
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji wa mtandao huu wa isaack zake. Katika kipengele cha maarifa ya kiroho ya Uliza Neno tunakwenda kujifunza mambo mbalimbali yanayoanishwa na neno la Mungu kwa lengo la kutusaidia utu wetu katika safari na majukumu tuliyonayo hapa duniani siku kwa siku. Katika somo lililopita tulijiuliza swali la ‘Je, kwa nini Unamtafuta Yesu?. Leo tunataka kujifunza juu ya kusudi la chakula. Karibu
‘Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha ya watu’ Mwa.45:5
Hii ni habari ya Yusufu mara baada ya kujitambulisha kwa ndugu zake kule Misri ambao walimuuza na hatimaye akawa mtu mkuu katika taifa la Misri. Kilichomsaidia Yusufu kupata nafasi hiyo ni uwezo wake wa kutafsiri ndoto na hekima ya kuhifadhi chakula ambacho kiliwasaidia Wamisri na nchi nyingi zilizokubwa na baa la njaa.
Mambo ya kujifunza
- Wanadamu tunakula chakula kila siku, na kwamba maisha yetu hayawezi kutengwa na chakula.
- Swali la msingi la kutafakari siku ya leo ni ‘Kwa nini tunakula chakula?’
- Naamini kila mmoja wetu atakuwa amejibu swali hili na wengi majibu yetu yatakuwa tunafanana ya kuwa ‘tunakula ili tuishi’. Ni sahihi kabisa
- Kama wote tunakubaliana juu ya kula chakula kwa ajili ya kuishi. Swali lingine muhimu ‘tunalisha nini katika utu wetu?’
- Kama tulivyoona katika masomo ya awali ya kwamba utu wetu unahusisha; roho, nafsi na mwili. Tunalisha kitu gani au sehemu gani ya utu wetu kila siku? Ni dhahiri wengi tunaupa mwili wetu kipaombele cha kwanza zaidi ya sehemu nyingine za utu wetu. Mpangilio wa maisha yetu na vipaombele vyetu katika kula vipo tofauti na jinsi Mungu anavyokusudia.
- Roho na nafsi zetu ni sehemu ya utu wetu vinadumu milele tofauti na mwili huu. Huu ni ukweli tunaopaswa kuukubali na kuuishi kila siku.
- Yusufu aliwekwa na Mungu kwa ajili ya kuhifadhi maisha ya watu kimwili wakati ule. Watu wote hawa yaani Wamisri na Mataifa yalioenda Misri kutafuta chakula kile hawapo tena ulimwenguni katika mwili yaani wamekufa, kwa kuwa chakula kile kilikuwa cha mwili tu.
- Yesu Kristo amekuja na yu hai sasa kwa ajili ya kuhifadhi maisha ya wanadamu wote ya sasa katika mwili na katika roho na nafsi kwa umilele.
- Kama tunakiri chakula ni kwa ajili ya kuhifadhi maisha yetu, tunakula nini leo kwa ajili ya nafsi na roho zetu ziweze kuishi?
- Chakula kwa mwili ni kwa muda tu pindi tupo hai katika mwili. Chakula cha nafsi na roho zetu kitokacho kwa Yesu Kristo ni cha milele chenye uwezo wa kutuvusha kutoka kwenye maisha haya hata uzima wa milele
- Tuanze sasa kuweka bidii na mkazo katika kutafuta chakula cha kiroho kwa kumwendea Yesu Kristo kila iitwapo leo kupata chakula hicho.
‘Utupe leo riziki yetu’
Mungu wetu atusaidie katika kutafakari maneno haya na kupata sababu ya msingi ya kumtafuta Bwana Yesu katika kila siku ya maisha yetu.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
Wako katika Bwana Yesu Kristo
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Isaack Zake ni wakili wa kujitegemea na mshauri katika masuala mbalimbali ya sheria za kazi na rasilimali watu, ndoa na sheria za ardhi na mikataba. Isaack Zake ni mwanzilishi wa mtandao wa kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria wa www.ulizasheria.co.tz ni mwandishi wa vitabu na makala mbalimbali kwenye nyanja za kisheria, kijamii, kiuchumi na kiroho na mwalimu wa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia mtandao wa www.isaackzake.co.tz . Isaack Zake pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Uhusiano wa chama cha Waajiri TAACIME – www.taacime.co.tz.
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!