
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji ni siku nyingine tena tumepewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kujifunza zaidi misingi ya chakula cha kiroho ili kutuwezesha kufanya mapenzi yake na kumtumikia kwa furaha na upendo siku ya leo.
‘Basi watu wengi miongoni mwa wanafunzi wake waliposikia, walisiema, Neno hili ni gumu, ni nani awezaye kulisikia?’ Yn.6:60
Mambo ya kujifunza
- Wanafunzi wake Yesu ambao alikuwa anaambatana nao ni wengi zaidi ya wale Thenashara yaani mitume 12. Wanafunzi hawa waliposikia maneno ya Bwana Yesu kuhusiana na chakula cha uzima waliona ni jambo gumu sana kwao kulisikia na kuliishi.
- Ni maeneo gani katika neno la Mungu unalosikia yanakukwaza na kuona ya kuwa ni gumu katika maisha yako kutimia au kutimizwa?
- Zipo changamoto nyingi tunazopitia kimaisha na tunadhani ya kuwa Neno la Mungu haliwezi kutusaidia huko. Maisha yetu ni matokeo ya neno lake pale alipotuumba hivyo hakuna kitu kitakachokuja mbele yetu tushindwe kupata msaada wake kwa sababu sisi ni uzao wake kwa Neno lake.
- Tunahitaji kuweka imani thabiti kwake Bwana Yesu kwa kile anachokisema, kisitusumbue ya kuwa kitafanyika kwa namna gani bali muhimu sana kwetu kuamini kile anachokisema kwa ajili yetu na hakika kitatimizwa.
- Leo hii chukua hatua ya kuamini kile unachosikia kutoka kwake na kisha fanya kulingana na maelekezo ya neno hakika utayaona mabadiliko katika maisha yako.
MAOMBI LEO
Ndugu yangu ikiwa ndani yako unashuhudiwa bado huna uhakika wa maisha yako na kumjua Mungu ipasavyo, ujue unahitaji ufahamu huo kupitia uzima wa Mungu kuingia ndani yako. Karibu ufuatane nami katika kuomba maombi haya ili uzima wa Mungu ukae ndani yako sasa;
‘Ee Mungu Baba ninakushukuru kwa neno lako la uzima, asante kwa sadaka ya Mwana wako Yesu Kristo pale msalabani kwa ajili yangu. Bwana Yesu ninakiri udhaifu wangu na wasi wasi wangu wa kupotea milele endapo nitaondoka katika maisha haya. Ninaomba unisamehe dhambi zangu zote nilizofanya na hata kuondoa asili ya dhambi ndani yangu, unitakase kwa Damu yako takatifu. Ninaomba ufute jina langu katika kitabu cha hukumu na kuliandika katika kitabu cha uzima. Ninaomba uniokoe na kunifanya upya ndani yangu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Uingie ndani yangu na kuniongoza tangu sasa na hata milele’ Amen.
Ikiwa umefanya sala hii kwa imani, Mungu kwa neema yake amekurehemu na kukusamehe kabisa, hata kama umefanya dhambi yeye ameisafisha na kuisahau. Unapaswa na wewe kujisamehe na kumfuata Yesu tangu sasa.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!