Day.44. Spiritual Food: Jenga tabia ya kula na kunywa ili upate uzima
Utangulizi
Karibu sana ndugu yangu msomaji ni siku nyingine tena tumepewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kujifunza zaidi misingi ya chakula cha kiroho ili kutuwezesha kufanya mapenzi yake na kumtumikia kwa furaha na upendo siku ya leo.
‘Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho’ Yn.6:54
Mambo ya kujifunza
- Bwana Yesu anatueleza juu ya siri kubwa ya kutusaidia kuvuka katika maisha haya pasipo hofu ya kifo. Wengi wetu tuna hofu juu ya kifo lakini tukijifunza vizuri maneno ya Bwana Yesu yanaweza kutuvusha salama.
- Siri ya maisha ya kudumu au maisha ya milele ipo katika kuula mwili na kunywa damu ya Yesu Kristo. Hapa maandiko yameeleza wazi kabisa juu ya uhakika tulionao katika maisha ya sasa na baadae.
- Utofauti uliopo kati ya watu wanaomfuata Yesu Kristo na wasiomfuata ni katika aina ya chakula wanachokula na kinywaji wanachokunywa. Yesu anasema aulaye na kuinywa damu yake. Hili si jambo la mara moja bali ni la kila siku. Kama tuna ratiba ya kula chakula cha kimwili kila siku basi tuna haja ya kuwa na ratiba ya kupata neno la Kristo na kuoshwa kwa damu yake kila wakati ili kuwa hai.
- Kadri tunavyokula chakula cha mwili wake na kuinywa damu yake tunao uzima wa milele sasa na si baadae. Hivyo hata mauti ya kimwili ikija katika maisha yetu hatuwezi kuogopa kwa sababu ndani yetu tunao uzima. Haleluya.
- Ni jambo la faraja sana hasa tunapotafakari wapendwa wetu waliotangulia mbele za haki kuhusiana na maisha yao endapo walikuwa wanafuatilia ratiba hii ya chakula basi tuna hakika wapo pamoja na Bwana. Kitakachoamua katika maisha yetu kuwa hai na Bwana si sala nyingi zinazofanywa na watu baada ya sisi kuachana na maisha haya bali tabia tuliyojijengea katika maisha yetu ya kula chakula cha kiroho kila siku.

- Hili ni jambo binafsi sana kwa kila mmoja wetu kufanya maamuzi ya msingi siku ya leo, pokea chakula hiki ili kuweka uzima ndani yako.
MAOMBI LEO
Ndugu yangu ikiwa ndani yako unashuhudiwa bado huna uhakika wa maisha yako na kumjua Mungu ipasavyo, ujue unahitaji ufahamu huo kupitia uzima wa Mungu kuingia ndani yako. Karibu ufuatane nami katika kuomba maombi haya ili uzima wa Mungu ukae ndani yako sasa;
‘Ee Mungu Baba ninakushukuru kwa neno lako la uzima, asante kwa sadaka ya Mwana wako Yesu Kristo pale msalabani kwa ajili yangu. Bwana Yesu ninakiri udhaifu wangu na wasi wasi wangu wa kupotea milele endapo nitaondoka katika maisha haya. Ninaomba unisamehe dhambi zangu zote nilizofanya na hata kuondoa asili ya dhambi ndani yangu, unitakase kwa Damu yako takatifu. Ninaomba ufute jina langu katika kitabu cha hukumu na kuliandika katika kitabu cha uzima. Ninaomba uniokoe na kunifanya upya ndani yangu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Uingie ndani yangu na kuniongoza tangu sasa na hata milele’ Amen.
Ikiwa umefanya sala hii kwa imani, Mungu kwa neema yake amekurehemu na kukusamehe kabisa, hata kama umefanya dhambi yeye ameisafisha na kuisahau. Unapaswa na wewe kujisamehe na kumfuata Yesu tangu sasa.
Mungu mwenyewe aliyetuita ni mwaminifu, naye atafanya katika Jina la Mwana wake Mpendwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Amen
‘Utupe leo riziki yetu’
Isaack Zake
Wakili, Mwalimu na Mshauri
Wasiliana na Isaack Zake kwa barua pepe info@isaackzake.co.tz au kwa simu 0713 888 040 kwa ushauri na mafundisho. Mungu akubariki sana
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!