
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji ni siku nyingine tena tumepewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kujifunza zaidi misingi ya chakula cha kiroho ili kutuwezesha kufanya mapenzi yake na kumtumikia kwa furaha na upendo siku ya leo.
‘Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena’ Yn.6:66
Mambo ya kujifunza
- Tunapoianza safari yetu ya kumfuata Yesu inajaa furaha na matumaini mengi sana. Kila mmoja wetu nadahani anaikumbuka sana siku alipoamua kwa dhati ya moyo wake kubadili Maisha ya kumkubali Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wake.
- Tunazikumbuka sana siku za awali jinsi tulivyokuwa tunajitoa kwa kweli na kumfuata Yesu wakati wote. Tunakumbuka tulivyokuwa tukishiriki katika fellowship, makongamano, maombi, kujifunza neno na kushirikiana na wengine wengi katika imani.
- Hatahivyo, kadri siku zinavyosogea tunajikuta tunaanza kupoa na kuona kama vile zile ahadi na ile furaha ya wokovu tuliyoanza nayo haipo tena ndani yetu. Taratibu tunaanza kurudi kule ambao tulidhani tumetoka.
- Hali hii huwakuta watu wengi sana kiasi kwamba huwezi kutofautisha wale wanaosema wameokoka na wa wale ambao hawajaokoka. Kwa bahati mbaya sana wale wanaojinasibu wameokolewa ndio huonekana dhahiri matendo na mwenendo wao kuwa mbaya Zaidi kuliko hata wale wasiookoka.
- Tunasikia kila wakati matendo mabaya yanakithiri ndani ya jamii yetu lakini ukichunguza ni watu ambao wanasema ni walokole.
- Ni kitu gani kimetokea njiani? Yapo mazingira ambayo uchovu wa safari na kukosa Imani kwa kile Bwana Yesu alichosema husababisha kurudi nyuma kwa wengi.
- Watu hukwazwa na matukio ya kushindwa, dhiki, kuona ahadi za Mungu kama hazitimii, majaribu, mifumo ya dunia, nk. Tunapaswa kujua safari hii ni vita wala si kwamba adui atatuacha twende tu bila kuweka upinzani.
- Tunaona hapa baada ya kusikia maneno ya Bwana Yesu wengi wa wanafunzi waliacha kumfuata. Je mimi na wewe tumesikia nini kiasi kwamba tumeacha kabisa kuambatana na Bwana Yesu? Ni wapi tumekwazwa au ni matukio gani katika Maisha yetu yametufanya tuache kumfuata Yesu?
- Leo ni siku ya kuendelea kutafakari safari yetu tangu tulipokutana na Yesu, iwapo bado tunaambatana naye au la? Ni hatua gani tunakwenda kuchukua ili turudi katika kuambatana naye siku zote.
ikiwa bado hujaanza kuambatana na Bwana Yesu katika safari ya maisha yako basi fana sala hii pamoja nami;
MAOMBI LEO
Ndugu yangu ikiwa ndani yako unashuhudiwa bado huna uhakika wa maisha yako na kumjua Mungu ipasavyo, ujue unahitaji ufahamu huo kupitia uzima wa Mungu kuingia ndani yako. Karibu ufuatane nami katika kuomba maombi haya ili uzima wa Mungu ukae ndani yako sasa;
‘Ee Mungu Baba ninakushukuru kwa neno lako la uzima, asante kwa sadaka ya Mwana wako Yesu Kristo pale msalabani kwa ajili yangu. Bwana Yesu ninakiri udhaifu wangu na wasi wasi wangu wa kupotea milele endapo nitaondoka katika maisha haya. Ninaomba unisamehe dhambi zangu zote nilizofanya na hata kuondoa asili ya dhambi ndani yangu, unitakase kwa Damu yako takatifu. Ninaomba ufute jina langu katika kitabu cha hukumu na kuliandika katika kitabu cha uzima. Ninaomba uniokoe na kunifanya upya ndani yangu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Uingie ndani yangu na kuniongoza tangu sasa na hata milele’ Amen.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!