Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji ni siku nyingine tena tumepewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kujifunza zaidi misingi ya chakula cha kiroho ili kutuwezesha kufanya mapenzi yake na kumtumikia kwa furaha na upendo siku ya leo.
‘Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake’ Yn.6:56
Mambo ya kujifunza
- Si kila chakula anachokula mwanadamu ni cha kumsaidia katika kuboresha maisha yake. Wapo watu wengi wanapata maradhi na hata kupoteza maisha kwa kula vitu ambavyo havina msaada katika miili yao.
- Wapo watu wanakula sumu au wanakunywa sumu kwa lengo la kukatisha maisha yao au kuleta madhara katika utu wao.
- Kama kuna kitu kinaweza kukatisha maisha ya mwanadamu kwa haraka ni kula kitu ambacho ni kinyume na mfumo wa kawaida wa maisha.
- Kama kipo chakula cha kweli na kinywaji cha kweli ina maana kipo chakula na kinywaji cha uongo. Je, mimi na wewe tunakula nini au tunakunywa nini siku ya leo?
- Bwana Yesu anatuambia ya kuwa mwili wake ndio chakula cha kweli na damu yake ndio kinywaji cha kweli. Tukitaka uhakika wa maisha yetu na usalama wetu kila siku tunapaswa kukitafuta chakula cha kweli na kinywaji cha kweli. Tuna sababu ya kupata neno la Kristo kwa ajili yetu ili kutuongoza na kutuwezesha kuishi katika makusudi ya Mungu. Halikadhalika tukitaka kusafishwa na dhambi yote na kuwa na haki mbele zake tunahitaji Damu ya Yesu Kristo kututakasa kila siku.
- Si kila kitu kinafaa kuwa chakula kwetu au kinywaji chetu bali kile ambacho Yesu Kristo anatuambia kila iitwapo leo.
MAOMBI LEO
Ndugu yangu ikiwa ndani yako unashuhudiwa bado huna uhakika wa maisha yako na kumjua Mungu ipasavyo, ujue unahitaji ufahamu huo kupitia uzima wa Mungu kuingia ndani yako. Karibu ufuatane nami katika kuomba maombi haya ili uzima wa Mungu ukae ndani yako sasa;
‘Ee Mungu Baba ninakushukuru kwa neno lako la uzima, asante kwa sadaka ya Mwana wako Yesu Kristo pale msalabani kwa ajili yangu. Bwana Yesu ninakiri udhaifu wangu na wasi wasi wangu wa kupotea milele endapo nitaondoka katika maisha haya. Ninaomba unisamehe dhambi zangu zote nilizofanya na hata kuondoa asili ya dhambi ndani yangu, unitakase kwa Damu yako takatifu. Ninaomba ufute jina langu katika kitabu cha hukumu na kuliandika katika kitabu cha uzima. Ninaomba uniokoe na kunifanya upya ndani yangu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Uingie ndani yangu na kuniongoza tangu sasa na hata milele’ Amen.
Ikiwa umefanya sala hii kwa imani, Mungu kwa neema yake amekurehemu na kukusamehe kabisa, hata kama umefanya dhambi yeye ameisafisha na kuisahau. Unapaswa na wewe kujisamehe na kumfuata Yesu tangu sasa.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!