Day.55. Spiritual Food: Je, ulipo kuna maneno ya uzima wa milele?

Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji ni siku nyingine tena tumepewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kujifunza zaidi misingi ya chakula cha kiroho ili kutuwezesha kufanya mapenzi yake na kumtumikia kwa furaha na upendo siku ya leo.
‘Basi Simon Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele’ Yn.6:68
Mambo ya kujifunza
- Kama tulivyoona kwenye makala iliyopita jinsi Bwana Yesu alivyouliza swali kwa wanafunzi wake iwapo nao wanataka kuondoka wasimfuate, ndipo tunapata jibu hili kutoka kwa Simon Petro mmoja wa wanafunzi wake.
- Katika muktadha wa maandiko haya mistari michache ya nyuma tunaona kundi kubwa la wanafunzi baada ya kusikia maneno ya Bwana Yesu kusema Yeye ndiye chakula cha uzima na damu yake ndio kinywaji cha uzima, waliacha kuambatana naye wakarejea nyuma. Lakini wale thenashara (wanafunzi 12) waliowakilishwa na Simon Petro walisema wazi kuwa hawana pa kwenda isipokuwa kwa Yesu tu.
- Katika safari ya kuambatana na Yesu huwa tunapitia vitu vingi sana na mambo mengi huwa magumu na haijawahi kuwa rahisi kwa sababu dunia au ulimwengu huwapinga wale ambao wanajinasibisha na Bwana Yesu katika mwenendo wa Maisha yao.
- Inawezekana tumefikia njia panda ya kujiuliza endapo ni sahihi kuendelea kumfuata Yesu na kupoteza baadhi ya fursa ambayo tunaziitaji sana ili kuboresha Maisha yetu ya kiuchumi, au kifamilia, au kikazi au kimahusiano lakini hazina kiwango kinachotakiwa na maelekezo ya Bwana wetu Yesu Kristo.
- Je, ni maneno gani ambayo tunasikia na yanatushawishi kwa sasa katika ufanyaji wa maamuzi yetu ya kila siku? Je, maneno hayo yanaashiria uzima wa milele (kumjua Mungu) au mauti (kutengana na Mungu)?
- Mimi na wewe tunakutana na changamoto nyingi sana za kimaisha, je ni kwa namna gani tunazitatua bila kuathiri uhusiano wetu na Mungu?
- Petro anasema twende kwa nani? Sisi tupo kwa nani mpaka sasa? Tunamkiri Yesu kama Bwana na Mwokozi lakini mioyo yetu ipo mbali naye au karibu naye? hili si suala la watu kuona kwamba bado tunasema Bwana asifiwe lakini ni suala la ndani yetu kama tupo na Yesu mwenye maneno ya uzima ambayo tunayafuata na kuyaishi kila leo.
- Ni maombi yangu kwa ajili yako na kwa ajili yangu kwamba pale tunapokutana na changamoto za kimaisha ambazo zitatuweka njia panda ya kuchagua baina ya maneno ya Yesu Kristo au maneno ya changamoto husika, basi tujaliwe neema kama ya wale thenashara ya kusema twende kwa nani Bwana, wewe Yesu unayo maneno ya uzima wa milele kwa ajili yangu.
MAOMBI LEO
Ndugu yangu ikiwa ndani yako unashuhudiwa bado huna uhakika wa maisha yako na kumjua Mungu ipasavyo, ujue unahitaji ufahamu huo kupitia uzima wa Mungu kuingia ndani yako. Karibu ufuatane nami katika kuomba maombi haya ili uzima wa Mungu ukae ndani yako sasa;
‘Ee Mungu Baba ninakushukuru kwa neno lako la uzima, asante kwa sadaka ya Mwana wako Yesu Kristo pale msalabani kwa ajili yangu. Bwana Yesu ninakiri udhaifu wangu na wasi wasi wangu wa kupotea milele endapo nitaondoka katika maisha haya. Ninaomba unisamehe dhambi zangu zote nilizofanya na hata kuondoa asili ya dhambi ndani yangu, unitakase kwa Damu yako takatifu. Ninaomba ufute jina langu katika kitabu cha hukumu na kuliandika katika kitabu cha uzima. Ninaomba uniokoe na kunifanya upya ndani yangu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Uingie ndani yangu na kuniongoza tangu sasa na hata milele’ Amen.
Ikiwa umefanya sala hii kwa imani, Mungu kwa neema yake amekurehemu na kukusamehe kabisa, hata kama umefanya dhambi yeye ameisafisha na kuisahau. Unapaswa na wewe kujisamehe na kumfuata Yesu tangu sasa.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!