
Utangulizi
Karibu tena ndugu msomaji katika mfululizo wa makala hizi za kujifunza juu ya maana ya kazi kwa lengo la kuboresha maisha yetu kila siku na kusaidia watu wengi ambao wanapaswa kufanya kazi ili kuingia kazini.
Katika mfululizo wa makala za tofauti ya kazi na ajira tumeanza kwa kuangalia maana ya neno kazi katika makala iliyotangulia. Katika makala zilizopita tumeona kwa kirefu utofauti wa maana kati ya maneno ‘kazi’ na ‘ajira’. Tunaendelea sasa kuzichambua tofauti kadhaa za maneno haya. Leo tunaangalia tofauti kubwa iliyopo kwenye malengo ya ‘kazi’ kulinganisha na malengo ya ‘ajira’. Karibu sana.
Lengo la kazi
Kama tulivyoonesha katika makala zilizopita lengo kubwa la kazi ni kuleta thamani kwanza kwenye jamii. Mtu anayefanya kazi ndani yake hatazami fedha kwanza bali anatazama kuboresha maisha ya jamii yake na kuongeza ufanisi kwa watu wengine. Hili ndilo lengo kuu la kazi mahali popote.
Ndio maana unaweza kushangaa watu wengi ambao ni matajiri wana fedha na mali nyingi bado wanafanya kazi. Fikra zao hazipo kwenye kupata fedha zaidi bali katika kuongeza ufanisi, tija na manufaa kwa jamii kubwa zaidi.
Wengi wetu tunafikiri kwa namna ya kuajiriwa ndio maana tunatafuta zaidi fedha na tunafikiria ya kuwa tukiwa na fedha kiasi kama cha Bill Gates au kiasi cha fedha cha kutuwezesha kuishi maisha tunayotaka basi hatuna haja ya kufanya kazi. Haya ni mawazo ya mwajiriwa siku zote na sio mfanyakazi. Mfanyakazi haweki malengo kwenye fedha ila ufanisi na tija anayoongeza katika jamii inayomzunguka. Kila wakati anaweza kutumia rasilimali zake kuhakikisha maisha ya watu wengine yanakuwa bora zaidi.
Lengo la Ajira
Tafsiri ya neno ajira ni shughuli inayofanyika mara kwa mara kwa ajili ya kupata fedha.
Ni dhahiri lengo kuu au kusudio ambalo linamsukuma mtu kuwa katika ajira ni kupata fedha au ujira. Hakuna zaidi ya hapo. Watu wengi wapo katika kundi hili na ndio kundi kubwa sana katika jamii zetu. Watu wanaokuwa kwenye ajira siku zote hujikuta wanakimbiza fedha lakini bado fedha haitoshi. Kwa kadri wanavyoweka malengo ya kupata fedha zaidi kwenye ajira zao ndivyo fedha inavyozidi kuwa ndogo kutokana na matumizi yao. Huu mzunguko huchukua muda mrefu sana kiasi kwamba ni vigumu mno watu kutoka kwenye kundi la kuwa waajiriwa kwenda kufanya kazi. Wengi wao wanaanza kufikiria kufanya kazi baada ya kutokuhitajika tena kwenye ajira kwa njia ya ‘kustaafu’ ndipo wanaanza kufikiria kitu cha kufanya.
Upo utetezi ambao wanakuwa wao waajiriwa ya kuwa kama wote tukiwa waajiri au wafanyakazi ni nani ataajiriwa?
Vyovyote vile unavyotaka kufikiri kuhusiana na maisha unayotayaka ni kwamba hakuna mtu tajiri aliye mwajiriwa hata kama unalipwa mshahara mkubwa ina maana yule unayemfanyia kazi anapata mara nyingi zaidi yako ndio maana anamudu kukulipa anavyokulipa.
Je, ni nini malengo yako katika kutumika ni kuleta thamani katika jamii kupitia kazi au kupata fedha kupitia ajira?
Asiyetaka kufanya kazi na asile…’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!