
(Mwili – utu wa nje) (Nafsi + Roho – utu wa ndani)
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji wa mtandao huu wa isaack zake. Katika kipengele cha maarifa ya kiroho ya Uliza Neno tunakwenda kujifunza mambo mbalimbali yanayoanishwa na neno la Mungu kwa lengo la kutusaidia utu wetu katika safari na majukumu tuliyonayo hapa duniani siku kwa siku. Katika somo lililopita tuliendelea kujifunza habari za kusudi la chakula. Tumeona makusudi 2 makubwa ya chakula ni kuhifadhi maisha na kutuwezesha kufanya kazi.Leo tunajifunza habari za kipaombele cha kulisha utu wa ndani.
‘Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku’ 2.Kor.4:16
Mtume Paulo anatueleza juu ya mchakato na kipaombele cha maisha yetu ya kila siku katika mpangilio wa ulaji wetu. Anaeleza juu ya matokeo ya chakula cha mwili na kile cha kiroho, ya kwamba utu wa nje unachakaa lakini ule wa ndani unafanywa upya kila siku.
Mambo ya kujifunza
- Tunaona juu ya maandiko kuweka wazi suala la uwepo wa utu wa ndani na utu wa nje. Yaani tuna sehemu ya utu wetu inayoonekana yaani mwili na ile isiyoonekana yaani nafsi na roho.
- Utu wa nje una mahitaji yake kadhalika utu wa ndani una mahitaji yake ili uweze kuishi na kufanya kazi ipasavyo.
- Utu wa nje pamoja na kupatiwa mahitaji yake ikiwepo chakula lakini mwisho wake ni kuchakaa/kuisha. Hii ina maana haijalishi ni kwa kiwango gani tunahudumia mwili bado mwisho wake ni kuisha na kifo. Kwa kadri tunavyoamka kila siku asubuhi ndivyo utu wetu wa nje unavyochakaa na kupiga hatua nyingine kuelekea kaburini.
- Bajeti zote tunazofanya kila siku kwa lengo la kuhudumia mwili ikiwa ni chakula, mavazi, malazi na kila kitu, bado mwisho wake ni kuchakaa na kifo. Huu ni ukweli mtupu.
- Hatahivyo kuna habari njema juu ya utu wetu wa ndani ambao unafanywa upya kila siku. Utu wetu wa ndani unafanywa upya kwa kupata chakula sahihi cha kiroho kinachotolewa kila siku na Yesu Kristo mwenyewe.
- Sisi ndio wenye kuamua juu ya hatma za utu wetu, endapo tutaweka kipaombele katika mwili unaochakaa na unaoelekea kaburini au tutaweka nguvu zetu katika kuhakikisha tunalisha nafsi na roho zetu zenye nafasi ya kuishi milele. Uchaguzi huu ni binafsi unaopaswa kufanywa kila siku.
- Ukosefu wa chakula cha kiroho katika maisha ya mwanadamu hupelekea kifo cha kiroho na kutoweza kufanya kazi za Mungu. Ila uwepo wa chakula au ukosefu wa chakula cha kimwili bado matokeo yake ni kifo baada ya muda.
- Uchaguzi wa busara katika maisha yetu ni kuweka kipaombele cha kupata chakula cha kuhuisha utu wetu wa ndani kila siku, ili hata pasipo mwili tuendelee kuishi katika uzima ndani ya Kristo mwenyewe.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Ahsante wakili Izack kumbe na ktk neno la mungu upo pia ubarikiwe kaka kwa mafunzo haya
Asante sana nashukuru Mungu kwa karama zake alizotupatia ili kuzitumia kwa wakati huu.