
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji ni siku nyingine tena tumepewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kujifunza zaidi misingi ya chakula cha kiroho ili kutuwezesha kufanya mapenzi yake na kumtumikia kwa furaha na upendo siku ya leo.
‘Kama vile Baba alie hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi’ Yn.6:57
Mambo ya kujifunza
- Hapa Bwana Yesu anatuonesha msingi wa chakula cha kiroho ambacho yeye amekuwa akila siku zote na matokeo yake kwenye maisha.
- Kuna siku mjaribu alimjia akamwambia ageuze mawe yawe mkate, lakini Bwana Yesu alimweleza mtu hataishi kwa mkate tu bali kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu. Hii ina maana ya kuwa maisha yetu ya kiroho yana nafasi kubwa sana kuhuishwa endapo tunategemea neno la Mungu wakati wote.
- Siri ya Bwana Yesu kuwa hai kwa ajili ya Baba ni kula chakula cha kiroho yaani neno la Mungu wakati wote. Ndio maana kipaombele chake katika huduma ilikuwa kuyatenda mapenzi ya Baba aliye mbinguni na si vinginevyo.
- Leo Bwana Yesu anatuambia juu ya kuwa hai kwa ajili yake kama Yeye alivyokuwa hai kwa ajili ya Baba wa Mbinguni.
- Ili tuweze kuwa hai hatuna budi kufuata mfano wake Bwana Yesu wa kula na kunywa chakula cha uzima. Hii ina maana uhai wetu au siku zetu tunazokaa hapa duniani tunapaswa kuziishi kwa kufuata mapenzi yake Bwana Yesu pekee na si vinginevyo.
- Paulo Mtume anatukumbusha ya kuwa kuishi kwetu ni Kristo na kufa ni faida, hii ina maana kama tupo katika mwili tunapaswa kuishi siku zetu zote ndani ya Kristo na hata kifo kinapokuja bado tutakuwa na faida ya kuwa ndani yake.
- Maisha yetu kwa sehemu kubwa hayaakisi ukweli huu, tunapenda kuishi maisha yetu wenyewe kibinafsi kwa kufuata matakwa yetu, lakini wakati huo huo tukifa tunataka tuwe ndani ya Kristo.
- Si suala la maombi ya watu au namna tulivyoshirikiana na wengine katika nyumba za ibada zitaamua hatma yetu, bali mfumo wa maisha yetu kama tuliishi kwa Kristo basi kifo chetu ndio huwa faida.
- Tunao wajibu wa kufanya maamuzi sasa ya kubadili mwenendo wetu na kuishi ndani ya Kristo sasa ili kufa kwetu kuwe na faida.
MAOMBI LEO
Ndugu yangu ikiwa ndani yako unashuhudiwa bado huna uhakika wa maisha yako na kumjua Mungu ipasavyo, ujue unahitaji ufahamu huo kupitia uzima wa Mungu kuingia ndani yako. Karibu ufuatane nami katika kuomba maombi haya ili uzima wa Mungu ukae ndani yako sasa;
‘Ee Mungu Baba ninakushukuru kwa neno lako la uzima, asante kwa sadaka ya Mwana wako Yesu Kristo pale msalabani kwa ajili yangu. Bwana Yesu ninakiri udhaifu wangu na wasi wasi wangu wa kupotea milele endapo nitaondoka katika maisha haya. Ninaomba unisamehe dhambi zangu zote nilizofanya na hata kuondoa asili ya dhambi ndani yangu, unitakase kwa Damu yako takatifu. Ninaomba ufute jina langu katika kitabu cha hukumu na kuliandika katika kitabu cha uzima. Ninaomba uniokoe na kunifanya upya ndani yangu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Uingie ndani yangu na kuniongoza tangu sasa na hata milele’ Amen.
Ikiwa umefanya sala hii kwa imani, Mungu kwa neema yake amekurehemu na kukusamehe kabisa, hata kama umefanya dhambi yeye ameisafisha na kuisahau. Unapaswa na wewe kujisamehe na kumfuata Yesu tangu sasa.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!