Day.54. Spiritual Food: Je, unataka kuondoka?
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji ni siku nyingine tena tumepewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kujifunza zaidi misingi ya chakula cha kiroho ili kutuwezesha kufanya mapenzi yake na kumtumikia kwa furaha na upendo siku ya leo.
‘Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka?’ Yn.6:67
Mambo ya kujifunza
- Kama tulivyoona katika Makala iliyopita ya kuwa wapo wengi walioanza safari ya kumfuata Bwana Yesu lakini walikwazwa njiani kwa maneno yake na wakaacha kumfuata kabisa. Inawezekana walimfuata Yesu kwa maslahi fulani, au masuala ya dhiki, udhia, udhaifu na kutoona ahadi zikitimia wakachoka njiani.
- Je, vipi kuhusu mimi na wewe leo tupo tayari kuendelea au na sisi tumechoka kumfuata? Mahusiano yetu na Mungu ni jambo linalopaswa kupewa kipaombele cha kwanza katika Maisha yetu ya kila siku.
- Mungu wetu kwa upendo wake alimtoa Yesu Kristo kwa ajili yetu ili kurudisha uhusiano uliokuwa umepotea kwa muda mrefu. Yeye alishafanya sehemu yake na suala la sisi kutambua na kuishi katika kweli hii ni sehemu yetu.
- Fikiria ile safari ya wana wa Israel wakiwa jangwani kwa miaka 40, je wewe na mimi tumeanza safari hii ya kumfuata Yesu kwa kipindi gani mpaka sasa? Je, tumekata tamaa kama wale walivyokata na wengi kuishia jangwani?
- Mungu wetu halazimishi kwetu ili sisi tubaki kumfuata Yeye ila ni suala la hiyari yetu binafsi na kupima ile thamani ya uhusiano wetu na Mungu ndiyo itatuvuta Zaidi katika kushikamana naye kila siku.
- Suala la kuondoka katika uhusiano halihitaji kuzungumza kwani kila mmoja anaweza kusema bado ninaendelea na Yesu, lakini kipimo halisi ni matendo yetu, je tunasoma neno lake na kulifanyia kazi?, je tunapata muda wa kufanya maombi katika Maisha yetu ya kila siku? Je, tunaendelea na uaminifu wetu katika nyanja zote za Maisha iwe kazi, mahusiano, biashara nk
- Kila mmoja wetu anaweza kujitathimini mwenyewe na kuona kama bado yupo katika uhusiano huo mpaka sasa.
MAOMBI LEO
Ndugu yangu ikiwa ndani yako unashuhudiwa bado huna uhakika wa maisha yako na kumjua Mungu ipasavyo, ujue unahitaji ufahamu huo kupitia uzima wa Mungu kuingia ndani yako. Karibu ufuatane nami katika kuomba maombi haya ili uzima wa Mungu ukae ndani yako sasa;
‘Ee Mungu Baba ninakushukuru kwa neno lako la uzima, asante kwa sadaka ya Mwana wako Yesu Kristo pale msalabani kwa ajili yangu. Bwana Yesu ninakiri udhaifu wangu na wasi wasi wangu wa kupotea milele endapo nitaondoka katika maisha haya. Ninaomba unisamehe dhambi zangu zote nilizofanya na hata kuondoa asili ya dhambi ndani yangu, unitakase kwa Damu yako takatifu. Ninaomba ufute jina langu katika kitabu cha hukumu na kuliandika katika kitabu cha uzima. Ninaomba uniokoe na kunifanya upya ndani yangu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Uingie ndani yangu na kuniongoza tangu sasa na hata milele’ Amen.
Ikiwa umefanya sala hii kwa imani, Mungu kwa neema yake amekurehemu na kukusamehe kabisa, hata kama umefanya dhambi yeye ameisafisha na kuisahau. Unapaswa na wewe kujisamehe na kumfuata Yesu tangu sasa.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!