Day.8. Spiritual Food: Gharama ya chakula cha kiroho

Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji wa mtandao huu wa isaack zake. Katika kipengele cha maarifa ya kiroho ya Uliza Neno tunakwenda kujifunza mambo mbalimbali yanayoanishwa na neno la Mungu kwa lengo la kutusaidia utu wetu katika safari na majukumu tuliyonayo hapa duniani siku kwa siku. Katika somo lililopita tuliendelea kujifunza habari za kusudi la chakula. Makala iliyopita tulijifunza habari za kipaombele cha kulisha utu wa ndani. Leo tunaangalia juu ya Gharama ya Chakula cha kiroho. Karibu sana.
‘Haya, kila aonaye kiu, njoni majini, Naye asiye na fedha; njoni, nunueni mle; Naam, njoni, nunueni divai na maziwa, bila fedha na bila thamani’ Isa.55:1
Ujumbe huu ulionenwa na Nabii Isaya ni ujumbe muhimu wa kuwaalika watu kwa ajili ya kupata chakula cha kiroho bure. Kuna mambo ya kujifunza juu ya ujumbe huu.
Mambo ya kujifunza
- Sisi zote tunajua ya kwamba chakula chochote ni gharama wala hakuna chakula cha bure. Hata kama leo umekula chakula cha bure nyumbani lakini yupo mtu aliyeingia gharama kukileta chakula hicho.
- Moja ya hitaji la msingi kabisa katika maisha ya mwanadamu ni kupata mlo wa kila siku. Mtu atakuwa tayari kukosa malazi au mavazi lakini si chakula. Kila mmoja wetu anahitaji chakula.
- Kwa kuwa na chakula ni gharama, je vipi kuhusu upatikanaji wa chakula cha kiroho.Hatununui chakula cha kiroho kwa fedha wala kwa kitu chochote cha thamani bali tunahitaji kuwa na KIU na NJAA ya chakula cha kiroho. Kama ilivyo kwa chakula cha kimwili ili kukipata tunahitaji fedha, lakini kwa chakula cha kiroho tunahitaji kiu na njaa.
- Msingi wa kupata chakula cha kiroho ni hali ya uhitaji wako wa ndani yaani Kiu na Njaa ya kiroho. Hatupati leo chakula kwa sababu hatujatengeneza kiu na njaa ya kutosha ndani yetu. Hali ya kukosa kiu na njaa ya chakula cha kiroho inatupelekea kutokuwa na msukumo wa kukitafuta chakula hicho.
- Bwana Yesu alipoanza kuhubiri alianza na ‘heri walio masikini wa roho..’ yaani wamebarikiwa wenye uhitaji wa mambo ya rohoni maana ufalme wa Mungu ni wao. Ukijua umuhimu/kusudi la chakula kwenye maisha yako kwamba ni kutunza uhai na kukuwezesha kufanya kazi ni wazi utaweka kipaombele kwa kutafuta neno au chakula kwa ajili ya nafsi na roho yako kila siku.
- Jenga kiu na njaa ya chakula cha kiroho kila siku ndio gharama ya kukipata kila siku. Tuanze sasa maadam ipo leo kwa kumwendea Bwana Yesu kwa moyo wa kiu na njaa ya chakula cha kiroho ili atushibishe kila siku.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!