwa suala la elimu halina maana au ni baya, ila inapaswa kuwa makini pale mtu unapochagua kujifunza juu ya fani fulani usilenge kupata ajira bali itumie fani husika kunoa au kudhihirisha kazi uliyonayo ndani yako
Asiyetaka kufanya kazi na asile…’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!