
Utangulizi
Karibu tena ndugu msomaji katika mfululizo wa makala hizi za kujifunza juu ya maana ya kazi kwa lengo la kuboresha maisha yetu kila siku na kusaidia watu wengi ambao wanapaswa kufanya kazi ili kuingia kazini.
Katika mfululizo wa makala za tofauti ya kazi na ajira tumeanza kwa kuangalia maana ya neno kazi katika makala iliyotangulia. Katika makala iliyopita tumeona tofauti ya kusudi la kazi na kusudi la ajira. Tunaendelea sasa kuzichambua tofauti kadhaa za maneno haya. Leo tunaangalia tofauti ya kazi kuwa ya ‘asili’ na ajira ya ‘muda’. Karibu sana.
Kazi ni ya asili
Unaweza kukosa ajira lakini huwezi kukosa kazi. Hii ni kweli kwa sababu kazi ni kitu cha asili kwa kila mmoja wetu. Kama vile tulivyopewa kinywa kwa ajili ya kula chakula halikadhalika tumepewa kazi ya kutuwezesha kupata mahitaji yetu ya kila siku binafsi bila kujali kiwango cha elimu au hadhi au utaifa au jinsia kila mmoja wetu anayo kazi ndani yake.
Kama tulivyoona katika tafsiri ya neno kazi katika makala zilizotangulia, ya kuwa kazi inausisha akili au nguvu au vyote kwa pamoja katika kufikia malengo maalum. Kazi inawezekana kwa awali isilete fedha lakini inaweza kukutengenezea kupata fedha hapo baadae kama utaifanya kwa bidii na ufanisi mkubwa.
Wanadamu wote tunayo asili ya kufanya kazi lakini wapo watu wanaoendekeza uvivu kwa kisingizio cha kukosa kazi. Unapaswa kusema umekosa ajira na sio kazi, badilisha mtazamo wako kwani kazi ni ya asili na ipo ndani yako tumia akili na nguvu zako kudhihirisha kilichopo ndani yako.
Ajira ni ya muda
Huu ni ukweli kabisa kwa mtu yeyote anayefanya shughuli kwa minajili ya kulipwa hulipwa kwa muda tu. Ndio maana vipimo vyote vya kiajira hupimwa ndani ya muda. Unaweza kuajiriwa kulipwa kwa saa au siku, au wiki au mwezi. Ajira inapimwa ndani ya muda. Hali hii inafanya wale walio na ajira kukosa uhuru wa maisha yao kwa sababu wanauza muda kwa fedha. Muda ndio rasilimali muhimu sana baada ya pumzi kwa mwanadamu.
Kama unatumia muda wako kwa ajili ya kuuza ili kupata kiasi cha fedha basi kuna sehemu kubwa ya maisha yako uliyopaswa kuishi na tofauti uliyopaswa kuileta hutopata muda wa kuifanya kikamilifu. Wengi walio katika ajira hudhani muda utawasubiri lakini kadri muda unavyokwenda ndivyo wanazidi kuzama katika dimbwi la ajira na inakuwa ngumu zaidi kutoka. Muda wanaokuja kuzinduka miaka 30 au 40 imepita na wanatakiwa kupumzika kwa sababu mahitaji ya mwajiri kwa sasa hayawezi kuendana na muhusika. Hapa ndipo wengi huanza kufikiri kama kuna ‘kazi’ wanaweza kufanya na maisha yao yaliyobaki.
Ajira ni ya muda jifunze kutumia asili yako katika kufanya kazi kuliko kujifunga ndani ya ajira kwa muda na kupoteza fursa kubwa iliyo ndani ya kazi.
Asiyetaka kufanya kazi na asile…’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Asante sana Wakili Zake, kweli ajira ni kupoteza muda wako, kama tutauzingatia ufahamu huu na kuamua kuweka kazi lazima tupate matokeo bora sana, barikiwa sana mwalimu.
Asante sana pia karibu na shirikisha maarifa haya kwa wengine wengi.