
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji ni siku nyingine tena tumepewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kujifunza zaidi misingi ya chakula cha kiroho ili kutuwezesha kufanya mapenzi yake na kumtumikia kwa furaha na upendo siku ya leo.
‘Lakini kuna wengine miongoni mwenu wasioamini. Kwa maana Yesu alijua tangu mwanzo ni nani wasioamini, naye ni nani atakayemsaliti’ Yn.6:64
Mambo ya kujifunza
- Bwana Yesu anadhihirisha hapa kuhusiana na makundi ya watu ambao walikuwa ni wanafunzi wake ya kuwa wapo ambao si waamini na wengine ni wasaliti.
- Injili inapohubiriwa wapo wengi wanaoambatana na injili husika lakini si wote wana moyo wa kuamini kile kinachosemwa kuhusiana na Bwana Yesu.
- Siku hizi tunashuhudia aina ya mahubiri yanayosisitiza sana mafanikio ya hapa duniani. Injili hizi zinaitwa ‘materialist gospel’ au injili ya vitu. Mkazo wa wahubiri haupo tena katika kuhubiri wokovu, ondoleo la dhambi na maisha ya utakatifu.
- Suala la muhimu sana kwetu sisi tunaopata kulisikia neno la Mungu wakati huu ni kujihadhari na aina ya wanafunzi wa Yesu kwani pamoja na kuonekana tupo wengi lakini ndani yetu wapo wasioamini na wapo wasaliti wa injili.
- Je, ni faida gani tunayoipata katika maisha yetu endapo tutajionesha tupo kwa Yesu lakini mwisho wa siku tusiamini au kumsaliti Bwana Yesu
- Tuna kila sababu ya kuhakikisha tunamfuata Bwana Yesu kwa kuamini mpaka mwisho wa safari ya maisha yetu bila kujali hali tunayopitia au changamoto zozote za kimaisha.
MAOMBI LEO
Ndugu yangu ikiwa ndani yako unashuhudiwa bado huna uhakika wa maisha yako na kumjua Mungu ipasavyo, ujue unahitaji ufahamu huo kupitia uzima wa Mungu kuingia ndani yako. Karibu ufuatane nami katika kuomba maombi haya ili uzima wa Mungu ukae ndani yako sasa;
‘Ee Mungu Baba ninakushukuru kwa neno lako la uzima, asante kwa sadaka ya Mwana wako Yesu Kristo pale msalabani kwa ajili yangu. Bwana Yesu ninakiri udhaifu wangu na wasi wasi wangu wa kupotea milele endapo nitaondoka katika maisha haya. Ninaomba unisamehe dhambi zangu zote nilizofanya na hata kuondoa asili ya dhambi ndani yangu, unitakase kwa Damu yako takatifu. Ninaomba ufute jina langu katika kitabu cha hukumu na kuliandika katika kitabu cha uzima. Ninaomba uniokoe na kunifanya upya ndani yangu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Uingie ndani yangu na kuniongoza tangu sasa na hata milele’ Amen.
Ikiwa umefanya sala hii kwa imani, Mungu kwa neema yake amekurehemu na kukusamehe kabisa, hata kama umefanya dhambi yeye ameisafisha na kuisahau. Unapaswa na wewe kujisamehe na kumfuata Yesu tangu sasa.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!